Imeelezwa kuwa ni wakati muafaka sasa wa Watanzania kuungana kwenye madai ya Katiba mpya ili kupata wigo wa kupunguza mamlaka ya Rais, kupata Tume huru ya Uchaguzi sambamba na Wananchi kuwa na nguvu ya maamuzi ya kuwawajibisha Viongozi walioko madarakani
Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mch.Peter Msigwa wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Chama hicho uliofanyika eneo la Mganza, Wilaya ya Chato, Mkoani Geita ambapo ameeleza kuwa Katiba iliyoko sasa haimsaidii Mwananchi wa kawaida na imekuwa ikinufaisha kikundi cha watu.
Wachache wenye maslahi binafsi, akitolea mfano nafasi ya Rais kuteuwa Viongozi kwa matakwa yake bila kuulizwa wala kuthibitishwa na chombo chochote jambo ambalo amedai kuwa linatengeneza taswira ya uonevu kwakuwa Viongozi walioteuliwa hawatafanya kazi kwaajili ya Wananchi bali kwa matakwa ya aliyewateuwa
Aidha, Mch. Msigwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyassa aliyeambatana na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Tanzania Bara Tundu Lissu ameendelea kufafanua kuwa kwenye mamlaka mbalimbali za uongozi viongozi wa kuteuliwa wamekuwa na nguvu na madaraka makubwa ya kufanya maamuzi kuliko wale wanaochaguliwa na Wananchi jambo linalotoa majibu ya udhaifu wa Katiba yetu aambayo kiuhalisia Wanaochaguliwa ndio walipaswa kuwa na mamlaka makubwa kwasababu wao ndio wawakilishi wa Wananchi
Itakumbukwa kuwa CHADEMA iko kwenye utekelezaji wa kampeni ya '+255 Oparation Katiba mpya, Okoa Bandari zetu' ikilenga kuendeleza mapambano dhidi ya madai ya Katiba mpya na kuuhamasisha Umma kupinga mkataba wa uwekezaji Bandarini ulioingiwa na serikali ya Tanzania na Dubai hivi karibuni.