Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kalokola amemwita kati JPM 2020, akina Membe wapo wapi?

33045 Kalokola+pic Tanzania Web Photo

Sun, 23 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Lugha ya mchezo, kumwita mtu kati, maana yake ni kuomba pambano. Katika soka kuweka mpira kati ni kuanza mchezo, ama kwa kipenga cha kwanza au baada ya goli kufungwa.

Mtaalamu wa uchumi, Dk Mussa Kalokola ambaye alikuwa mmoja wa waliochukua fomu za kuomba tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili awe mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2015, ameshatangaza azma ya kumpa changamoto Rais John Magufuli katika Uchaguzi Mkuu 2020.

Dk Kalokola amesema ataomba tiketi ya CCM ili awe mgombea urais mwaka 2020. Utaratibu wa CCM ni kumpa heshima Rais aliye madarakani kwa tiketi ya chama hicho, kugombea muhula wa pili bila kupingwa.

Utaratibu huo wa kumpa heshima Rais ya kugombea muhula wa pili bila kupingwa siyo wa kikatiba. Hivyo, hakuna kipingamizi cha kikatiba kwa mwanachama mwingine kuomba ridhaa ya chama ili kimpitishe kugombea yeye badala ya Rais aliye madarakani.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010, aliyekuwa kada wa CCM, John Shibuda, alitangaza kuchukua fomu CCM mbele ya Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete. Baadaye Shibuda hakuchukua fomu, Kikwete alipitishwa kugombea muhula wa pili bila kupingwa.

Mtikisiko CCM ulitokea kuelekea Uchaguzi Mkuu 2005 Zanzibar. Rais wa awamu ya sita wa Zanzibar, Aman Karume, alikuwa akielekea kugombea muhula wa pili, aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, alijitokeza kuchukua fomu.

Kutokana na nguvu kubwa ya kisiasa aliyokuwa nayo Dk Bilal Zanzibar, ilionekana chama kingepata mpasuko. Hivyo, wazee walimuweka chini ili ajitoe. Dk Bilal akajitoa na kumwacha Karume apitishwe kugombea muhula wa pili bila changamoto.

Kalokola amemwita kati JPM

Ni dhahiri kuwa mwaka 2020 Rais Magufuli atagombea muhula wa pili. Cha kuomba ni afya na uhai. Matarajio yalikuwa asingetokea mwana CCM mwingine wa kumpa changamoto. Kalokola amevunja ukimya.

Hoja ya Kalokola ni kwamba utaratibu wa chama chao kumwacha Rais agombee muhula wa pili bila kupingwa ni pale kiongozi anapofungua milango ya kushauriwa na wana CCM wenzake.

Amesema, utaratibu wa kutompinga Rais uliwekewa masharti kuwa lazima wana CCM wawe wanamshauri Rais. Kalokola amedai kuwa vikao vilivyokuwepo huko nyuma vya CCM ambavyo wanachama walikutana na kupitisha ushauri wao kwa Rais hivi sasa hakuna.

Kuiweka hoja ya Kalokola katika ufafanuzi mzuri ni kwamba utaratibu wa kumwacha Rais apite bila kupingwa ni sharti aongoze kwa kufuata ushauri wa wanachama wa chama hicho. Na kwa mtazamo wake ni kuwa sharti hilo Rais Magufuli amelivunja katika uongozi wake.

Na kwa muktadha huo, Kalokola anaona tayari anayo leseni ya kumkabili Rais Magufuli mwaka 2020. Na ameona haina haja kujificha pembeni, ametangaza mapema, anachosubiri ni muda ufike.

Kwa lugha ya mchezo, Kalokola ameshamwita kati Rais Magufuli. Kumpa changamoto Rais aliye madarakani tafsiri yake ni kuwa anaamini yeye atakuwa Rais mzuri kuliko Magufuli.

Akina Membe wapo?

Marekani, wanachama wa Republican, Gavana wa Ohio, John Kasich, Seneta wa Arizona, Jeff Flake na mgombea urais mwaka 2012 kwa tiketi ya Republican, Mitt Romney tayari wameshaweka wazi azma zao za kumpa changamoto Trump, kinyume na utaratibu wao wa kumwacha Rais madarakani atetee muhula wa pili bila kupingwa.

Inashauriwa bora chama kimketishe Rais madarakani na kumlazimisha atangaze kutogombea muhula wa pili, kuliko kuacha ashindane na wanachama wenzake, uwezekano wa kutokea mgawanyiko ndani ya chama ni mkubwa.

Machi 31, 1968, ikiwa ni miezi mitano kabla ya Kongamano la Kitaifa la Chama cha Democrat kumpitisha mgombea urais, Rais wa 36 wa Marekani, Lyndon Johnson alitangaza kutogombea muhula wa pili. Ilielezwa kuwa Johnson alilazimishwa na viongozi wa chama kutangaza kutogombea.

Rais wa 14 wa Marekani, Franklin Pierce, alikutana na changamoto, alipojikuta anapambana na James Buchanan katika uchaguzi ndani ya Democrat. Buchanan alimshinda Pierce kisha akaenda kushinda Uchaguzi wa Rais Marekani mwaka 1856 na kuwa Rais wa 15. Hivyo, si kitu kigeni Rais kushindwa kwenye chama.

Pamoja na yote, inapendeza kama nia ya kugombea ipo, isemwe hadharani na si kunong’ona kwenye korido. Na katika kumpinga Rais madarakani ndani ya chama, inatakiwa kuwe na sababu. Kalokola ameisema sababu yake ya kumwita kati Rais Magufuli mwaka 2020.

Ipo minong’ono kuwa waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, anajipanga kumpa changamoto Rais Magufuli mwaka 2020. Kwamba hiyo ndiyo sababu anatajwa kumhujumu mpaka akaitwa kwenda kujieleza kwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally.

Kama ya Membe yana ukweli au mwingine yeyote ndani ya CCM mwenye nia ya kumpa changamoto Rais Magufuli, afanye kama Kalokola. Wasinong’one koridoni. Minong’ono ndiyo chanzo cha kuonekana wanahujumu wakati kumbe ni haki yao kikatiba.



Chanzo: mwananchi.co.tz