Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu kesho Alhamisi Novemba 7, 2019 kutoa msimamo kuhusu mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Novemba 6, 2019 Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema kabla ya kutoa msimamo, kikao hicho kitakutana na wabunge wote wa chama hicho.
“Tumeitisha kikao cha dharura cha kamati kuu na baada ya kikoa hiki tutakutana na wabunge na kisha tutatoa msimamo wa chama,” amesema Mrema.
Alipoulizwa kikao hicho kitafanyika wapi amesema, “tutaangalia maana wabunge wapo Dodoma, baadaye tutajua kama watakuja Dar es Salaam na kufanyia kikao jijini humo au kitafanyika huko Dodoma.”
Kuanzia Jumanne Novemba 4, 2019 Chadema kimekumbana na kilio cha wagombea wake wengi kuenguliwa katika mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.
Katika mchakato huo kwenye baadhi ya maeneo wagombea wa Chadema wameenguliwa wote huku chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania kikieleza kuwa chanzo ni ukiukwaji wa kanuni na kufanyiwa hujuma.