Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya Mbowe yafukiza ubani ndani ya Ukawa

29799 Mbowe+pic TanzaniaWeb

Mon, 3 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katika hali ya kuonyesha ushirikiano wanachama wa CUF upande wa Maalim Seif Sharif Hamad na Chadema wameungana kimyakimya kusikiliza shauri la rufaa ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mhazini wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bavicha), Esther Matiko.

Wanachama hao wa CUF walifika mahakamani hapo kwa ajili ya kufuatilia kesi ya uhalali wa Ibrahim Lipumba ndani ya CUF walijikuta wanaungana na wenzao wa Chadema katika kesi ya jinai inayomkabili Mbowe.

Katika kesi hiyo, Mbowe na Matiko walivuka kikwazo cha kwanza cha rufaa ya dhamana yao baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kukubali kusikiliza rufaa hiyo na kutupilia mbali mapingamizi ya Serikali, uamuzi ambao serikali iliukatia rufaa.

Wakiwa mahakamani hapo wanachama wa CUF wamekuwa wakifuatilia kinachoendelea kwenye shauri la Mbowe na Matiko.

Akizungumza na gazeti hili Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF upande wa Maalim Seif, Mbarara Maharagande alisema pamoja na kuwapo mahakamani hapo kwa kesi yao na Lipumba, pia wanafuatilia rufaa ya Mbowe.

“Tupo hapa hadi muda huu (juzi saa 11:15 jioni), kufuatilia rufaa ya Mbowe,” alisema Maharagande.

Alisema kufuatilia kinachoendelea kwa Mbowe na Matiko ni jambo la kawaida kwanza ni wenzao kwenye upinzani, lakini pili ni Mbowe ni mwenyekiti wao kwenye Ukawa.

Mbali na Maharagande mahakamani hapo wafuasi wa CUF wanaomuunga mkono Maalim walikuwa bega kwa bega na wa Chadema ikiwa ni pamoja na kuingia kwenye chumba cha kusikilizia kesi. “CUF wameungana na Chadema, nawaona wapo hapa pamoja na wanafuatilia shauri la Mbowe,” alisikika mmoja wa watu waliokuwa mahakamani hapo.



Chanzo: mwananchi.co.tz