Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Joto la uchaguzi lazidi kupanda Moshi Vijijini

Moshiii 0117280 Joto la uchaguzi lazidi kupanda Moshi Vijijini

Fri, 12 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

 Joto la uchaguzi linazidi kupanda Jimbo la Moshi Vijijini linaloongozwa na Profesa Patrick Ndakidemi (CCM), zikiwa zimebaki siku 700 kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

Kwa utamaduni uliozoeleka wa uchaguzi kufanyika Jumapili ya mwisho ya Oktoba, basi kama utamaduni huo utaendelea, uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaweza kufanyika Oktoba 26, hivyo zimebaki siku 714.

Licha ya viongozi wa CCM kukemea makada wake walionza kusaka udiwani na ubunge mapema, mtifuano katika jimbo hilo sio wa kawaida kwani umefikia hatua ya baadhi ya makada kuchafuana katika mitandao ya kijamii.

Baadhi ya madiwani wa jimbo hilo kutoka CCM, wanadaiwa kujitokeza hadharani kumpinga Profesa Ndakidemi na kutamka waziwazi kuwa hawawezi kufanya naye kazi, lakini kauli zao zinahusishwa na ubunge mwaka 2025.

Hata hivyo, Profesa Ndakidemi alipotafutwa na gazeti hili kama anafahamu kinachoendelea katika jimbo lake, amesema anafahamu na tayari viongozi wa chama Taifa, mkoa na wilaya walishatoa maelekezo na kuonya watu kuacha kampeni kabla ya muda kwa kuwa hatua hiyo inakivuruga chama na kuwachanganya wananchi.

Amesema ni vema wenye nia ya kutafuta ubunge wakawaacha wabunge waliopo madarakani watimize majukumu yao ya kuwatumikia wananchi na wakati ukifika nafasi itatolewa kila mwenye nia akachukue fomu.

“Si jambo jema kuanza kuchafuana kwa sababu ya kusaka ubunge, hili halijengi chama, linabomoa, maana badala ya kuwaza kuwapa watu maendeleo, tunakuwa tunavurugana wenyewe kwa wenyewe, kwa kujitengenezea nafasi,” amesema Profesa Ndakidemi.

“Tusubiri wakati ukifika kila mmoja atoke kuomba nafasi hii...kama viongozi wetu wa chama wanavyosema, watupe muda wabunge tulioko madarakani tutekeleze majukumu yetu, kwani wote ni CCM na tunajenga nyumba moja.”

Jimbo hilo linaloongozwa na Profesa Ndakidemi lina kata 16 na kwa sasa kumeibuka vita kubwa ya baadhi ya makada wanaotafuta ubunge uchaguzi mkuu wa 2025 huku baadhi wakidaiwa kuwarubuni na kuwanunua baadhi ya madiwani.

Hali hiyo imeelezwa na baadhi ya viongozi na makada wa CCM kuwa imesababisha mpasuko unaoweza kukigharimu chama hicho katika uchaguzi mkuu 2025, kama uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki na unaoaminika.

“Hili jambo litatugharimu sana uchaguzi mkuu wa 2025 kama tutaufumbia macho mpasuko unaoendelea. Wasaka ubunge wameanza kutugawa mapema. Wamwache Profesa (Ndakidemi) atekeleze ilani yetu,” amesema kada mmoja.

Kada huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema pale kunapojitokeza watu wanajipitisha jimboni, mbunge aliyeopo anakosa amani na kushindwa kutekeleza ilani, kwani naye akili inahamia huko kama ana mpango wa kutetea kiti hicho.

Mwenyekiti CCM afunguka

Hivi karibuni, katika kikao cha Halmashauri kuu ya wilaya hiyo, mwenyekiti wa CCM wilayani Moshi Vijijini, Sirili Mushi alifichua uwepo wa baadhi ya madiwani ambao wamenunuliwa na kuanza kupita mtaani kumnadi mgombea wao.

Ingawa katika kikao hicho mwenyekiti huyo hakumtaja mbunge anayepingwa na kukejeliwa, lakini taarifa zinaeleza kuwa, vita kubwa ipo katika Jimbo la Moshi Vijijini licha ya kwamba wilaya hiyo ya kichama inalo pia jimbo la Vunjo.

Mwenyekiti amesema kumeibuka makundi ya wanaosaka ubunge wanaowarubuni baadhi ya madiwani ili kuwaunga mkono na kumkataa mbunge aliyepo, lakini tayari chama kimepata video ya mmoja wa madiwani hao.

Mushi amesema  katika video hiyo anasikika diwani huyo akisema hawezi kufanya kazi na mbunge na tayari CCM kimeanza kuchukua hatua kwani hawatakubali watu wachache wakisababishie mpasuko chama hicho tawala.

Amesema hali hiyo inaweza kukigharimu chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 utakaowachagua viongozi wa serikali za vijiji na mitaa na uchaguzi mkuu 2025 na kusisitiza kuwa wanachokifanya ni nje ya maadili ya chama.

“Kumekuwepo na malalamiko ya baadhi ya viongozi wetu hasa madiwani, kununuliwa na kuwabeba watu wameanza kutangaza kugombea ubunge kwenye majimbo yetu, hili limekuwepo muda mrefu na tumelisema muda mrefu,” amesema.

“Tumelisema kwa wanohusika lakini bahati mbaya siku chache zilizopita nililetewa Clip (mkanda) ya diwani mmoja anasema kwamba simtaki mbunge na sitafanya kazi naye. Tumelifuatilia na siye peke yake huyo diwani,” amesema na kuongeza:

“Wapo kama madiwani wanne ambao mmenunuliwa na anayegombea ubunge bila kibali na kabla ya muda anayetaka kumuondoa mbunge aliyeko madarakani kabla ya wakati wake. Amediriki kusema hamtaki mbunge aliyetokana na CCM.

“…ana mbunge wake ambaye anamkampenia na anawaambia watu wengine hiyo lugha ili wamkatae mbunge, hili limeenda kwenye kamati ya siasa tutachukua hatua," alisisitiza mwenyekiti huyo wa CCM bila kuwataja kwa majina.

Vigogo CCM wakuna kichwa

Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya ameitaka kamati ya siasa na halmashauri kuu ya wilaya kuchukua hatua dhidi ya wote wanaokiuka kanuni na taratibu na kwamba endapo watashindwa, watawajibishwa wao.

Katibu huyo ambaye pia alihimiza umoja na mshikamano, miongoni mwa viongozi na wanachama akisema bila umoja na mshikamano hawatavuka na usaliti miongoni mwao hautakoma, alisema ni lazima hatua zichukuliwe mapema.

Amesema kuchukuliwa hatua kwa wavunjifu wa maadili ndio kutasaidia kulinda heshima na nidhamu ya chama akisema, “tunalo tatizo, viongozi hatufahamu kwamba jukumu letu kama viongozi ni kujiandaa ili watu watuone tunafaa”

“Sasa matokeo yake siku hizi tumezusha tabia ya kuwaandaa watu watuone tunafaa. Ili mradi una shilingi mbili, wewe kazi yako ni kwenda kununua vitochi, kuwapa Sh10,000 au S20,000 wakupigie makofi unafaa, uongozi siyo hivyo,” amasema Mabihya.

"Tunawataka chukueni hatua, lazima chama cha mapinduzi kijengwe kwa nidhamu. Acheni kupanga safu. Tunakwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, najua kuna watu wanajiandaa kuweka wenyeviti wao”

“Hao si wenyeviti wa wananchi wala chama, acheni hilo, kwani upangaji wa safu ni uvunjifu wa kanuni, tutachukua hatua,” amesisitiza Katibu huyo wa mkoa.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi alisema kuna madiwani kama 10 ambao wako kwenye utaratibu wa kutafuta mbunge wao, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu na kanuni za chama.

“Wabunge wapo tuwape ushirikiano, tuache kupitapita huko nyuma kuchafuana, na tukijua upo unamtengeneza mbunge wako, wewe diwani na huyo unayemtengeneza wote tutawakata, subirini wakati ufike,” amesema Boisafi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live