Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi mkulima kupinga ukomo wa urais kusikilizwa Septemba 24

76096 Ukomopic

Tue, 17 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Septemba 24, 2019 Mahakama Kuu itaanza kusikiliza kesi ya kupinga ukomo wa urais iliyofunguliwa na Dezydelius Mgoya dhidi ya mwanasheria mkuu wa Serikali (AG).

Mgoya, mkulima mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam  amefungua kesi hiyo chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Utekelezaji Haki na Wajibu, Sura ya 3 ya mwaka 1994 na chini ya Ibara ya 30 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Uamuzi wa kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo umetolewa leo mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Kiongozi Eliezer Feleshi; Jaji Benhajj Masoud na Jaji Seif Kulita.

Kabla ya kuendelea kwa maelezo zaidi, Jaji Felesh alimuuliza Mgoya ni mkulima wa mazao gani na kama ana wakili na kujibiwa kuwa ni mkulima wa mihogo, matikiti maji na mboga na katika kesi hiyo hana wakili.

Kesi ya kupinga ukomo wa urais yatinga kortini

Baada ya maelezo hayo wakili wa Serikali, Daniel Nyakiha aliieleza mahakama kuwa walipeleka majibu yao na mapingamizi nane, kutokana na kukosa anuani ya Mgoya, walimpatia nyaraka hizo asubuhi ya leo.

Pia Soma

Advertisement
Baada ya maelezo hayo, Mgoya aliomba apewe siku saba kupitia nyaraka hizo ili aweze kuzijibu.

Jopo la majaji liliridhia ombi la Mgoya na kupanga Septemba 24, 2019 kuendelea na kesi hiyo huku likimtaka mkulima huyo kama atakuwa na majibu ya nyongeza kuhusu hati ya kiapo kinzani ayawasilishe kabla ya siku hiyo.

Mgoya amefungua kesi hiyo chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Utekelezaji Haki na Wajibu, Sura ya 3 ya mwaka 1994 na chini ya Ibara ya 30 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, Mgoya anahoji Ibara ya 40 (2) ya Katiba ambayo inaweka ukomo wa mihula miwili tu ya miaka mitano mitano (10) ya uongozi katika nafasi hiyo ya urais.

Hivyo anaiomba mahakama hiyo itoe tamko na tafsiri ya maana sahihi na athari za masharti ya ibara hiyo.

Pia anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana dhahiri ya masharti ya Ibara ya 42 (2) ya Katiba kwa kuhusianisha na masharti ya Ibara za 13, 21 na 22 za Katiba hiyo. Vilevile anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana ya Ibara hiyo ya 40(2) kwa kuhusianisha na Ibara ya 39 ya Katiba.

Katika hati yake ya kiapo kinachounga mkono kesi hiyo, Mgoya anadai kuwa shauri hilo linatokana na kukinzana kwa ibara mbalimbali katika Katiba ya nchi, ambazo anazitaja kuwa ni Ibara ya 13, 21, 22(2), 39 na 40(2).

VIDEO: Huyu ndiye mkulima aliyeenda kortini kupinga ukomo wa urais

Anafafanua kuwa Ibara ya 13 inatoa usawa mbele ya sheria na kwamba hakuna sheria ambayo itatungwa na mamlaka yoyote nchini, kuweka sharti ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa tahathira yake.

Kuhusu Ibara ya 21 anaeleza kuwa inaweka haki na uhuru wa kushiriki kikamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye, maisha yake na au yanayolihusu Taifa.

Kwa Ibara ya 22 (2) anasema kuwa inaeleza kwamba kila raia anastahili fursa na haki sawa kwa masharti ya usawa, ya kushika nafasi yoyote ya kazi na shughuli yoyote iliyo chini ya mamlaka ya nchi.

Mgoyo anabainisha kuwa ibara hizo zote 13, 21 na 22 (2) zinapatikana katika sehemu ya Tatu ya Sura ya Kwanza ya Katiba, ambazo mtu yeyote anaweza kutafuta nafuu katika mahakama hiyo kuhusu ukiukwaji wake.

Anadai kuwa Ibara ya 40(2) ya Katiba inaweka ukomo wa muda wa mtu kuchaguliwa kuwa rais, kwamba mtu hawezi kuchaguliwa zaidi ya mara mbili kushikilia wadhifa wa urais.

Hivyo anadai kuwa masharti ya ibara hiyo ya 40(2) yanakiuka haki za kikatiba za Ibara za 13, 21 na 22(2) za Katiba hiyohiyo kwa kutoa mihula miwili tu ya raia kuchaguliwa kuwa rais kwa ukomo wa miaka 10 tu.

Mgoya anadai kuwa ukomo uliowekwa chini ya Ibara ya 40 (2) ya Katiba yanakinzana na haki ya kikatiba ya uhuru wa kushiriki katika shughuli za umma kwa kuchagua au kuchaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na usawa mbele ya sheria chini ya Ibara ya 21 na 13. “Kwa msingi huo ninaomba amri ninazoziomba zikubaliwe na mahakama hii.”

Chanzo: mwananchi.co.tz