Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilichoibeba Yanga hiki

98512 Yanga+picv Kilichoibeba Yanga hiki

Tue, 10 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Udhaifu wa safu ya kiungo ya Simba, uhodari wa kipa Metacha Mnata na juhudi za mchezaji mmoja mmoja ni sababu kuu zilizochangia Yanga kupata ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya watani wa jadi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Licha ya wengi kuipa Simba nafasi ya kushinda kutokana na mwendelezo wa kupata matokeo mazuri katika mechi tano kabla ya mchezo wa juzi, mambo yalikuwa tofauti na wakajikuta wakipoteza huku Yanga ikionyesha kiwango bora uwanjani.

Kwa muda mwingi wa mchezo, Yanga ilionekana kumiliki mpira na kutawala kwa kupiga pasi zilizofikia walengwa kwa usahihi, kutengeneza nafasi na kushambulia lango la Simba.

Haikushangaza kuona Yanga ikimaliza mapema mechi hiyo kwa kupata bao pekee dakika ya 44 kupitia kwa Bernard Morrison aliyefunga kwa mkwaju wa faulo ya moja kwa moja iliyotokana na madhambi aliyochezewa na Jonas Mkude.

Ubora wa safu ya kiungo ya Yanga katika mchezo huo kwa kiasi kikubwa ulichangia kupata ushindi kwani waliunganisha vyema timu, kuvunja na kutibua mipango ya viungo wa Simba na kutengeneza nafasi.

Tofauti na Simba ambayo ilianza na viungo wanne tu ambao kati yao, watatu ni wa kushambulia, Yanga ilianzisha watano ambapo wawili, Feisal Salum na Papy Tshishimbi walicheza nafasi ya kiungo wa chini mbele ya mabeki huku mbele yao wakiwepo viungo washambuliaji watatu Haruna Niyonzima, Mapinduzi Balama na Morrison.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Viungo watano wa Yanga, waliipa ufanisi kwa kupiga pasi zilizofikia walengwa kwa usahihi, kupoka mipira kutoka kwa wachezaji wa Simba na kuunganisha timu jambo lililofanya wawe na uwiano mzuri katika kushambulia na kuzuia.

Wachezaji hao walipopoteza mpira, walihaha kusaka na walipokuwa nao walihakikisha haunaswi kirahisi na wapinzani wao jambo lililowapa wakati mhumu Simba.

Pia mikono ya kipa Mnata nayo ilichangia kupatikana kwa ushindi huo wa Yanga kutokana na kazi nzuri ambayo kipa huyo alifanya katika kulinda lango lake iligeuka mwiba kwa Simba.

Kama sio uhodari wa Mnata kuokoa mashuti aliyoelekezewa na washambuliaji wa Simba, pengine Yanga wangeweza kufungwa idadi kubwa ya mabao katika mchezo huo.

Kipa huyo aliokoa mashambulizi matatu ya ana kwa ana dhidi ya Meddie Kagere na John Bocco ambayo yangeweza kuwapa wapinzani wao mabao.

Kana kwamba haitoshi, Metacha aliwasiliana vyema na safu ya ulinzi, kuipanga timu na kuwakumbusha mabeki kila walipoonekana kuyumba.

Haikushangaza kocha wa timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’, Bakari Shime akisifu kiwango cha Mnata na kudai ndiye aliamua matokeo.

“Kifupi mechi ilikuwa bora kimbinu na kila upande ulicheza vizuri lakini kubwa zaidi kipa wa Yanga, Metacha Mnata ndiye anastahili kuwa mchezaji bora ameokoa hatari ambazo kwa hali ya kawaida zilionekana kuwa mabao,” alisema Shime.

Wachezaji wa Yanga walikuwa na morali wakicheza kwa kujitolea dakika zote na kuonyesha nidhamu ya mbinu jambo lililoiweka salama timu yao dhidi ya Simba.

Wachezaji hao hawakuwa wakipoteza mipira ovyo kama ilivyokuwa kwa Simba na kila mchezaji alitimiza vyema majukumu aliyopewa na benchi la ufundi.

“Ingawa Yanga imeshinda lakini kama wangekuwa watulivu katika kutengeneza mipira ya kufunga wangepata mabao zaidi. Wachezaji walifanya kazi nzuri ya kunyang’anya mipira,”alisema kocha Sekilojo Chambua.

Mchambuzi Ally Mayay alisema kocha wa Yanga Luc Eymael aliizidi Simba kwa kuingia na mbinu tofauti ikiwemo kudhibiti eneo la safu ya kiungo ya Simba ambayo ndio nguvu ya timu hiyo.

“Nilikuwa namfuatilia kocha wa Yanga katika mahojiano yake kabla ya mchezo alionekana alifanya utafiti wa kuwajua wapinzani wake ubora wao uko wapi na alifanikiwa. Eymael alisema Simba ni timu bora kwa mchezaji mmoja mmoja, lakini haina uwezo wa kucheza kitimu udhaifu ambao alitumia kushinda mchezo huo.

Chanzo: mwananchi.co.tz