Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigogo UVCCM awapa wazee mtihani

Sun, 26 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kheri James amewasihi wazee na viongozi wa chama hicho kutumia uzoefu wao kuwajenga na kuwaandaa vijana kuwa viongozi badala ya kuwananga kuwa hawajalelewa, kuandaliwa na kuiva kuwa viongozi.

Akizungumza jijini Mwanza jana wakati wa uzinduzi wa operesheni ya ‘Mwanza ya kijani’ inayolenga kuwahamasisha vijana kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, Kheri alisema vijana wana uwezo wa kufanya makubwa iwapo wataandaliwa, kulelewa na kuelekezwa vyema na wazee.

“Kijana anapofanya makosa anastahili kurekebishwa, kuonywa na kuelekezwa kwa njia za kukuza maadili, lakini viongozi wengine wamekuwa wakiwananga kwenye majukwaa, huu siyo utaratibu wa chama,” alisema.

Hata hivyo, Kheri alikataa kuzungumza na waandishi kufafanua kauli yake.

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally aliwahi kukaririwa katika matukio na maeneo tofauti akisema baadhi ya viongozi vijana wanafanya makosa yanayotokana na kukosa maandalizi ya kushika nafasi za uongozi.

Dk Bashiru aliwahi kuwataja Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na Hussein Bashe wa Nzega kuwa ni viongozi vijana wazuri, wenye udadisi na uwezo wa kujenga hoja, lakini wanafanya makosa yanayohitaji kulelewa, kusimamiwa na kuelekezwa.

Pia Soma

Katibu mkuu huyo wa CCM alirejea kauli hiyo mjini Moshi wakati wa ibada ya mazishi ya Reginald Mengi alipokuwa akimwombea msamaha mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kauli yake kuhusu ugumu wa Wachaga linapofika suala la kutoa fedha.

Akizungumzia operesheni ya “Mwanza ya Kijani”, Kheri aliwataka vijana wa CCM kujitolea kutumia elimu na uwezo wao kukijenga chama chao kwa masilahi ya Taifa.

Chanzo: mwananchi.co.tz