Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Katibu Mkuu CCM atema cheche

CHONGOLO.jpeg Katibu Mkuu CCM atema cheche

Sat, 10 Jul 2021 Chanzo: ippmedia.com

Katika taarifa yao ya kuhitimisha ziara ya siku mbili mkoani Rukwa, wajumbe hao wakiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, wamesema katika kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM ya 2020-2021, hawatamvumilia kiongozi  au  mtendaji  serikalini  atakayekuwa  kikwazo  katika kuitekeleza  kwa ufanisi.

Wajumbe wengine ni Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, ambaye ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Shaka Hamdu Shaka, Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kenani Kihongosi.

Katika  kikao kilichofanyika kwenye ukumbi  wa  Halmashauri  ya  Manispaa  ya Sumbawanga, mkoani humo juzi, Chongolo alisema, ziara yao iliyoanza Julai 7 hadi 8 kutembelea mashina ya CCM, wameshuhudia miradi ambayo thamani ya fedha hailingani na viwango husika.

Chongolo alitoa mfano kwamba hospitali za wilaya za Nkasi na Kalambo, kila moja imepatiwa Sh. bilioni 2.3, lakini ujenzi hauridhishi kwa sababu thamini ya fedha hailingani na kazi iliyofanyika.

Kutokana na hali hiyo ya ovyo, Katibu Mkuu Chongolo alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti, kuhakikisha ndani ya siku zisizozidi 14 ujenzi wa hospitali hizo unalingana na thamani ya fedha na kwamba maelekezo hayo si porojo.

“Tunamaanisha, si kurembaremba, ni lazima tufanye kazi yenye tija,” alisema  Chongolo  katika  kikao  hicho kilichohudhuriwa  na viongozi  na watendaji wa  CCM, viongozi  na  watendaji  wa  serikali, madiwani  pamoja  na wabunge.

“Wananchi wakiona mambo hayaendi, watatuona sisi tunapiga porojo na sisi hatuko tayari kuitwa wapiga porojo,” alionya.

Kero nyingine ambayo wananchi wanakumbana nayo ni ukosefu wa dawa katika hospitali, vituo vya afya na zahanati, licha ya serikali kutoa fedha nyingi kuwezesha wananchi kupata huduma hiyo.

Katibu  Mkuu  atawasiliana  na  Waziri  wa  Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Doroth Gwajima, pamoja na uongozi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), kujua mamilioni ya fedha yanayotolewa kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa dawa yanakwama wapi.

“Tunataka watueleze nani anasababisha mkwamo katika upatikanaji wa dawa. Nasema hivi, sisi viongozi tunawajibu wa kufuatilia na kusimamia thamani ya fedha katika kila eneo,” alisema.

Chongolo alisema kila kiongozi na mtendaji katika chama na serikali anawajibu wa kutimiza wajibu wake kwa kuhakikisha upatikanaji wa tija unakuwapo.

Kuhusu migogoro ya ardhi, Chongolo alimwagiza Mkirikiti pamoja na wakuu wa wilaya za mkoa wa Rukwa kutafuta suluhisho la kero  hiyo,  ambayo  imekuwa ikipoteza muda  mwingi  wa  wananchi,  ambao wangeutumia katika uzalishaji mali.

Kwa upande wa maji alisema  bado  ni  changamoto,  na  kudokeza kwamba ni wakati muafaka kuanza kufikiria kuwa na mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Tanganyika kwa ajili ya Mkoa wa Rukwa.

Chanzo: ippmedia.com