Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jussa apata mpinzani vita ya kumrithi Othman

Jussa Zct.png Jussa apata mpinzani vita ya kumrithi Othman

Fri, 23 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wanachama wa ACT Wazalendo bado wanapiga vikumbo kuwania nafasi mbalimbali za uongozi zikiwa zimesalia siku kabla ya pazia kufungwa rasmi.

Mtifuano zaidi unatarajiwa kwenye nafasi ya mwenyekiti wa chama na ngome ya vijana, na sasa mgombea wa nafasi ya makamu mwenyekiti (Zanzibar), Ismail Jussa naye amepata mpinzani.

Awali, ni Jussa pekee ndiye aliyechukua fomu kuwania nafasi hiyo ambayo kwa sasa inashikiliwa na Othman Masoud, aliyechukua fomu kuwania nafasi ya uenyekiti akichuana na Juma Duni Haji ambaye anatetea wadhifa huo.

Hata hivyo, mapema leo Ijumaa, Februari 23, 2024 kada mwingine Hija Hassan Hija amejitosa kuchukua fomu kuchauana na Jussa.

Hija anayetoka Jimbo la Kiwani Mkoa wa Kusini Pemba, amewahi kuwa mwakilishi kupitia CUF kabla ya kuhama na kujiunga na ACT-Wazalendo.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Hija amesema amechukua fomu akitumia haki yake kidemokrasia kugombea nafasi ya uongozi ndani ya chama.

“Natumia haki yangu na kuna mambo yamenisukuma kugombea nafasi hii na nsio sababu nimechukua fomu. Nataka kueneza hamasa na harakati za ACT kwenye maeneo yote ambayo kwa kiasi kikubwa hamasa ni kama imepotea kwa sasa. Nikichaguliwa nitafanya ziara matawi yote kuzungumza na viongozi na wanachama, lengo ni kukijenga chama chetu.

‘’Kuna shida imejitokeza hivi karibuni suala la utendaji wa chama kuanzia matawi hadi taifa kuna kasoro nyingi zinazohitaji kufanyiwa kazi na sisi wengine tupo tunaweza kuifanya kazi hiyo kwa usahihi,” amesema Hija.

Amesema kwa sasa chama kimebakiwa na mwaka mmoja kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 hivyo, kinahitaji kushinda kwa kura nyingi hivyo, lazima kipate damu mpya na yenye mikakati ya kisasa ya kisiasa.

Hija alijiunga na CUF mwaka 1992 akiwa na miaka 18 tu na mwanafunzi wa Kidato cha tatu katika Sekondari ya Mwambe.

Mwaka 1995 wakati wa vuguvugu la uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi akiwa mwanafunzi wa Chuo cha Ufundi Karume yeye na wenzake 12 walifukuzwa kutokana na kujihusisha na siasa akiwa shuleni.

Hata hivyo, walifungua kesi kupinga uamuzi huo wa chuo kumfukuza ambapo, walishinda lakini hawakurejeshwa kuendelea na masomo.

“Baada ya kufukuzwa chuo, nilianza harakati rasmi za kisiasa nikateuliwa kuwa katibu wa kamati ya uchaguzi jimbo la Kiwani na msaidizi wa mwakilishi jimbo hilo, Haji Ali Machano (sasa marehemu).

Mwaka 2005 alijitosa kuwania nafasi ya uwakilishi kwenye jimbo hilo na kushinda aikilitumika jimbo hilo kwa miaka 15.

Mbali na nafasi hizo, Hija amepata kushinda nyadhifa zingine mbalimbali ndani ya CUF ikiwemo Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kuanzia mwaka 1999-2018 na Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa mwaka 2015-2020.

Kwa sasa Hija ni Katibu wa Habari na Uenezi wa Jimbo la Kiwani. Nafasi zingine za uongozi zinazowaniwa kwenye uchaguzi wa ACT Wazalendo unaotarajiwa kufanyika Machi 5-6, 2024 kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, ni Mwenyekiti wa ACT Taifa ambapo, wagombea ni Othman Masoud na Babu Duni.

Ngome ya Vijana Taifa waliochukua fomu ni Abdul Nondo, ambaye anatetea nafasi yake hiyo na atachuana na Julius Masabo, Petro Ndolezi na Ruqair Nassir huku wote wakiwa na ushawishi mkubwa kwa vijana wa chama hicho. Nafasi ya Kiongozi wa Chama waliochukua fomu mpaka sasa ni Dorothy Semu ambaye atachuana na Mbarala Maharagande. Dorothy ndiye Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Bara) wakati Mbarala akiwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Sheria na Katiba. Ngome ya Wanawake mchuano utakuwa kwa Severin Mwijage na Janeth Rite ambao, wote wamechukua fomu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live