Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jesca Kishoa: Niliteuliwa kugombea nafasi ya ubunge nikiwa mjamzito

46500 Pic+kishoa

Wed, 13 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ijumaa ya Machi 8 mwaka huu, Tanzania iliungana na nchi nyingine duniani katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake. Hii ni njia ya kutuma ujumbe kwa jamii katika vita dhidi ya ukandamizaji wa mwanamke kuanzia nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Hata hivyo, hali bado hairidhishi na mabinti wengi nchini wanatamani kufungua mnyororo huo ili kutimiza ndoto za uongozi ndani na katika duru za kimataifa lakini wanakumbana na vikwazo.

Ili kufikia mafanikio hayo, Jesca Kishoa, mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) anasema katika mahojiano kuwa ziko hatua zinazohitaji nidhamu ya hali ya juu.

Mwandishi: Jesca, Kwa upande wako ulikutana na changamoto gani kabla ya kuwa mbunge?

Jesca: Nakumbuka wakati wa uchaguzi mwaka 2015 niliteuliwa kuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema. Changamoto kubwa niliyokuwa nayo ni hali yangu ya kiafya kwa kuwa nilikuwa na ujauzito wa miezi tisa.

Hali hii ilipelekea mume wangu na ndugu zangu kutoniunga mkono katika ushiriki wangu kugombea nafasi hiyo wakihofu ninaweza kupata madhara kutokana na mikikimikiki ya kampeni.

Lakini jambo moja ambalo nilikataa ni kuruhusu changamoto yoyote kunirudisha nyuma. Namshukuru Mungu nilikazana mpaka dakika ya mwisho, sikufanikiwa kwa njia ya jimbo lakini kutokana na ushiriki huo chama changu kilinipatia nafasi ya kuwa mbunge wa viti maalumu.

Mwandishi: Kwa uzoefu huo, unadhani hiyo ninaweza kuwa kikwazo kwa mabinti wengi kutofikia ndoto zao?

Jesca: Changamoto siyo hiyo tu, ziko zaidi ya hizo. Binafsi, ninayatazama mambo yafutayo kama changamoto kwa wanasiasa mabinti.

Kwanza, kuna changamoto ya mitazamo hasi ya jamii dhidi ya wanawake wanasiasa. Katika jamii yetu inayotawaliwa kwa mfumo dume, msisitizo mkubwa umewekwa kuwa majukumu ya mwanamke ni ya nyumbani, yaani kulea watoto, kutunza nyumba na kuwa mzalishaji wa mazao. Majukumu yanayohusu maamuzi yoyote hufanywa na wanaume bila hata ridhaa ya wanawake.

Kwa hali hiyo, wanasiasa mabinti hubezwa sana katika chaguzi zetu. Kwenye kampeni lugha zisizo na staha hutumiwa kuwadhofisha wanawake.

Kuna changamoto nyingine ya kiuchumi. Katika ulimwengu wa siasa kuna gharama kubwa, kwa mfano kuandaa machapisho, nembo, mikutano makongamano na shughuli mbalimbali za siasa na wanawake wanashindwa kuzimudu.

Nimeshiriki katika shughuli na matukio tofauti ya kisiasa, nimekumbana sana na hali hii. wanawake wenye uwezo na vipaji vya uongozi wanaweza kukwama ndoto zao kupitia vikwazo hivi.

Tatu ni ushirikiano mdogo na wadau wa siasa kwa wanawake wasiokuwa na mtandao ndani ya asasi za kisiasa, uzoefu mdogo, pamoja na uwezo mdogo kifedha unaweza kuwakwamisha.

Mwandishi: Unautazamaje ushiriki wa wananchi hapa nchini ukilinganisha na nchi nyingine?

Jesca: Wanawake wanachukua asilimia 52 ya idadi ya watu duniani lakini uwiano ni asilimia 80 kwa wanaume na asilimia 20 kwa wanawake katika vyombo vya maamuzi ulimwenguni.

Riporti ya Umoja wa Mataifa kitengo cha wanawake 2018 inaonyesha kuwa wanawake wana asilimia 24 tu katika ngazi ya ubunge duniani kote. Hadi kufikia Januari 2019 katika nafasi ya wakuu wa nchi na Serikali duniani wanawake ni 23 tu.

Hali ya uwakilishi duni wa wanawake katika vyombo vya maamuzi na siasa katika bara la Afrika kwa sasa linaridhisha kiasi, kwani katika baadhi ya mataifa wanawake wamekaribia au kufikia mpango wa 50/50.

Kwa mfano, wanawake katika vyombo vya maamuzi nchini Rwanda wamefikia asilimia 55.6 ukilinganisha na wanaume. Afrika ya Kusini ni asilimia 41, Senegal na Tanzania asilimia 37, hao ni kwa uchache . Kasi ya Ethiopia ya hivi karibuni inapongezwa na wadau wa masuala ya kijinsia duniani.

Lakini pamoja na mgawanyo huo, jambo la muhimu ni wanawake wenyewe kujitokeza na kuwa jasiri kupambana na changamoto zilizo mbele yao

Chanzo: mwananchi.co.tz