Dar es Salaam. Licha ya chama cha ACT-Wazalendo nchini, Tanzania kujitoa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, jina la mgombea wa chama hicho limechomoza kwenye orodha ya wagombea wanne wa nafasi ya wajumbe wa mtaa wa Mikoroshini wilayani Kinondoni.
Kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi wa Kinondoni, Kiduma Mageni mgombea huyo Yasin Matereka anachuana na wagombea wengine watatu wa CCM wanaowania nafasi tatu za kuwa wajumbe wa mtaa huo uliopo kata ya Ndugumbi.
Uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji unafanyika leo Jumapili, Novemba 24, 2019 katika mikoa mbalimbali isipokuwa ya Tanga, Katavi na Rukwa ambayo wagombea wa CCM wamepitwa bila kupingwa.
Katika uchaguzi huo, vyama vya CUF, ACT-Wazalendo, Chadema, Chaumma, UPDP na NCCR-Mageuzi vimejitoa kwa kile walichodai kutoridhishwa na mchakato huo. Hata hivyo vyama vya ADC, AAFP, DP na Ada Tadea vinashiki uchaguzi huo.
Akizungumza na Mwananchi, Mageni amesema wilaya ya Kinondoni uchaguzi huo unafanyika katika mtaa wa huo kwa wagombea wa CCM na ACT-Wazalendo kuwania nafasi ya wajumbe.
Kuhusu jina la mgombea wa ACT-Wazalendo kuwepo katika karatasi za kura Mageni amesema “ Ninachojua alichukua fomu na kurejesha na alidhaminiwa na chama chake ngazi ya tawi. Baada ya kuzipitia fomu zake alikidhi vigezo na kuteuliwa kugombea mchakato huu.
“Suala la kujitoa au kutojitoa ni la mgombea husika. Ukiona hadi jina la mgombea lipo katika hatua hii, nina imani alikusudia kushiriki mchakato huu,”amesema Mageni.
Hata hivyo, Mageni amesema katika mchakato huo mawakala wa mgombea huyo hawapo lakini haibatilishi uchaguzi huo kwa mujibu wa kanuni, akibainisha kuwa endapo akishinda atatangazwa kama kawaida.
“Tumeapa katika mchakato huu na kura zake tutazihesabu kwa mujibu wa kanuni. Hata kama hatokuwepo kwenye kuhesabu kura akishinda tutamtangaza,” amesema Mageni.
Mageni amesema wanatarajia kuwatangaza washindi wa mchakato huo leo jioni baada ya mchakato wa kuhesabu kura kukamilika huku akiwashukuru wakazi wa mtaa huo kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi huo.
Mwananchi imeshuhudia polisi wakiimarisha ulinzi wakati wote wa mchakato kuanzia wananchi wanapohakiki majina, kupiga kura.