Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jumuiya ya wazazi CCM wakumbushia ombi lao kwa Rais Magufuli

Jumuiya ya wazazi CCM wakumbushia ombi lao kwa Rais Magufuli

Fri, 29 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imekumbushia ahadi ya mwenyekiti wa chama hicho, Rais wa Tanzania John Magufuli juu ya  kuongezea idadi ya wabunge na madiwani wa viti maalum ili jumuiya zote tatu ziwe na uwakilishi sawa.

Mwaka 2017, Rais Magufuli alipokea ombi la jumuiya hiyo la kutaka idadi ya wabunge na madiwani wa viti maalum iwe inatolewa sawa na jumuiya nyingine za vijana na wanawake zilizo ndani ya chama hicho.

Akizungumza katika kongamano maalum la kumpongeza Rais Magufuli na Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein kwa utekelezaji wa ilani ya CCM leo Ijumaa Novemba 29, 2019 jijini Dar es Salaam,  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa,  Dk Edwin Mndolwa amesema jumuiya zote zina nafasi sawa ndani ya chama hicho na wanataka wabunge hao wachaguliwe na baraza kuu la chama hicho.

Amesema wanaomba utekelezaji wa ahadi hiyo ufanyike mapema ili wanachama wake wajulishwe mapema.

"Jumuiya itafurahi utekelezaji ukifanyika mapema ili wanachama wajulishe na tufanye maandalizi mapema," amesema Dk Mndolwa.

Amesema kwa sasa wanao wabunge wawili tu wa viti maalum idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na jumuiya nyingine.

"Sisi ndio tunawajua wawakilishi wetu tunaomba wabunge wa kundi la wazazi wachaguliwe na baraza kuliko sasa wanachaguliwa na Baraza Kuu la Wanawake (UWT)," amesema Dk Mndolwa

Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula amesema ombi hilo amelipokea na atafikisha kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Magufuli.

Chanzo: mwananchi.co.tz