Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Job Ndugai ajiweka kando

Ndugai The Young Man Job Ndugai

Mon, 9 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Spika wa Bunge mstaafu, Job Ndugai ametangaza rasmi nia ya kuachana kabisa na siasa pindi awamu ya sita itakapo maliza muda wake 2025.

Amesema hatagombea tena ubunge katika Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma.

Ndugai, alibainisha hayo jana alipokuwa akizungumza kwenye ibada ya kuweka wakfu gari ya Pareshii ya Mtakatifu Michael Kanisa la Aglikana Tanzania Dayosisi ya Mpwapwa.

“2025 sitagombea nafasi ya ubunge tena nastaafu siyo kama nastaafu kwa kushindwa, lakini ni jambo ambalo tayari nilishalipanga kutoka muda mrefu uliopita hivyo tutaendelea kushirikiana kama ambavyo tunashirikiana sasa,”alisisitiza Ndudai.

Kuacha kugombea tena ubunge ni uamuzi wa pili, baada ya kujiuzulu uspika hivi karibuni na nafasi yake kuchukuliwa na Tulia Ackson.

Ndugai ameliongoza jimbo hilo kwa takribani miaka 20 na kufanikiwa kushika nafasi mbalimbali ikiwamo uenyekiti wa bunge, naibu spika na Spika nafasi ambayo alikuwa nayo hadi anajiuzulu Januari 6, mwaka huu.

Sakata la kujiuzulu kwa Ndugai lilianza mapema mwaka huu baada ya mwishoni mwa mwaka jana kusambaa kwa sauti yake kwenye mitandao ya kijamii akipinga serikali kuendelea kukopa.

Katika sauti hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii alisikika akisema kuwa nchi kama itaendelea na mikopo ipo siku itauzwa kutokana na madeni.

Baada ya kujiuzulu kwake bunge lilianza mchakato wa kumtafuta Spika mwingine atakaye chukua nafasi yake ambapo uchaguzi ulifanyika Februari mwaka huu na kumchagua Dk. Tulia Ackson kushika nafasi hiyo na Mussa Azzan Zungu kuwa Naibu Spika. 

Akizungumzia kuhusu gari hiyo iliyonunuliwa kwa kuchangisha michango kwa waumini wa kanisa hilo pamoja na watu mbalimbali alisema anapongeza wote ambao wamehusika kupatikana kwa gari hiyo.

“Tunapaswa kufanya vitu vyetu wenyewe bila kutegemea mtu aje kutusaidia kwani hata maandiko yanasema kuwa tutakula kwa jasho lakini siyo kwa dezo kama yapo maandiko hayo basi inabidi viongozi wa dini waanze kutufundisha, lakini mimi sijawahi kuyaona,” alisema.

Aidha, alisema Watanzania wanapaswa kuondokana na habari ya kutegemea mtu kuja kuwafanyia mambo yao.

Askofu wa Kanisa Aglikana Tanzania Dayosisi ya Mpwapwa, Jacob Chimeledya, alisema ni aibu kuendelea kutegemea wahisani katika kila jambo.

“Ni aibu sisi Watanzania tulivyo na rasilimali za kutosha kuendelea kusubiria wahisani kutoka nje kufanyia mambo yetu ni aibu pia kiongozi wa serikali kuitangaza Tanzania kuwa ni masikini licha ya uwepo rasilimali za kutosha,” alisema Askofu Chimeledya.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka, aliwapongeza waliofanikisha kupatikana kwa gari hiyo ambayo itatumika na kanisa hilo kutatua changamoto za usafiri kila linapo hitajika.

Mtaka, alisema jambo ambalo limefanywa na waumini hao kununua gari bila kusubiri msaada ni jambo  la kuigwa na watu wote.

“Lazima sisi kama waumini tuache kitu ambacho tutaendelea kukumbukwa na kanisa na kuwapa wepesi viongozi wa dini katika mahubiri yetu siyo kutunga uongoo kwenye maziko yetu,” alisema.

Aidha, aliwataka viongozi wa dini kutumia nyumba zao za ibada kuelimisha masuala mbalimbali ya kijamii ikiwamo zoezi la sensa ya watu na makazi Agosti 23, mwaka huu.

“Tanawashukuru viongozi wa dini kwa kutupa ushirikiano katika mambo mbalimbali ikiwamo wakati wa chanjo ya UVIKO-19 na sasa tunapokwenda kwenye sensa tunaomba ushirikiano wenu wa kutosha kufanikisha zoezi hili,” alisema Mtaka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live