Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati ya Bunge yataka taasisi zilipe madeni TBA

33cdbad7b5211b7fdac6ccc60dda1594.png Kamati ya Bunge yataka taasisi zilipe madeni TBA

Wed, 17 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imezitaka taasisi za serikali zilizopanga kwenye majengo ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kulipa madeni zinayodaiwa na wakala huyo ili aendeleze ujenzi wa miradi.

Kamati hiyo imeridhishwa na mradi unaoendelea wa nyumba za Magomeni Kota mkoani Dar es Salaam uliofikia asilimia 93 hadi sasa.

Katika ziara ya kamati kukagua ujenzi wa nyumba hizo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Sulemani Kakoso, alisema wameridhishwa na kazi iliyofanywa na TBA.

"Tumetembelea mradi huu kuona unavyotekelezwa,; tumeridhika na kazi inayofanywa, tunachotaka sasa ni taasisi zote za serikali zilizokodi majengo ya TBA wzilipe pango ili wakala uendelee kutekeleza miradi mingi zaidi," alisema Kakoso.

Alisema TBA imetekeleza mradi huo mkubwa kwa gharama nafuu na kwamba kama ungetekelezwa na wakandarasi wa nje, ungegharimu fedha nyingi.

Kakoso alisema mradi huo ni wa majengo matano huku manne kati ya hayo, kila moja likiwa na ghorofa nane na jengo la tano likiwa na ghorofa tisa.

Mradi huo uliogharimu Sh bilioni 50.58 utazinufaisha kaya 644 zilizokuwa zinaishi hapo awali kwa kuwa zitasaini mkataba kuishi eneo hilo.

Kakoso alisema mradi utaboresha makazi ya wananchi.

Aliagiza Wizara ya Ujenzi na Miundombinu kuhakikisha wote wanaokaimu nafasi TBA wathibitishwe katika nyadhifa zao kama wana sifa na vigezo vinavyotakiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa TBA, Daudi Kandoro, alisema mradi huo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli aliyetaka makazi hayo yaboreshwe.

Meneja wa Mradi wa Magomeni Kota, Bernad Mayemba, alisema mradi ulianza kutekelezwa mwaka 2016 na kupaswa kutekelezwa ndani ya miezi 18. Mradi unatarajiwa kukamilika Aprili 20, mwaka huu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz