Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Katiba mpya suluhu kero za Muungano’

Katibapic New Madai ya Katiba yamekua yakishamiri

Wed, 27 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Tanzania ikiadhimisha miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wasomi na wanasiasa wameshauri litafutwe suluhisho la kudumu la kero zilizopo.

Muungano huo uliosisiwa Aprili 26 mwaka 1964 umekuwa wa mafanikio makubwa mpaka sasa licha ya changamoto chache zinazoendelea kushughulikiwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wasomi na wanasiasa waliotoa maoni yao kuhusu maadhimisho hayo, walisema faida zikuwa nyingi zaidi changamoto zikimalizwa.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Bakari Mohamed alisema kuna kero katika muundo wa Muungano zinazohitaji majukwaa ya wadau kujadili.

“Tatizo la msingi siyo kwenye masuala ya kiutawala kwa maana ya uendeshaji bali kuna matatizo ya msingi ya muundo wenyewe wa Muungano, mdau mmoja wa Muungano anajulikana, mwingine hajulikani,” alisema.

Profesa huyo alisema suluhu itapatikana kukiwa na muundo wa Serikali tatu zitakazosimamia makubaliano yaliyopo.

Advertisement “Ukiwa na Serikali tatu unakuwa unajua, hii ni ya Tanganyika, hii ni ya Zanzibar na hii ya Muungano na masuala ya kushirikiana,” alisema.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alisema katika miaka 58 ya Muungano, changamoto nyingi zimejitokeza lakini umeendelea kusimama imara.

“Wakati tunaadhimisha miaka 58 ya Muungano, ni muhimu kufanya tafakuri ya kina kutathmini changamoto na fursa ni zipi,” alisema.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema miaka 58 ya Muungano wa Tanzania umepitia misukosuko mingi hasa malalamiko ya wananchi.

Ili Muungano huu uendelee kuwepo na udumu zaidi, alisema ni lazima kero hizo zikabiliwe mapema na suluhu ipatikane.

“Jambo la kufanya ili kuuimarisha Muungano ni kuwasikiliza wenye Muungano wao ambao ni wananchi kujua wanataka nini, wanataka Muungano wa aina gani, na kujiuliza kwa nini malalamiko hayaishi,” alisema Mrema.

Mrema alisema wananchi walisema kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba aina ya Muungano wanaoutaka hivyo kuzishauri mamlaka husika kuyachukua maoni hayo na kuyafanyia kazi ili kuondoa kero zilizopo.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka alisema Tanzania imeundwa kwa utashi, nia njema na shauku ya kuendeleza umoja, udugu na ujirani mwema.

“Uthubutu, utayari na uzalendo waliokuwa nao wakuu wa nchi za Tanganyika na Zanzibar wakati huo ambao ndio waasisi wa Taifa letu ambao ni Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume ndio uliotuachia urithi adhimu na tunu ya Muungano tulionao leo,” alisema Shaka.

Alisema Muungano wa Tanzania umekuwa wa mfano barani Afrika na duniani hivyo kuwataka Watanzania kuulinda na kuuenzi.

“Zimepatikana faida nyingi zinazotokana na Muungano huu wa hiyari wa wananchi wenye udugu na wanaozungumza lugha moja ya Kiswahili zikiwamo za kisiasa, kiuchumi na kijamii,” alisema.

Naye Mhadhiri wa UDSM, Dk Richard Mbunda alisema sifa kubwa ya Muungano wa Tanzania ni kwamba umedumu kwa muda mrefu na uko imara na bado utaendelea kudumu kwa sababu ya utaratibu mzuri wa kupokezana madaraka.

“Kitu pekee ambacho kinaleta chokochoko kwenye muungano ni pale tu hatuzingatii kupeleka maendeleo pande zote za Muungano lakini Serikali ikisimamia, miradi ya maendeleo ikafanyika, naamini kabisa watu watapenda kuwa ndani ya Muungano,” alisema Dk Mbunda.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza), Profesa Mohamed Makame Haji alisema Muungano ni kielelezo cha umoja kwani nchi tofauti Afrika zilijaribu kuungana lakini hazikufanikiwa hivyo Tanzania kuwa mfano bora.

“Changamoto zipo lakini namna ambavyo tunaona zikiendelea kufanyiwa kazi zinaleta matumaini makubwa,” alisema.

Ali Makame, mchambuzi wa siasa Zanzibar alisema bado Wazanzibari wanaona wanatengwa kwa sababu mambo makubwa yote kufanyika Tanzania Bara.

“Kiuhalisia yapo mambo mengi ukienda Bara utaona kuna tofauti kubwa na ukifika Zanzibar, kule ipo miradi mikubwa inafanyika lakini ukifika Zanzibar haioni,” alisema.

Makame alitolea mfano madaraja makubwa yaliyojengwa Bara akisema iwapo viongozi wangetaka kuwanyamazisha Wazanzibari basi wangejenga hata daraja la kuiunganisha Tumbatu na Mkokotoni.

Hivi karibuni Waziri wa wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dk Selemani Jafo aliwaambia waandishi wa habari jijini Dodoma kuwa maadhimisho hayo yatafanyika sambamba na uzinduzi wa andiko la historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Imeandikwa na Peter Elias, Jessy Mikofu na Mainda Mhando.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live