Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jokate awapa angalizo wabunge viti maalumu

Jokate Mwegelo Jokate awapa angalizo wabunge viti maalumu

Fri, 27 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT), Jokate Mwegelo amewataka wabunge wa Viti Maalum wanaotokana na jumuiya hiyo, wasiishie kujipendekeza kwa wajumbe pekee, badala yake wahudumie wananchi.

Kauli ya Jokate, inatokana na kile alichoeleza, kumekuwepo na changamoto ya baadhi ya wabunge wa viti maalumu wanaotokana na jumuiya hiyo kuishia kujipendekeza kwa wajumbe wakati wote, badala ya kukutana na wananchi.

Jokate ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam leo, Ijumaa Oktoba 27, 2023 alipozungumza na vyombo vya habari kutoa taarifa ya ziara ya kamati ya Utekelezaji ya UWT iliyofanyika katika mikoa 10 nchini Julai hadi Oktoba mwaka huu.

Amesema katika ziara hiyo, kamati ya utekelezaji imebaini baadhi ya wabunge wa viti maalum hawafanyi mikutano ya hadhara kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Ametaka wabunge wote waliopata nafasi kupitia jumuiya hiyo kuhakikisha wanafanya mikutano ya hadhara kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua, kadhalika wayaseme mazuri ya Serikali.

"Ukipewa dhamana unapewa na CCM lakini sisi UWT tumepewa nafasi katika kuchochea uwakilishi wa wanawake kwenye nafasi mbalimbali za maamuzi, ni vyema tukaondokana na ile kasumba kwamba tunajihusisha na wajumbe pekee," amesema.

Kulingana na Jokate, inashangaza kuona wabunge hao wakijikita kutoa Khanga na vitu mbalimbali kwa wajumbe, lakini wananchi wanaopaswa kuwawakilisha hawawafikii.

"Hatuwezi kupunguza kero za wanawake kama kila siku tunajihusisha na wanawake wale wale, nimeandika barua kusisitiza kwenye hili na naamini maoni yangu yatafanyiwa kazi," amesema.

Katika taarifa yake hiyo, Jokate amesema ziara hiyo imevuna jumla ya wanachama 514,032 waliojiunga na CCM.

Ziara hiyo, amesema imehusisha mikutano 733 ya hadhara katika Kata 750 na Wilaya 62, huku miradi 1,284 ikikaguliwa.

Ametoa msimamo wa jumuiya hiyo, utakapofika wakati CCM inahitajika kutaka mgombea wake wa urais, UWT itakwenda kumchukulia fomu.

"Tumesema wakati ukifika na CCM kitakapohitaji mgombea wa urais, sisi UWT tutakwenda kumchukulia fomu Rais Samua kwa sababu tumeona amefanya kazi kubwa ya kuwaingiza wanawake kwenye nafasi za uongozi," amesema.

Hata hivyo, amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwakani.

"Tunataka wanawake sasa hivi tuingie ulingoni, tusiendelee kuwa wasindikizaji na niwahakikishie UWT haitakuwa kikwazo cha wanawake wanaotaka kugombea, sana sana tutakuwa daraja la kuwasemea," amesema.

Katika hatua nyingine, Jokate ametangaza vikao vikuu vya jumuiya hiyo vinavyotarajiwa kufanyika visiwani Zanzibar, kikiwemo cha sekretarieti, kamati ya utekelezaji na Baraza Kuu la UWT.

Ameeleza tayari timu ya Mwenyekiti na Kamati ya Utekelezaji kuanzia Oktoba 25, umeshaanza kutembelea mikoa mbalimbali ndani ya visiwa hivyo na miradi imetembelewa.

Lakini, amesema mwisho wa vikao hivyo, jumuiya hiyo itafanya tukio kubwa la kusherehekea miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, huku kaulimbiu ikiwa ni 'miaka mitatu ya mafanikio neema ziendelee'.

"Tunaendelea kuwapa moyo viongozi wetu wakuu, kazi wanayofanya ni kubwa, ya kutumika hakuna anayeweza kuwalipa zaidi ya Mungu," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live