Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jopo la vigogo 12 CCM kuwahoji Kinana, Makamba na Membe

88789 CCm+pic Jopo la vigogo 12 CCM kuwahoji Kinana, Makamba na Membe

Tue, 17 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambayo itasikiliza mashtaka yanayowakabili viongozi wa zamani wa chama hicho, inaundwa na wajumbe 12 wazito.

Itakuwa na jukumu la kutekeleza agizo la Halmashauri Kuu ya CCM iliyokutana wiki iliyopita jijini Mwanza na kuazimia kuwa makatibu wakuu wa zamani, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba pamoja na waziri wa zamani, Bernard Membe kufika mbele ya kamati hiyo.

Kwa mujibu wa mabadiliko ya Katiba ya CCM ya mwaka 2017, kamati hiyo ya usalama na maadili ipo chini ya mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli.

Kamati hiyo inatokana na mabadiliko hayo ya katiba ya chama hicho tawala ambapo pia ziliundwa kanuni za uongozi na maadili toleo la 2017 ambazo usimamizi wake unafanywa na kila ngazi ya uongozi ya chama hicho kuanzia tawi hadi taifa.

Kwa mujibu wa katiba hiyo, mbali ya kuongozwa na mwenyekiti wake, Rais Magufuli, katibu wa kamati hiyo ni katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally.

Wajumbe wa kamati hiyo ni makamu wawili wa mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula (Bara) na Dk Ali Mohamed Shein ambaye ni Rais wa Zanzibar. Wajumbe wengine ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, manaibu katibu mkuu wa CCM, Dk Abdallah Juma Mabodi (Zanzibar) na Rodrick Mpogolo (Bara), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na wajumbe wanne wa kamati kuu, wawili kutoka Bara na wawili Zanzibar.

Kamati hiyo itaanza kutekeleza jukumu hilo la Halmashauri Kuu ya CCM iliyokutana wiki iliyopita jijini Mwanza kwa kuwaita Kinana, Makamba na Membe. Watatu hao wameitwa katika kipindi ambacho sauti zao zilisambaa katika mitandao ya kijamii zikizungumzia kupasuka kwa CCM kwa kiwango ambacho hakiwezi kuungika na wakati fulani wakilaumu uongozi kwa kusababisha hayo.

Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa anayedaiwa kutokuwa na uhusiano mzuri na viongozi wa juu wa CCM, itakuwa mara ya pili kufika mbele ya kamati hiyo, lakini wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Mangula. Mara ya kwanza ilikuwa Februari 10, 2014 akiwa na wenzake William Ngeleja (aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini) na Januari Makamba (akiwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).

Wengine walioitwa ni Edward Lowassa na Frederick Sumaye waliowahi kuwa mawaziri wakuu na Steven Wasira aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais.

Kamati hiyo iliwahoji viongozi hao kwa madai ya kukiuka kanuni na kuanza kampeni mapema za kuwania kuteuliwa kugombea urais ndani ya chama hicho. Mapendekezo ya kamati hiyo yaliwasilishwa kwenye kamati kuu na wote walifungiwa kutojihusisha na siasa ndani ya chama hicho kwa miezi 12.

Mbali na Kinana, Makamba na Membe, wengine walioonekana kutofautiana na uongozi wa juu wa CCM walikuwa Nape Nnauye, January Makamba na William Ngeleja, lakini baadaye Rais Magufuli alitangaza kuwasamehe Ngeleja na Makamba walioamua kwenda kuomba msamaha wenyewe. Baadaye Nape alionekana kwenye televisheni akienda Ikulu kuomba msamaha na Magufuli akatangaza pia kumsamehe.

Kinana na Makamba waliwahi kuandika waraka mrefu kwa baraza la wazee wa chama hicho, wakilalamikia kuchafuliwa na mtu mmoja anayejiita mwanaharakati huru wakisema wanashangaa uongozi wa juu wa CCM kuendelea kunyamazia suala hilo.

Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa vigogo wa CCM kuitwa katika kamati ya maadili.

Horace Kolimba ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu alifikishwa katika kamati ya maadili baada ya kutamka kuwa CCM imekosa dira. Aliishiwa nguvu alipokuwa akihojiwa na baadaye kufariki dunia alipokimbizwa hospitali.

Kihistoria CCM imewahi kuwa na makatibu wakuu tisa, Pius Msekwa (1977-1982), Rashidi Kawawa (1982-1990,) Horace Kolimba (1990-1995), Lawrence Gama (1995-1997), Philip Mangula (1997-2007), Yusuf Makamba (2007-2011), Wilson Mukama (2011-2012), Abdulrahman Kinana (2012-2018) na sasa Dk Bashiru Ally kuanzia 2018.

Ukiacha Msekwa na Kawawa wanaofuatia waliondoka kwa misukosuko.

Kolimba aliponzwa na kauli yake ya kuwa CCM imekosa dira, huku Gama akiponzwa na figisufigisu wakati wa uchaguzi mkuu wa 1995 alipokwaruzana na mmoja wa wagombea urais kwa wakati huo. Jakaya Kikwete alimlalamikia kwa kuonyesha upendeleo kwa mgombea aliyekuwa akishindana naye kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM. Kwa maneno ya wengi, Gama alionekana kumpendelea Cleopa Msuya.

Mangula alikuwa mmoja wa makatibu wakuu bora na imara wa CCM, hakuwa na maneno mengi hadharani, alikuwa mtendaji mzuri ndani ya CCM, lakini baada ya Rais wa Awamu ya Nne, Kikwete kuchukua uongozi wa chama, siku hiyohiyo alimuweka pembeni na kumteua Yusuf Makamba.

Kikwete alijaribu kukiokoa chama kwa kuja na sera ya kujivua gamba ambayo ilikuwa matokeo ya utafiti uliofanywa na tume ya Mukama na alimuondoa Makamba aliyekuwa akilalamikiwa kukizamisha chama na kumuweka Mukama ili atekeleze sera aliyoifanyia utafiti.

Mukama hakuwa na nguvu za kisiasa ndani ya CCM na hapakuwa na utayari wa kisiasa wa kumuunga mkono hivyo, Kikwete akalamizika kumuondoa na kumuweka Kinana ambaye anatajwa kuwa katibu mkuu bora katika orodha ya watendaji hao wakuu wa CCM hiyo ikijumlisha uzoefu wake katika uongozi wa Serikali na chama chenyewe.

Sifa zake nyingine ni jinsi alivyokuwa akielewa sera na mahitaji ya chama hicho, kiwango cha juu cha upevu na hekima pamoja na kukubalika kwake na wengi katika ngazi mbalimbali za chama hicho.

Kinana aliamua kukaa pembeni na nafasi yake ikashikwa na Dk Bashiru aliyekuwa mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm).

Dk Bashiru aliteuliwa muda mfupi baada ya kuwasilisha ripoti ya tume iliyoundwa na Rais Magufuli ya kuhakiki mali za chama hicho.

Chanzo: mwananchi.co.tz