Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli ya Bashiru Ally yamuibua Msambatavangu

29385 Bashiru+pic TanzaniaWeb

Thu, 29 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM mkoani Iringa, Jesca Msambatavangu amesema anasubiri barua ya msamaha wa chama hicho, siku moja baada ya katibu wake mkuu, Dk Bashiru Ally kusema wako tayari kusamehe wanachama waliokisaliti.

Msambatavangu ni mmoja wa wenyeviti wanne waliotimuliwa uanachama na Halmashauri Kuu ya CCM Machi 11, 2017 kutokana na tuhuma za kukiuka maadili wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Juzi, Dk Bashiru aliwaambia wanachama mkoani Iringa kuwa CCM imefungua mlango wa msamaha kwa watu walioadhibiwa kwa usaliti.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi jana, Msambatavangu alisema aliandika barua hiyo tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Msambatavangu alisema ameupokea kwa furaha ujumbe wa Dk Bashiru na anaendelea kusubiri uamuzi wa chama hicho kumrejesha.

“Nimepokea vizuri taarifa hiyo, ila kurudi ni uamuzi wa chama maana ni lazima taratibu zifuatwe, vikao vikae ndipo uitwe,” alisema Msambatavangu.

“Mimi niliandika barua tangu mwanzoni mwa mwaka huu, bado sijajibiwa ndiyo nasubiri.” Mbali na wenyeviti hao, CCM ilimfutia uanachama mjumbe wa Kamati Kuu , Sophia Simba, aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake na kumpa onyo Emmanuel Nchimbi (mjumbe wa Kamati Kuu) pamoja na kumsamehe Adam Kimbisa, ambaye pia alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu.

Hata Simba amerudishwa na kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, huku Nchimbi akiteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Brazil.

Juzi akizungumza na wanachama wa CCM mkoani Iringa, Dk Bashiru alisema wanachama wote walioadhibiwa kwa namna moja au nyingine kwa sababu ya kosa au dhambi ya usaliti, wana nafasi ya kusikilizwa.

Aliwataka viongozi wa chama hicho wa ngazi zote Taifa wanaodhani sasa wamejirekebisha na wanakiri kuwa walikosea wawasilishe maombi yao ya msamaha na kwamba watasikilizwa, kupimwa kabla ya uamuzi kutolewa.

Suala la usaliti lilianza kuvuma tangu wakati wa kampeni na wakati fulani Rais Magufuli aliwahi kusema kuna viongozi wanaipigia kampeni CCM mchana na usiku wanakuwa Ukawa.



Chanzo: mwananchi.co.tz