Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Francis Mbatia, amedai kuwa unaoitwa, “mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama chake” uliomsimamisha wadhifa wake, “ni batili.”
“Hakuna mkutano wowote wa Halmashauri Kuu ya NCCR Mageuzi, uliyoitishwa na uongozi wa chama. Kamati Kuu (CC), haijawahi kuitisha mkutano na hivyo, kinachoitwa mkutano wa NEC, ni kitu ambacho siyo halali,” ameeleza Mbatia.
Amesema, atashangaa ikiwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, atabariki maazimio ya mkutano huo.
Amesema, juzi chama chake kilipeleka kwa msajili muhtasari wa kikao cha Kamati Kuu, ambapo pamoja na mengine, kumjulisha kusogezwa mbele kwa Mkutano wa Kamati Kuu na kumsimamisha kazi, Katibu Mkuu, Matha Chiumba.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya chama hicho, Kamati Kuu, iliyokutana mwishoni mwa wiki, iliamua kuusogeza mbele mkutano huo hadi 18 Agosti mwaka huu.