Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kibarua kigumu cha Jokate, Lulandala CCM

Jokate, Lulandala Kibarua kigumu cha Jokate, Lulandala CCM

Tue, 3 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwateua Fakii Lulandala kuwa Katibu Mkuu wa UVCCM na Jokate Mwegelo (Katibu Mkuu Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), imeelezwa kuwa viongozi hao wana kibarua kigumu kukiandaa chama hicho kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa (2024) na Uchaguzi Mkuu (2025).

Viongozi hao pia wana kibarua kigumu cha kujenga mikakati ya ushawishi kwa kundi la vijana ambalo ndilo lina wapiga kura wengi na kuziandaa jumuiya zao kuwa na mvuto dhidi ya vyama vingine.

Ushawishi huo unaakisi takwimu za Ripoti ya Makadirio ya Taifa ya Idadi ya Watu chini ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kuonyesha ifikapo mwaka 2024 Taifa linatarajiwa kuwa na vijana zaidi ya milioni 9.5 wenye umri kati ya miaka 20 hadi 39 ambao huenda wakashiriki uchaguzi mkuu mwaka 2025.

“Uzoefu unaonyesha wazee bado wanaamini vyama vilivyoleta uhuru, lakini vijana wanahitaji mbadala kwa sababu ya changamoto nyingi zilizokosa majibu ikiwamo ajira,”alisema Profesa Mohammed Bakari kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alipozungumza na Mwananchi jana.

Aliongeza: “Kwa hiyo hawa (Jokate na Lulandala) wana mtihani mkubwa licha ya ushawishi wao, ni uteuzi wa kimkakati, sasa viongozi vijana katika vyama vya upinzani hawana kazi kubwa sana kutokana mahitaji ya vijana wenyewe kuonekana wakitafuta mbadala.”

Mtazamo huo unaibuka ikiwa ni siku chache baada ya Halmashauri Kuu ya chama hicho kumteua Jokate kurithi mikoba ya Dk Phillis Nyimbi na Lulandala kurithi mikoba ya Kenani Kihongosi aliyeteuliwa Mkuu wa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida.

Jokate ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe amekabidhiwa jukumu hilo akiwa ni kijana mwenye umri wa miaka 36 na mwenye ushawishi wa wafuasi zaidi ya milioni 8.7 katika ukurasa wake wa Instagram na milioni 1.1 ukurasa wa X na karibu 400,000 Faceboo.

Akitoa uzoefu jana, Mwenyekiti wa zamani wa UWT kati ya 1994 to 2008, Anna Abdalah, alisema anaamini uteuzi huo hususani wa Jokate utaleta mageuzi ya kuongeza wafuasi kwa vijana na wanawake kutokana na ushawishi wake kidijitali.

“Mazingira ya sasa ni tofauti na zama zetu, wakati wetu hata hazikuwa za kisasa. Pia ni mbunifu na kila eneo alipoteuliwa ameonyesha ubunifu,” alisema.

“Pili, nafasi yake ni kiutendaji, ndio eneo sahihi la vijana, wazee hutumika nafasi ya mwenyekiti kama washauri kwani hata mimi katibu wangu Halima Mamuya alikuwa kijana kwa wakati huo.”

Kwa upande wa Lulandala, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Momba Mkoani Songwe, ni kijana aliyekuwa kada wa Chadema, ndani ya umoja wa vijana na sasa anachukua nafasi hiyo ya kiutendaji ndani ya UVCCM iliyokuwa chini ya Kenani Kihongosi kimkakati.

Upinzani wazungumza Wakati CCM ikitueua vijana hao, Katibu wa Baraza la wanawake Chadema (Bawacha) Catherine Ruge jana alisema hawana hofu kwani tayari wana mtaji wa wanawake milioni nne.

“Sisi tunachosubiri waimarishe mfumo wa Tume Huru ya Uchaguzi, tuko kila mkoa, wilaya.Jokate atashawishi mabinti kugombea uongozi ndani kwani miaka mingi iliongozwa na wazee ila sio kujiunga CCM, sisi tulishawekeza siku nyingi kwa vijana ndio sababu ya mtaji mkubwa tulionao,”alisema.

Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chama cha Wananchi (CUF), Salvatory Magafu, alisema hawana hofu na uteuzi huo kutokana na msingi wa mahitaji ya vijana.

“Hao walioteuliwa ni kweli wana ushawishi lakini vijana hawashawishiki kwa umaarufu wa mtu kwa sasa, wameelimika na wanajitambua, wanataka kujua endapo wakienda kuunga mkono CCM watapata suluhisho la changamoto zao? Jibu ni hapana,”alisema Magafu.

Naye Katibu Mkuu wa Ngome ya Vijana ACT Wazalendo, Mwanaisha Mndeme, alisema ushawishi wa Jokate katika jamii hauna uhusiano na mahitaji ya vijana kwa CCM. “Ni kweli vijana wengi wanatamani kuwa kama Jokate lakini Jokate sio CCM, ambayo imebeba mfumo wa maisha yao.

“Huyu Lulandala naona hesabu za CCM hazikuwa sawa kwa vijana, namwona ni mtu mzima sana kwa hiyo ninaamini hatakuwa na ushawishi wowote kabisa,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live