Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KALAMU HURU: CCM iache utaratibu wa kusuluhisha mizozo ya ndani kwa kebehi

68050 PIC+KALAMU

Wed, 24 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baada ya makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana kuandika waraka wa malalamiko dhidi ya kada mwenzao anayedaiwa kutumia vyombo vyake vya habari na mitandao ya kijamii kuwakashifu na kuwatuhumu, kibao sasa kimewageukia.

Kinana na Makamba waliandika waraka wao kwenda kwa Baraza la viongozi Wastaafu na Katibu wa Baraza hilo, Pius Msekwa alishawajibu pamoja na mambo mengine akisema ataupeleka kwenye ngazi za chama na wao wajibu mapigo.

Hata hivyo, wakati viongozi wakuu wa chama wakiwa kimya, baadhi ya makada wameibuka na kuanza kuwaponda makatibu hao. Miongoni mwa makada hao ni pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi.

Wote hao wamewakosoa vikali wazee hao, huku pia wakiwataja makada wengine wanaodaiwa kukihujumu chama pamoja na mwenyekiti ambaye ni Rais John Magufuli.

kama hiyo haitoshi, kumekuwa na sauti za simu zilizorekodiwa zinazodaiwa kuwa na makada hao wakipanga njama za kukihujumu chama. Sauti hizo sasa zinachunguzwa na Jeshi la Polisi.

Kwa chama kikongwe na kikubwa kama CCM kingetegemewa kuonyesha staha ya kumaliza mambo yake kwenye vikao, lakini hatuwasikii viongozi wa chama hicho wakizungumza.

Pia Soma

Kwa kuwa Kinana na Makamba walipeleka andiko lao kwenye baraza la viongozi wastaafu, basi wangeitwa na pengine suala lao lingepatiwa ufumbuzi kwenye vikao vya chama.

Wakosoaji wanaibua hoja mbalimbali kwamba, kama ni kupeleka malalamiko hadharani, walianza wastaafu hao. Ni sawa, pengine walikosea kuweka waraka wao kwenye vyombo vya habari, lakini kwa nini kosa lisahihishwe kwa kosa? Kwa nini wasingepewa onyo au adhabu ya kupeleka jambo hilo kwenye vyombo vya habari?

Wengine wamesema viongozi hao wastaafu walisharuhusu tabia wa makada kutoa matamko na kuponda viongozi wengine katika uongozi wao.

Narudi palepale kwamba, kama kosa lilishafanyika huko nyuma, ndiyo uongozi mpya unalirudia ili kulipiza kisasi?

Potelea mbali, hata kama Kinana na Makamba walikosea kutoa tamko lao kwenye vyombo vya habari, lakini hoja zao zimejibiwa? Wao wanalalamika kutukanwa na kuzushiwa na kada mwenzao waliyedai kuwa anatumika. Pengine vikao vya chama vingelichunguza jambo hilo likamalizwa na vikao hukohuko.

Lakini kinachoonekana sasa ni mashindano ya kutoa matamko; kada huyu analipuka hapa, huyu kule, ilimradi kila mtu ni msemaji ndani ya chama.

Kuna wakati katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally alimtaka waziri wa zamani, Bernard Membe afike ofisini kwake akidai kuwa amekuwa akimhujumu Rais Magufuli katika uchaguzi ujao. Lakini baadaye wito ule ukayeyuka kwa sababu ambazo hazikueleweka.

Kilichofuata sasa ni baadhi ya makada wa chama hicho kurusha vijembe kwa Membe na makada wengine wanaodaiwa kukihujumu chama. Makada hao hawaonywi kwa utaratibu unaoonyesha waonyaji wamepata baraka za chama.

Halafu kuna kila dalili kuwa CCM haina demokrasia ndani yake. Kwamba sasa mwanachama hata awe mstaafu serikalini na kwenye chama, akihoji mambo yanavyokwenda, anaonekana kuwa anakihujumu chama. Maana yake hawaruhusiwi hata kukosoana kwenye vikao vyao?

Si dalili njema kwa chama hiki kikongwe, hata kama kiko madarakani. Ni lazima kiwe na nafasi ya kutosha kwa wanachama kukosoana na kupata suluhu.

Chanzo: mwananchi.co.tz