Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati Kuu ACT yatoa maazimio ya hoja za siri

Act Kamati Kuu ACT yatoa maazimio ya hoja za siri

Tue, 24 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamati hiyo imefikia maazimio hayo kupitia kikao chake kilichofanyika Januari 21 mwaka huu mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, alisema miongoni mwa maazimio hayo ni kutoa maelekezo kwa kamati ya wasemaji wa kisekta wa chama hicho kufanya uchambuzi wa kina wa hali ya kiuchumi na hatua za kuchukua kuukwamua.

Mengine kwa mujibu wa Shaibu ni pamoja na kutoa maelekezo kwa kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe kukamilisha uundwaji wa kamati ya kuisimamia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ili kuiwajibisha na kupaza sauti dhidi ya hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi wa Zanzibar.

Azimio lingine kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, ni kuitaka SMZ kuweka wazi kalenda ya utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti ya vikosi kazi vya demokrasia.

Lingine ni kuitaka serikali kuweka wazi muda wa kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya hususani hatua muhimu za kupitiwa upya kwa sheria ya mabadiliko ya katiba hiyo pamoja na sheria ya kura ya maoni, kuitishwa kwa mkutano wa majadiliano ya kitaifa kuhusu Katiba, kuundwa kwa kamati ya wataalamu wa kuandaa rasimu na kupigwa kwa kura ya maoni.

Alisema Kamati Kuu pia iliitaka SMZ kuweka bayana kalenda na mchakato wa uundwaji wa Tume huru ya Uchaguzi na kutaka maelezo ya kina kuhusu uundwaji wa kamati ya uteuzi ya wajumbe wa Tume za Uchaguzi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wakiwamo mwenyekiti, makamu mwenyekiti, mkurugenzi na upatikanaji wa wajumbe wake.

"Kamati Kuu imeazimia kumtaka Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi kufanya uamuzi juu ya masuala yaliyoachwa kwenye kikosi kazi cha Zanzibar baada ya mashauriano na Makamu wa Kwanza wa Rais wa SMZ kuhusu kura ya mapema na mfumo wa kupatikana kwa kamati ya uteuzi wa wajumbe wa ZEC.

Kuhusu Mwelekeo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), Shaibu alisema Kamati Kuu ilielekeza uamuzi kuhusu suala hilo uwasilishwe kwa barua rasmi kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Rais Mwinyi na kunakiliwa kwa barua hiyo kwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan.

Kamati hiyo pia imeazimia kuwaagiza viongozi wakuu wa chama hicho kuonana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini na serikali zao ili kuwaeleza mwenendo wa sasa aliodai usioridhisha wa SUK.

Shaibu alisema chama chao kinamtaka Rais Mwinyi kuweka wazi ripoti ya kikosi kazi alichokiunda kushughulikia masuala ya demokrasia Zanzibar kama ambavyo imefanyika kwa Rais wa Tanzania.

"Penye nia ya dhati, masuala yanayogusa maslahi ya umma huwekwa wazi, hakuna sababu inayohalalisha kufichwa kwa ripoti ya kikosi kazi.

"Kwa kuwa kwenye vikao mbalimbali Rais wa Zanzibar amekuwa akieleza kuwa hoja za maridhiano zitatekelezwa kwa ufanisi, atakapochaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Kamati Kuu imeweka muda wa utekelezwaji wa makubaliano baina ya Rais Mwinyi na marehemu Maalim Seif Sharif Hamad waliyoyafanya kabla ya ACT-Wazalendo kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, tunataka utekelezaji kwa vitendo wa hoja tatu zilizowasilishwa kwa Rais Mwinyi.

"Mbali na hoja ya kuachiwa huru viongozi wa ACT-Wazalendo waliokuwa mahabusu au wameshikiliwa kwa njia nyingine ambayo imetekelezwa, Kamati Kuu inataka utekelezwaji wa hoja ya kufanyika uchunguzi huru wa kimahakama kuhusu uvunjwaji wa haki za binadamu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kuwapatia fidia waathirika wa uchaguzi huo na kufanyiwa mapitio na mabadiliko mfumo wa uchaguzi na Mahakama wa Zanzibar," Shaibu alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live