Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kama unajipanga kutoa rushwa uchaguzi Serikali za Mitaa utakumbana na haya

76657 Rushwa+pic

Sat, 21 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetoa tahadhari kwa watakaojihusisha na vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Moja kati ya makosa yatakayowatia hatiani wagombea katika uchaguzi huo ni kugawa zawadi kwa wapiga kura.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Septemba 21, 2019 kaimu mkurugenzi mkuu wa Takukuru,  Brigedia Jenerali John Mbungo amesema miongoni mwa makosa ya rushwa wakati wa uchaguzi ni mpiga kura kupewa hongo ili asijiandikishe katika daftari la wapiga kura na kutopiga kura.

Amesema  makosa mengine ni mgombea kujitoa kwenye kinyang’anyiro kwa sababu ya kuhongwa, kuamriwa mtu wa kumpigia kura na kutumia njia za rushwa kuandaa kundi la watu kufanya vurugu kwenye mikutano ya kampeni ili mgombea mwingine asipate fursa ya kujinadi vizuri kwa wapiga kura.

“Wanaotarajia kupiga kura hawapaswi kupokea fulana au kitu chochote ambacho kitahamisha utashi wake wa kumchagua kiongozi anayemtaka, zawadi yoyote yenye lengo hilo iwe, soda, chakula au kusafirishwa ni rushwa,” amesema Mbungo.

Hata hivyo, amesema vyama vina utaratibu wake wa kuvaa sare ambao huwezi kuingiliwa lakini kama sare hizo zitatolewa kwa lengo la kushawishi kupigiwa kura hiyo ni rushwa kwa kuwa ina athiri dhamira halisi ya mtu.

Pia Soma

Advertisement
“Kujua kama mtu amepewa ‘tisheti’ kama rushwa hilo ni jambo gumu kidogo. Tunawasihi wananchi kuwa tayari kufichua wale wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuwa tayari kutoa ushahidi wa katika kesi zinazochunguzwa katika mapambano dhidi ya rushwa ,” amesema Mbungo.

Mbungo amesema Takukuru kwa kuzingatia umuhimu wa mchakato wa kura katika maendeleo ya Taifa ina dhamira ya kuona wananchi wakichagua viongozi waadilifu, wazalendo na wasiojihusisha na rushwa kwa vitendo.

Chanzo: mwananchi.co.tz