Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kada wa CCM adai chama kimekosa fursa ya kumshauri Rais Magufuli

31890 Ccm+pic Dk Mussa Muzamili Kalokola

Mon, 17 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbio za urais ndani ya CCM kwa mwaka 2015 zilizokuwa na watia nia 42, zilimuibua kada wa chama hicho mkoani Tanga, Dk Mussa Muzamili Kalokola aliyekuwa miongoni mwa wana CCM waliochukua fomu kuomba ridhaa ya chama kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano. Hata hivyo waliorudisha fomu walikuwa 38. Dk Kalokola naye hakuweza kurudisha.

Dk Kalokola katika kinyang’anyiro hicho ndani ya CCM alijikuta akipata umaarufu baada ya kupata mkong’oto kwa kupigwa mtama na wanamgambo wa chama hicho, maarufu kama Green Guard kwa madai ya kuingilia mkutano wa kusaka wadhamini uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya Edward Lowassa (wakati huo akiwa CCM).

Mbali na tukio hilo analodaiwa aling’ang’ania kipaza sauti, siku moja kabla hukohuko Tanga kwenye ofisi ya CCM wilaya, alidaiwa kushawishi wagombea wasimdhamini mgombea mwingine Bernard Membe ambaye naye alikuwa amekwenda kutafuta wadhamini.

Huyo ndio Dk Kalokola, kada wa CCM mkoani Tanga na wakati mwingine hujinasibu kukisaidia chama hicho, Mwananchi imefanya mahojiano naye na hoja yake kuu ni kuiomba CCM impe ridhaa ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 ambao Rais Magufuli atakuwa anagombea kipindi chake cha pili.

SWALI… Dk Kalokola tangu kumalizika kwa uchaguzi umekuwa kimya sana, kwa sasa unashughulika na nini?

JIBU. Kama inavyofahamika mimi ni kada wa Chama cha Mapinduzi, mfanyabiashara na mtaalamu wa uchumi hayo yote naendelea kuyafanya, lakini pia naongoza taasisi ya kudumisha fikra sahihi za Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Haya yote nayafanya kwa sababu ndizo shughuli zangu za kila siku sijaacha kukitumikia chama changu cha mapinduzi, sijaacha biashara na kupitia taasisi ya Mwalimu Nyerere nashukuru shughuli zinaendelea.

SWALI. Nini maoni yako kuhusu uchumi wa Tanzania, je unapanda au unashuka?

JIBU. Ninaamini kwamba katika uchumi bado kuna mambo ambayo yanahitaji kurekebishwa na kama hayatafanyika haya Tanzania itakuwa na watu wenye dhiki kuliko wote duniani na hatimaye itakuwa na watu masikini kuzidi wote Duniani.

Mfumo wote umekuwa wa matatizo, vyombo vya fedha havisaidii, analimbikiziwa utitiri wa kodi matokeo yake mtu aliyeajiriwa serikalini anakuwa na pato la kumzidi mtu aliyejiajiri.

Hii inasababisha watu wengi hasa vijana kukimbilia kuajiriwa serikalini wakati enzi zetu sisi tulikuwa tukiacha serikalini tunakwenda kujiajiri wenyewe na maisha yetu yalikuwa yanaonekana bora kuliko ya yule mtu aliyeajiriwa serikalini.

Kwa hivyo mimi naona bado tatizo la uchumi lipo na ni tatizo la mfumo kwa ujumla na hii inatokana na ukweli kwamba tumeacha mwongozo uliopo katika kitabu cha azimio la Arusha na mwongozo wa CCM wa mwaka 1981 ambao ukienda kwenye ofisi za CCM huukuti kwa sababu wameshauficha.

SWALI. Unaonaje mwelekeo wa nchi kwa sasa?

JIBU. Rais wetu John Magufuli kwa kweli katika kipindi kifupi cha utawala wake amejitahidi kusukuma mbele uchumi wa nchi na ameonesha nia ya dhati na ya

kizalendo katika nchi hii kwa hilo lazima tumpongeze na tumsaidie.

Kwa mtazamo wangu naona lawama nyingi zinazoelekezwa kwake ni kwamba analaumiwa kwa matatizo yaliyotengenezwa na awamu zilizopita, kiasi amejaribu lakini hajarekebishika na tunatakiwa kumshauri.

Lakini la kumshauri Rais Magufuli na wote waliopo kwenye uongozi, watambue kwamba kugombea katika uongozi isiwe sababu ya uadui, mtu anayegombea ni kwamba ni mzalendo na ana kitu ambacho anaona labda angepata nafasi angeweza kukibadili.

Kwa hivyo, Rais Magufuli katika mapungufu aliyoyafanya ni kushindwa kuwatumia wale watu ambao walikuwa wamegombea, watu wanafikiria kwamba walikuwa wengi lakini ile ilikuwa ni hazina kubwa.

Kila mmoja katika wale waliogombea alikuwa na ajenga yake kwa hiyo angewatumia huenda ikawa angekuwa Rais bora kuliko wale waliomtangulia, mfano ni Jaji Augustino Ramadhani ambaye katika masuala ya sheria angempa msaada mkubwa.

Sisi wengine ni wataalamu wa uchumi, tunafahamu wapi tulikotoka na wapi tulikosea kuna mfano wa Baba wa Taifa kuna wakati alisema ukigeuka nyuma utageuka jiwe, sisi tulikuwa tukienda na siasa ya ujamaa...akaja

Profesa Ibrahim Lipumba na andiko lake akawachanganya watawala na andiko lake la “PSRC 1995 and beyond “akaja na sera ya ubinafsishaji akaacha ujamaa.

Leo inalaumiwa CCM kwamba iliacha siasa ya ujamaa lakini ukweli ni kwamba Lipumba ndiye aliyetumia usomi wake na kulifikisha Taifa hapa lilipofika na kwa bahati mbaya kila tulipopiga kelele tukionekana hatuna maana.

Kosa kubwa hivyo kosa kubwa analofanya Rais Magufuli ni kuwapa nafasi kubwa Maprofesa na wasomi wa chuo kikuu bado nasisitiza kwamba hawa kazi yao ni kufanya utafiti.

Na matatizo ya kiuchumi nchini yameanzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kwa sababu maadui wa Taifa hili ambao wanajiita wakubwa kutoka nje wanawagharamia wasomi kuandika tafiti na profesa hawezi kupata PhD bila kuandika la kumridhisha aliyempa fedha za kufanya huo utafiti hivyo wanapandikiza mambo ambayo ni potofu.

SWALI. Msimamo wako ukoje kuhusiana na malumbano yanayoendelea ya kudai Katiba mpya?

JIBU. Katika hili la Katiba naunga mkono maoni ya Rais John Magufuli kwamba huu si wakati wa kushughulikia masuala ya Katiba bali ni muda wa kutumia rasilimali tulizonazo kwa kujenga uchumi wa nchi badala ya kutaka Katiba mpya.

Nasema hivi kwa sababu msingi mkubwa wa Katiba ni kwa wale walioapa kuilinda na kila mwananchi kuhakikisha wanaifuata.

Hapa naona kubwa hasa ni kuhakikisha Katiba iliyopo inafuatwa kwa sababu hata yale yanayoelezwa kwamba hayapo kwenye mapungufu hayafuatwi.

Kilichopo ni kujenga tabia ya kufuata na kuheshimu Katiba iliyopo kwanza na tukiona hili limefanikiwa ndipo tuangalie namna ya kufanyia marekebisho baadhi ya vipengele na siyo kuandika Katiba mpya kwa sababu huko pia ni kukiuka katiba kwa mujibu wa sura namba 183.

Ushauri wangu ni kumuomba tume ya kurekebisha sheria (The Law Reform Commission) iwe inazunguka nchi nzima kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu sheria kandamizi.

Tume hiyo ipewe haki na jukumu la kuwasilisha mapendekezo yao kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili bunge lifanye marekebisho husika bila kufungwa kupita kiasi na shinikizo la Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

SWALI. Mwaka 2015 uliingia katika mchakato wa kuomba ridhaa ya chama chako kuteuliwa kuwa mgombea wa urais lakini ukashindwa je bado una nia hiyo kwa siku zijazo?.

JIBU. Kwanza nikurekebishe kwamba mwaka 2015 sikushindwa isipokuwa nilidhulumiwa haki yangu ni kwamba mimi nilichukua fomu nikacheleweshwa Dodoma siku mbili naomba fomu wananinyima mpaka nikaenda polisi kuripoti kwamba nanyimwa fomu ndipo wakanipa, lakini ikawa zimebaki siku nane. Nimekuja Tanga wakanipiga hao walionipiga mpaka leo hawajapelekwa mahakamani.

Wakati narudisha fomu njiani nikakutana na msafara mitatu tofauti wa Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinga,Waziri wa Ethiopia na wa Rais nikajikuta anapoteza muda barabarani.

Ilitakiwa itumike sheria ya Limitation act ambayo inasema kwamba kama kuna kitu chochote kinachokuzuia kufika kwa wakati hizo siku zinaondolewa ningeweza kufika kwa wakati na kurejesha fomu bila wasiwasi.

Kwa hivyo jibu langu ni kwamba nia ya kuwania urais bado ipo na mwaka 2020 nitaingia katika kinyang’anyiro cha kuwania urais kwa sababu yale yaliyonisababisha niwanie mwaka 2015 ya kutaka kila Mtanzania afaidi rasilimali za nchi bado hayajafanyiwa kazi.

SWALI. Ni desturi kwa chama cha CCM kwamba Rais anapomaliza kipindi cha miaka mitano ya awamu yake, wanaCCM humpa nafasi ya mgombea pekee ili amalizie miaka mitano inakuwaje wewe uamue kujitokeza kipindi hiki?

JIBU. Mimi ninachofahamu Rais anapomaliza miaka yake mitano madarakani ni haki yake kikatiba ya nchi na hata katiba ya CCM kuwania tena nafasi hiyo, lakini hainyimi haki wengine kujitokeza kuwania kwa sababu nafasi za kugombea urais ni kila baada ya miaka mitano.

Isipokuwa ndani ya CCM huko nyuma tulikuwa tumeona kwamba itakuwa siyo lazima kutokea upinzani wa kumpinga rais aliyepo madarakani kwa masharti kwamba rais aliyepo madarakani anapaswa kutoa fursa kwa wana CCM kumshauri.

Sasa kama kipindi hiki inaonekana kwamba ushauri kutoka kwa wanaCCM umepungua, vikao vya CCM tulivyokuwa tukivifanya hakuna, vikao vya wazee hakuna, wale watu ambao wana fikra za kusaidia kulivusha Taifa hazipo.

Kwa hiyo siamini kwamba kila mwana CCM amepata fursa ya kumshauri Rais Magufuli. “Mantiki ya kusema kwamba asipingwe baada ya miaka mitano ni kwamba wana CCM mlikuwa mna nafasi ya kumshauri Rais aliyeko madarakani kama unampinga kwanini humshauri wakati yuko madarakani.

Sasa hili atajilaumu yeye mwenyewe kwa sababu hakutoa yeye au wapambe wake hawakutoa nafasi kwa wana CCM kumshauri.

Halafu ameruka mpaka, watu wamehangaika, wamemfanyia kampeni amekuwa Rais, leo anawathamini watu wa vyama vya upinzani ambao mimi katika dini yangu ya Kiislamu inasema kwamba “mtu ambaye hakupendi hawezi kukushauri yaliyo mema.”

Kwa hiyo unamkaribisha mpinzani ambaye hakupendi kwa hiyo yeye atakachofanya akiingia ndani, anaiba siri zenu za CCM na kukihujumu chama.

Mfano, mwindaji anayemtumia mbwa kumkamata swala akishamkamata yule mbwa anafukuzwa kwamba ni haramu, sasa ni kama sisi wana CCM tumehangaika lakini matunda wanafaidi wapinzani.

Kwa namna hiyo naona mheshimiwa Magufuli amekidhoofisha chama na kwa hivyo ili kukijenga chama chetu, ninahitaji kuwania urais mwaka 2020 badala ya kusubiri afikishe miaka 10.



Chanzo: mwananchi.co.tz