Dar es Salaam. Kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, kimewateua Omar Kumbilamoto na Geofrey Mwanichisye kugombea nafasi ya unaibu meya wa manispaa ya Ilala, Dar es Salaam na Mikindani Mtwara kupitia chama hicho.
Mbali na hilo kimewapendekeza Omary Zubeir Mbwana, Elizaberth Andrea Mihale na Abdulrahaman Makame Shake kugombea nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu ya taifa ya mkoani Kaskazini Pemba visiwani Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Itikadi na Uenezi wa CCM , Hamphrey Polepole imeeleza kikao hicho kimefanyika leo Alhamisi Juni 27, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Mwenyekiti wake, Rais wa Tanzania John Magufuli.
Polepole amesema kikao hicho kiliwapendekeza Makame Omar Makame, Othman Ali Maulid na Suleiman Ame Vuai kugombea ujumbe wa halmashauri kuu ya taifa ya mkoa wa Kusini Unguja.
“Kikao kiliwapendekeza Bakari Msangi, Gerald Munisi na Elipokea Urio kugombea nafasi ya katibu wa siasa na uenezi wa mkoa wa Arusha. Pia kikao kimeridhia kwa kauli moja pendekezo la Kamati Kuu la kumteua Munde Tambwe (Mbunge wa Viti Maalum) kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa,” amesema Polepole.
Mbali na hilo, Polepole amesema kikao wajumbe wa kikao hicho wamepokea na kujadili taarifa ya uhakiki wa mali za chama hicho uliofanyika Zanzibar na kuelekeza sekretarieti ya halmashauri kuu ya taifa kuchukua hatua stahiki za kinidhamu kwa waliohusika na kupeleka mashauri yao kwa kamati ndogo ya usalama, maadili na udhibiti wa nidhamu kwa wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kuhujumu mali za chama.
Pia Soma
- Zitto ataka Bunge kuibana Serikali ya Tanzania kuhusu kukopa
- Tiba asili za barabarani zapigwa marufuku Iringa
- Nyama ya nyumbu yampandisha kortini mtumishi wa hifadhi ya Ikona
- Kiongozi wa mbio za Mwenge amgomea Mkuu wa Wilaya ya Mwanga