Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kikosi kipya cha CCM kupambana na nguvu ya ushawishi wa matajiri

11467 Kikos+pic TanzaniaWeb

Mon, 16 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hatua ya Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kuunda Baraza jipya la Wadhamini la chama hicho inaelezwa kuwa ni mkakati wa kukisuka kisije kuelemewa na nguvu ya ushawishi wa matajiri.

Taarifa ya mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inaonyesha kuwa Rais Magufuli alizungumza na wajumbe wa baraza hilo Ikulu ya Dar es Salaam hivi karibuni akiwataka kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Wajumbe hao ni Anna Abdallah (mwenyekiti), John Chiligati, Jaji Mark Bomani, Balozi Daniel Ole Njoolay, Pandu Ameir Kificho, Christopher Gachuma, Dk Haruni Kondo na Hassan Omar Mzee.

Rais alilitaka baraza hilo jipya kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa pamoja na kusimamia mali zote za CCM na jumuiya zake ikiwa ni pamoja na kuzifanyia tathmini ya mara kwa mara.

Pia alilitaka kutoa ushauri juu ya mabadiliko yoyote yanayohitajika katika umiliki wa mali za CCM na kutekeleza majukumu mengine ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

Suala la mali za chama limekuwa likigonga vichwa vya vigogo wa CCM na mwishoni mwaka jana, NEC ya chama hicho iliunda kamati maalumu ya kufuatilia mali za chama hicho ikiongozwa na Dk Bashiru Ally ambaye sasa ni katibu mkuu wa chama hicho.

Katika maelekezo ya Rais Magufuli kwa baraza hilo, alisisistiza kuwa hatarajii kuona dosari za usimamizi wa mali za chama zikiendelea na kulitaka kuhakikisha CCM inanufaika na mali zake na kuachana na utegemezi.

Anna Abdallah alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwateua na kuahidi kwamba watatekeleza majukumu yao kwa umakini kwa masilahi ya CCM.

“Mambo hayatakuwa kama walivyozoea huko nyuma kwamba kila mtu anamiliki kipande chake cha mali za chama, hapana. Mali zote za chama ni mali za Baraza la Wadhamini la CCM,” taarifa ya Msigwa imemnukuu Anna.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema baraza hilo halitakuwa mwarobaini wa udhibiti wa mali za umma.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema baraza hilo ni mkakati mpya wa Rais Magufuli wa kukijenga upya chama.

Lakini alisema, “Haliwezi kuwa mwarobaini wa upotevu wa mali za chama, ila ameona ni vizuri akawa na mfumo mpya au mkakati mpya wa kukijenga chama.”

Alisema licha ya baraza hilo kutawaliwa na wazee waliokulia kwenye chama hicho, kinachotakiwa ni kujua majukumu yao kwa mujibu wa katiba ya chama.

“Wengi wamekulia kwenye chama hicho na hata wakati mambo hayo ya kupotea kwa mali yakitokea walikuwa wanachama humo humo. Nafikiri huo ni mkakati mpya tu wa kujenga chama,” alisema.

Kwa mtazamo wake, mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, Dk Azaveli Lwaitama alisema lengo ni kudhibiti wafadhili wa chama wasije kuleta ushawishi ulio kinyume na matakwa ya chama.

“Mali za chama zinatokana na michango ya wanachama, kama vile wanachama wa Tanu walivyochangia thumni zao na Mzee John Rupia akajazia ili kupigania uhuru,” alisema na kuongeza:

“Nimemwona Gachuma pale, nadhani lengo ni kuwadhibiti matajiri na wafadhili wa chama wasije kuleta ushawishi usiotakiwa kwenye chama.”

Aliongeza pia kuwa muundo wa baraza hilo ni kuweka misingi ya sheria badala ya urasimu katika kutatua kero za chama.

“Pale kuna wataalamu wa sheria kama Jaji Mark Bomani, kazi yao ni kuweka utaratibu na kufuata sheria na kuondoa urasimu usiohitajika kwenye chama. Chiligati yeye ni mzoefu kwenye chama na ni mjamaa, anakijua vizuri chama,” alisema Dk Lwaitama.

Majukumu

Ibara ya 125 ya Katiba ya CCM inatambua kuwapo kwa Baraza la Wadhamini ikisema litakuwa na mwenyekiti anayeteuliwa na mwenyekiti wa CCM kutoka miongoni mwa wajumbe.

Baraza hilo litakuwa na wajumbe wanane waliochaguliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa.

Majukumu ya baraza hilo ni pamoja na kusimamia mali zote za CCM zinazoondosheka na zisizoondosheka, kufanya tathmini ya mara kwa mara ya mali za CCM na jumuiya zake na kutoa ushauri juu ya mabadiliko yanayohitajika katika umiliki wa mali za CCM na jumuiya zake kwa mfano mali zinazostahili kuuzwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz