Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kikosi kazi cha demokrasia chajipambanua kwa hoja tisa

6f276d98d07bd5506eb903a237ff2627 Kikosi kazi cha demokrasia chajipambanua kwa hoja tisa

Fri, 15 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi kazi kilichopo chini ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi kimeainisha masuala makuu tisa ya kuyafanyia kazi.

Masuala hayo makuu yatakayofanyiwa kazi na kikosi hicho kilichoundwa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na kuzinduliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, ni pamoja na mikutano ya hadhara ndani ya vyama vya siasa, masuala yanayohusu uchaguzi na mfumo wa maridhiano ili kudumisha haki, amani, utulivu na Umoja wa kitaifa.

Masuala mengine ni ushiriki wa wanawake na makundi maalumu katika siasa na demokrasia ya vyama vingi vya siasa, elimu ya uraia, rushwa na maadili katika siasa na uchaguzi, ruzuku ya serikali kwa vyama vya siasa, uhusiano wa siasa na mawasiliano kwa umma na Katiba mpya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Kikosi kazi, Sisty Nyahoza, kikosi kazi hicho kinaalika taasisi, kikundi cha watu na mtu yeyote mwenye maoni, mapendekezo au nyaraka kuhusu masuala hayo tisa au mengine yoyote yanayohusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa, yatakayosaidia kikosi hicho kuandaa mapendekezo mazuri yanayotekelezeka.

Alisema maoni na mapendekezo hayo yawasilishwe kwa Kikosi kazi hicho kupitia barua pepe taskforcemaoni@ orpp.go.tz, WhatsApp ujumbe kwenda kwa Katibu wa Kikosi Kazi, 0784 394883; Sanduku la Posta, 2851 Dodoma; au Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyopo Dodoma na Zanzibar, Mbweni Matrekta. Pia, alisema Kikosi kazi kinaandaa utaratibu wa kukaribisha taasisi, vikundi na watu maalumu kuzungumza nao, ili kupata ufafanuzi wa maoni na mapendekezo yao, ili kiweze kutekeleza kazi zake kwa mujibu wa mpango kazi uliopo.

“Mnaombwa kuwasilisha maoni, mapendekezo au nyaraka hizo ndani ya muda wa siku 31 kuanzia jana,” alihimiza Nyahoza.

Desemba 15, 16 na 17, mwaka jana jijini Dodoma, kulifanyika mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini uliofunguliwa na Rais Samia na kufungwa na Dk Mwinyi.

Washiriki wa mkutano huo walipendekeza na serikali ikaridhia kwamba, kiundwe Kikosi kazi ambacho kitachambua maoni na mapendekezo yaliyojitokeza na kuandaa mapendekezo mahususi ambayo yatawasilishwa serikalini kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Desemba 23, mwaka jana kikosi hicho kiliundwa na kilizinduliwa Januari 10, mwaka huu na Dk Mwinyi na kilianza kazi Januari 11, mwaka huu na kinaendelea na kazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live