Dar es salaam. Kamati Kuu ya Chadema jana ilijifungia ndani kwa zaidi ya saa 10 kujadili masuala mbalimbali ya kitaifa na kichama yaliyojitokeza na yanayotarajiwa kujitokeza katika siku za usoni, ikiwamo ubunge wa Joshua Nassari.
Kikao hicho maalumu cha siku moja chini ya mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kilijadili suala hilo ikiwa ni siku mbili baada ya Mahakama Kuu kukubaliana na uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai wa kumvua ubunge wa Arumeru Mashariki. Nassari ameelezea kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo.
Kwa uamuzi huo, kama Nassari hatakata rufaa, Tume ya Uchaguzi (NEC) ambayo ilizuiwa kufanya taratibu za uchaguzi na mahakama hiyo inaweza kuendelea. Awali, Mahakama Kuu ilizuia kufanyika kwa uchaguzi katika jimbo hilo hadi kesi ya maombi madogo ya kufungua kesi ya msingi kwa ajili ya kutengua uamuzi wa Spika itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Akizungumza na Mwananchi jana, msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alisema kutokana na uzito wa suala hilo hususan kuelekea kwenye vikao vya Bunge la bajeti siku chache zijazo, kamati hiyo italijadili ili kuona ni namna gani litawasilishwa katika vikao hivyo kama sehemu ya mjadala.
“Ni suala ambalo limetokea katika kipindi cha siku mbili - tatu hizi kabla ya kamati kukutana, lakini katika kujadili masuala ya hali ya kisiasa tutaangalia mambo mengi sana ikiwamo hili (kuvuliwa ubunge Nassari),” alisema Makene.
Nassari alifungua kesi namba 22/2019 mahakamani hapo baada ya Spika kuitaarifu NEC kuwa amepoteza sifa za kuwa mbunge kwa kutohudhuria vikao vitatu mfululizo
Vikao ambavyo vilitajwa kuwa Nassari hakushiriki ni vya Septemba na Novemba 2018 na Januari 29 hadi Februari 9 na kwamba ofisi ya Bunge haikuwa na taarifa za mahali alipokuwa.
Makene alisema kamati hiyo ilikutana katika kikao hicho maalumu kujadili na kutoa mwelekeo wa masuala yanayojitokeza ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa katiba ya Chama hicho toleo la 2016 ibara ya 7:7:15 inatoa maelekezo kwa kamati hiyo kukutana kwa ajili ya kujadili na kutoa mwelekeo wa masuala yanayojitokeza kisiasa nchini.
“Katika kipindi hiki kuna matukio mengi yamejitokeza na mengine yatakayojitokeza, kwa hiyo kikao kitajadili na kuangalia ushiriki wake katika mwelekeo wa Taifa ili kugusa mahitaji ya Watanzania.”
Alisema, “baada ya hapo kuna ajenda zitatokana na kikao hiki tutawajulisha na taarifa nyingine zitakazotokana na kikao hiki.”
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinabainisha kuwa kilijadili maandalizi kuelekea vikao vya Bunge la Bajeti litakaloanza wiki ijayo, uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Makene alisema jambo kubwa lililofanyika chini ya Mbowe aliyeshiriki kikao hicho kwa mara ya kwanza tangu alipotoka mahabusu ni kuwashukuru wajumbe wa kamati hiyo na wanachama kwa umoja waliouonyesha alipokuwa mahabusu.