MGOMBEA wa Ubunge katika Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, ameahidi kuinua kipato cha mtu mmojammoja na kuongeza kasi ya mzunguko wa fedha jimboni humo ili kukuza kipato cha wananchi.
Alitoa ahadi hiyo kwa wapigakura wa jimbo hilo katika ufunguzi wa kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu uliofanyika Uwanja wa Kata ya Ngokolo na kusisitiza kuwa, tatizo kubwa katika jimbo hilo ni kipato kwa watu na mzunguko wa mdogo wa fedha.
Kwa mujibu wa Katambi, endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, kazi yake ya kwanza itakuwa kuhakikisha anaishawishi na kuiomba serikali na watu binafsi kuleta taasisi zao ili kuongeza mzunguko wa fedha.
“Tunahitaji kuwa na vyuo vikuu viwili, kwa sababu vikifunguliwa hapa kutakuwepo na mzunguka wa fedha. Serikali itakopesha wanafunzi hao na hivyo, wakazi wa eneo letu watafanya biashara na vijana watapata ajira,” alisema.
Alisema licha ya kuwapo ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, kunahitajika mikakati ya haraka kupata mazao mengine ya chakula na biashara yatakayosaidia kuongeza kipato na mzunguko wa biashara na kuleta picha halisi ya mji huo.
“Shinyanga Mjini ilikuwa ikizalisha tani 10,000 ya mazao, lakini sasa hivi kutokana na juhudi ya serikali iliyopo madarakani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imefikisha uzalishaji wa tani 27,000 katika mazao yote,” alisema.
Katambi alisema kilimo cha biashara kilikuwa kikizalisha tani 600 za mazao, lakini sasa kimefikia tani 1,220 na mkakati wa kilimo umekua na idadi ya watu imeongezeka mjini na hadi zaidi ya 150,000 hivyo mahitaji nayo kuongezeka.
Alisema bado kuna changamoto kwa wakazi wa mji wa Shinyanga ambazo kama atapewa ridhaa ya kuongoza jimbo hilo, atazishughulikia kikamilifu.