Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi Lukuvi anavyotenga muda wa uwaziri na kuhudumia jimbo

32364 Pic+lukuvi Waziri Lukuvi

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni rahisi kwa mbunge ambaye pia ni waziri kujitetea majukumu mengi wakati anaposhindwa kutekeleza ahadi zake jimboni.

Kihalisia ni vigumu kutekeleza ahadi hizo kwa wakati, ikiwa yapo majukumu mengine ya kitaifa yanayokuandama zaidi ya ubunge.

Pamoja na ukweli huo, Mbunge wa Jimbo la Isimani na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi anasema hapati wakati mgumu kutekeleza majukumu yake ya kibunge licha ya kuongoza wizara inayomuhitaji kila wakati.

Anasema kinachomfanya asisahauliwe jimboni kwake ni uwezo wake wa kupanga ratiba za utekelezaji wa kazi zake.

“Nikikanyaga Isimani mimi ni mbunge wenu nakuja kutekeleza ahadi zangu kwenu,” anasema Lukuvi wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Idodi, alipotembelea jimbo hilo kukagua shughuli za maendeleo.

Anasema uwaziri wa sio sababu ya kutotelekeza Ilani ya Uchaguzi ya CCM na ahadi alizotoa wakati alipochaguliwa kuongoza jimbo hilo.

Tangu Oktoba 2015 alipochaguliwa mpaka sasa, mbunge huyo ametumia Sh227. 6milioni kwa ajili ya kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo.

Katibu wa Jimbo la Isimani, Thomas Malenga anasema kati ya fedha hizo Sh66.2 milioni alitoa taslim na zinazobaki alinunua vifaa ikiwamo sementi na bati kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwamo zahanati, vituo vya afya na shule.

“Kwenye ziara hii ametoa Sh11.8 milioni , mifuko ya sementi 1450 na bati 1200,” anasema Malenga.

Katika kijiji cha Malinzanga, Lukuvi aliwaahidi wananchi kuwa Sh200 milioni toka kwa rafiki zake nchini Japan zimeshasainiwa kwa ajili ya ujenzi wa mfereji wa maji ya kumwagilia mashamba katika Kijiji cha Mafuruto.

“Natamani kuona mfereji huu unaanza kufanya kazi Januari ili wananchi wanufaike na kilimo cha umwagiliaji,” anasema Lukuvi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mafuruto, Bahati Kazimoto anasema wanachosubiri wananchi ni kuanza kwa mfereji huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Malinzanga, Lulamso Kadaga anasema licha ya kazi nyingi alizonazo kwenye wizara yake, bado mbunge huyo amekuwa akifanya ziara na kutekeleza ahadi zake kama kawaida jambo wanalojivunia.

“Angekuwa waziri mwingine tusingemuona jimboni, angejitetea si tunamuona kila siku akihangaika na migogoro ya ardhi? lakini wewe unakuja na unatimiza ahadi zako, sisi wananchi wa Isimani tunakuombea,” anasema Kadaga.

Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Iringa Vijijini, Costantino Kihwele anasema kazi ya ubunge sio kubeba vyuma isipokuwa kuwawakilisha wananchi kama anavyofanya mbunge huyo.

“Ni kati ya wabunge wasio wasumbufu na wanaotekeleza ilani kwa vitendo,” anasema Kihwele.

Chanzo chake fedha jimbo

Katika ziara hiyo, Lukuvi aliwaambia wananchi wake licha ya mfuko wa jimbo, fedha anazotumia kwa ajili ya maendeleo ya jimbo lake zinatoka kwa wafadhili.

“Hakuna kazi ngumu kama kuomba misaada kwa watu lakini mimi nimegeuka ombaomba, inabidi nifanye hivyo wananchi mnahitaji maendeleo,” anasisitiza.

Anadai kuwa kinachompa nguvu ya kuomba zaidi misaada hiyo kutoka kwa rafiki na wadau wa maendeleo wa jimbo hilo ni jitihada za wananchi wenyewe katika kujitoa kuchangia shughuli za maendeleo.

“Mnanipa nguvu kiasi kwamba hata ninapoenda kuomba misaada hii sijisikii vibaya japo kuomba ni kazi ngumu kwelikweli, napata tabu,” anasema Lukuvi.

Ujenzi wa barabara

Kwa kuwa jimbo la Isimani limepitiwa na barabara inayoenda Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Lukuvi anasema ahadi ya Serikali kuhusu ujenzi wa barabara ya kwenda hifadhi hiyo kwa kiwango cha lami ipo palepale.

“Niliwaahidi ujenzi wa lami wa barabara hii nafurahi Serikali imechukua jukumu, ikijengwa itachangia sana kuongeza uchumi wa jimbo, vuteni subira,” anasema.

Anaeleza kuwa kinachoendelea sasa ni mazungumzo baina ya Serikali na Benki ya Dunia ili kupata fedha zitakazowezesha ujenzi wa barabara hiyo inayotarajia kugharimu zaidi ya Sh700 bilioni.

“Hii barabara ikijengwa itasaidia kukuza uchumi kwa sababu ndege za watalii sasa zitatua nduli, watatumia magari na kupita kwenye vijiji vyetu. Mtaweza kuuza bidhaa,” anasema.

Magari ya wagonjwa

Lukuvi anasema karibu kila kituo cha afya cha wilaya hiyo kinalo gari la wagonjwa.

Hata hivyo, anaahidi kununua magari mengine mawili kwa ajili ya kituo cha afya cha Idodi na Shule ya Sekondari ya Malinzanga.

“Idodi mlikuwa na gari lakini limepata ajali na limechakaa kabisa, nafikiria kuleta gari aina ya cruser hii itafaa kwa mazingira ya huku,” anasema.

Hata hivyo, anatumia nafasi hiyo kuwakumbusha wananchi wake kuhusu kuchangia mfuko wa afya wa jamii.

Anasema hizo ndizo fedha zitakazosaidia kuwa na uhakika wa dawa.

Diwani wa Kata ya Mlowa, Charles Nyagawa anasema kinachosaidia kasi ya maendeleo kwenye jimbo hilo ni ushirikiano ulipo baina ya mbunge huyo na wananchi wake.

Kero ya maji

Baadhi ya wananchi walimuomba mbunge huyo kushughulikia kero ya maji inayowakabili kwenye vijiji vyao.

Mkazi wa Kijiji cha Tungamalenga, Anjelina Kasimba, mkazi wa Kijiji cha Tungamalenga anasema uhaba wa maji umekuwa ukichangia kuzorota kwa shughuli za maendeleo.

Kutokana na ombi hilo, Lukuvi anasema maeneo mengi ya jimbo hilo tayari yana maji na kuahidi kushughulikia kero ambako bado.

Kituo cha afya Idodi

Kwa mara ya kwanza, jimbo hilo limefanikiwa kuwa na kituo cha afya ambacho ukarabati wake na ununuzi wa vifaa tiba umegharimu Sh1.3 bilioni.

Lukuvi anasema kati ya fedha hizo Sh700 milioni zilitolewa na Rais John Magufuli wakati vifaa vya Sh600 milioni ni jitihada zake.

“Hivi vifaa nilitumiwa na rafiki zangu kutoka huko Marekani, kituo hiki kitaweza kufanya upasuaji wowote ule na tunao wataalamu wa kutisha hapa,” anasema.

Anasema ahadi yake ilikuwa kuwa na kituo cha afya kikubwa kitakachoweza kutoa matibabu bora kwa wananchi ikiwamo upasuaji, tayari ameshatimiza.

“Nimshukuru Rais Magufuli kwa kukiona kituo hiki na kutoa fedha Sh400 milioni za ujenzi na 300 milioni za vifaa zaidi ya aina 80. Na hivi vifaa vya Sh600 milioni vinavyoletwa vimetoka kwa rafiki zangu wa huko Marekani,” amesema

Mtaalamu wa Maabara wa Kituo hicho cha Afya, Seka Dege alisema wagonjwa wengi wanaopatikana kwenye eneo hilo wanaugua malaria na UTI.



Chanzo: mwananchi.co.tz