Mgombea wa nafasi ya urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM ) John Magufuli amewataka wakazi wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam kuchagua wabunge na madiwani wa chama hicho ili wawe kiunganishi na yeye kwenye utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Aidha amemuagiza Waziri wa Maji, Katibu Mkuu wake kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha ifikapo mwezi Desemba mwaka huu wakazi wa kata ya Bonyokwa, Kinyerezi na Kifuru wanapata huduma ya maji safi na salama.
Magufuli amesema hayo muda mfupi uliopita hii leo akiwa katika Kata ya Kinyerezi, akiwa kwenye mwendelezo wa kampeni kuwania kiti hicho na kubainisha kuwa kama wakichagua wabunge na madiwani wa CCM atabaki kuwa na deni kwenye utekelezaji wa yale yote aliyohaidi.
“Madiwani ndio wanakaa maeneo yenye shida hivyo wataniletea matatizo yao moja kwa moja kupitia wabunge wa CCM kama mkiwachagua”amesema Magufuli.