Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli ya Mahanga ya ‘wizi wa kura’ yaibua mjadala

13991 Pic+mahanga TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Arusha. Kauli ya Dk Makongoro Mahanga kwamba alishinda ubunge vipindi viwili vya miaka 10 Jimbo la Ukonga kwa ‘kuiba kura’ akiwa CCM imeibua mjadala mzito.

Dk Mahanga aliongoza Jimbo la Ukonga kwa miaka 10 kuanzia 2000 hadi 2010 kabla ya jimbo hilo kugawanywa na kuanzishwa jipya la Segerea aliliongoza kwa miaka mitano kati ya 2010 na 2015.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamezungumzia kauli ya Dk Mahanga aliyoitoa juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni za ubunge za Chadema Jimbo la Ukonga wakisema imedhihirisha madai ya wadau na wanasiasa kuwa uchaguzi huwa si huru.

Pia, wengine wameeleza kuwa kauli hiyo inamwondolea uaminifu na uadilifu Dk Mahanga, hivyo Chadema imchukulie hatua.

Dk Mahanga alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa kauli hiyo jana alisema ataendelea kusema ukweli ili Watanzania wajue wizi wa kura unavyofanyika.

“CCM nawafahamu, wanawatumia mabalozi kununua kadi za kupigia kura hata mimi walikuwa wananifanyia hivyo na ninashinda,” alisema Dk Mahanga juzi, ambaye aliwahi kuwa naibu waziri kwa miaka 10 kuanzia 2005 hadi 2015.

Dk Mahanga ambaye ni mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Ilala alisema, “Kura zinazoibwa si za Chadema ni za wananchi, wananchi kataeni kuibiwa.”

Lakini akizungumza katika mahojiano na Mwananchi jana, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Benson Bana alisema, “Nadhani amesema yeye na kauli yake inawakilisha yeye alivyo kama Mahanga. Uadilifu na uaminifu wake ni wa kutilia shaka.”

Dk Bana alisema, “(Mahanga) anapaswa kuthibitisha madai hayo na mahali pa kuthibitisha ni mahakamani kwa kuwa alichokisema na kukitenda ni jinai.”

Akifafanua kauli yake jana, Dk Mahanga alisema, “Kile ambacho CCM inakifanya cha kuwatumia mabalozi kuiba kura na wala si mimi moja kwa moja niliyekuwa naiba. Kusema huko hakuniondolei uadilifu au kuaminika kwangu.”

Dk Bana alisema kwa kauli aliyoitoa Dk Mahanga hata alivyohamia Chadema bado uadilifu na uaminifu wake unatiliwa shaka na anapaswa kuhojiwa ikiwamo kuchukuliwa hatua.

“Kwa kauli hiyo, Mahanga aombe kujiuzulu uongozi Chadema kwa kuwa amethibitisha alishirikiana na wezi kuiba, huwezi kuwa na kiongozi mwizi, Chadema wanapaswa kumchukulia hatua kama kweli wanasimamia uadilifu,” alisema Dk Bana.

Juzi, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (siasa na uhusiano wa kimataifa), Ngemela Lubinga alisema Dk Mahanga ni mtu wa kupuuzwa kwa kuwa anaidhalilisha elimu yake.

“Huwezi ku-deal na mtu kama huyo. Yaani anawaambia wananchi kuwa alikuwa anaiba kura? Ili iweje? Anaidhalilisha hata PhD (shahada ya uzamivu) aliyonayo, mtu kama huyo ni wa kuachana naye,” alisema Lubinga.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema mwaka 2010 walifungua kesi mahakamani kupinga matokeo ya Dk Mahanga dhidi ya mgombea wa Chadema, Fredy Mpendazoe lakini walishindwa.

“Chadema hatuwezi kumchukulia hatua (Mahanga), tulichukua hatua mwaka 2010 kwa kufungua kesi mahakamani na alichokisema kimethibitisha madai yetu,” alisema Mrema.

Alisema hatua watakayochukua ni kudhibiti mianya ya wizi kwa kumtumia Mahanga.

Kuhusu hoja ya Dk Bana ya kukichafua chama hicho, Mrema alisema, “Hachafui chama kwa sababu yeye amekiri hadharani na amesema alikuwa mwizi alikokuwa, hivyo amekiri makosa na chama hakina tatizo naye.”

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Onesmo Olengurumwa alisema, “Kauli hii (ya Mahanga) inadhihirisha mambo ambayo wadau wa uchaguzi au upinzani na wanasiasa wanasema uchaguzi kutokuwa huru.”

Olengurumwa alisema vitendo hivyo ndivyo vinavyokatisha tamaa wananchi ya kwenda kupiga kura. “Yaliyokuwa yanasemwa na wadau na wapinzani sasa yanasemwa na wahusika wenyewe, wamekuja kukiri na hiyo ina faida isiyokamilika na ili ikamilike hatua zinapaswa kuchukuliwa madhubuti ili kutokomeza wizi au hujuma katika uchaguzi,” alisema

Alisema hayo yote yatafanikiwa iwapo kutakuwa na Katiba mpya itakayokuwa imebainisha uwapo wa Tume huru ya uchaguzi.

CCM kuzindua kampeni Ukonga

Mbali ya hayo, mgombea wa CCM Jimbo la Ukonga, Mwita Waitara alisema atazindua kampeni Septemba Mosi.

“Mimi ni mbunge ninayeendelea na ninapozungumza na wananchi nasema ninafanya lakini mgombea mwenzangu wa Chadema (Asia Msangi) anasema nitafanya, sasa huoni nimekwisha kushinda tayari,” alisema Waitara aliyekuwa mbunge jimboni humo kwa tiketi ya Chadema kabla ya kujiuzulu na kuhamia CCM iliyompitisha tena.

Mangula, Lowassa kuwa Monduli

Jimboni Monduli CCM na Chadema watazindua kampeni keshokutwa. Uchaguzi mdogo utafanyika Septemba 16 kwa majimbo mawili na kata 23.

Makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula na waziri mkuu wa zamani ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa wanatarajiwa kuzindua kampeni hizo maeneo tofauti jimboni Monduli.

Wakati Mangula atazindua kampeni za CCM, Monduli mjini kumnadi Julius Kalanga aliyekuwa mbunge kupitia Chadema kabla ya kurudi CCM Julai 31, Lowassa atamnadi Yonas Laizer eneo la Mto wa Mbu.

Jana, Katibu wa Uenezi wa CCM Mkoa Arusha, Shaaban Mdoe akizungumza na Mwananchi alisema maandalizi ya uzinduzi wa kampeni yamekamilika.

Kalanga aliyekuwa CCM kabla ya mwaka 2015 alipohamia Chadema na kugombea ubunge alisema amejiandaa kutetea jimbo hilo.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Arusha, Aman Golugwa alisema wamejipanga kuzindua kampeni kwa kishindo

Chanzo: mwananchi.co.tz