Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaka yake Lissu ajitenga na uchaguzi mdogo

65921 Pic+kaka+lisu

Mon, 8 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Singida. Kaka yake Tundu Lissu, wakili Alute Mughwai amesusa kiaina kushiriki kinyang’anyiro cha ubunge Jimbo la Singida Mashariki baada ya kusema hajaachana na siasa, lakini umri unamsuta.

Alute ambaye ni wakili wa kujitegemea jijini Arusha, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 alijitosa kuwania ubunge wa jimbo hilo tiketi ya CCM lakini akashindwa kupenya kura za maoni.

Hata hivyo, Lissu ambaye ni mdogo wake aliteuliwa na Chadema kupeperusha bendera yake na kuibwaga CCM.

Aliiambia Mwananchi kwa simu jana kuwa kwa sasa umri wake umeenda na anakabiliwa na shughuli za kifamilia, hivyo hatamudu mikimikiki ya kisiasa ila hajaachana nazo.

Kuhusu Lissu, alisema katika uchaguzi huo mdogo hana sifa ya kutetea nafasi yake kwa sababu anatumikia adhabu ya kutenguliwa. “Mdogo wangu atatumikia kutenguliwa kwake hadi Bunge la sasa litalokoma mwakani. Pia, kipindi hicho chote hatalipwa mshahara. Baada ya Bunge kumaliza muda wake na adhabu ya Lissu itaisha,” alisema.

Hata hivyo, alisema katika uchaguzi mkuu ujao, Lissu anaweza kugombea tena ubunge kama atakuwa na sifa ya kuwa Mtanzania kwa kuzaliwa na hajafungwa jela kwa kosa lolote la jinai.

Pia Soma

Katika hatua nyingine, Chadema Mkoa wa Singida imesema haitashiriki uchaguzi huo kwa sababu kuna viashiria vya kutokuwa wa haki na uwazi.

Akizungumza kwa simu jana, mwenyekiti Chadema Wilaya ya Ikungi, Omari Toto alisema jimbo hilo lina vijiji 51 hivyo ni vigumu kwa siku 11 zilizotangazwa za kampeni kufikia kila kijiji.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ikungi, Mika Likapakapa alisema wamejipanga vyema kurejesha jimbo hilo akisema pia wana uhakika wa kuzoa nafasi zote kwenye uchaguzi wa serikali za vijiji na mitaa.

Alisema uchaguzi wowote ndani ya CCM ukimaliza muda, huwa ni mwanzo wa mwingine.

Chanzo: mwananchi.co.tz