Waziri mpya wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa leo Sept 04,2023 amefika Ofisi ya Wizara hiyo Jijini Dodoma na kupokelewa na Watumishi wa Wizara ambapo baada ya mapokezi amevitaja vipaumbele vyake 12, ambavyo ni pamoja na kuhahakisha Nchi inapimwa na kupangwa na kumaliza migogoro ya ardhi ndani ya siku 100 huku akisema yeye harubuniwi kwa rushwa na alishawahi kukataa rushwa ya Tsh. bilioni 1 Ilala.
Waziri Silaa amewashukuru waliomtumia pongezi na kusema mwisho wa pongezi ni jana kwa sasa ni muda wa kazi na amewataka Watumishi Wizarani wasisubiri kupangwa maana Mtu akipangwa atapanguliwa.
Vipaumbele vitano kati ya 12 ambavyo amenukuliwa akivitaja ni “Ukipigiwa, uwe na majibu, sina Mtu nyie wote ni Watu Timu ya Wizara, ndani ya siku 100 kila Mtu amalize mgogoro kwa ngazi yake, Mh. Rais ametuelekeza maslahi ya Wananchi kwanza, mtende haki kwa wote Mnyonge ana haki, mwenye uwezo ana haki, Mtanzania mwenye asili yoyote ana haki”
“Kuhusu rushwa sichukui rushwa, usiniletee hela, nitakuitia TAKUKURU, sina Wakala, situmi sms, siuzi appointment, Dar niingilie upande wa Wananchi, hakuna anayenimudu, Ilala nilikataa rushwa ya bilioni 1, tukatoa mapato bilioni 9- bilioni 32 -bilioni 54, tukakusanya data , leo miaka 9 ndio Satura anakusanya data, ingawa gharama yake ni kubwa Mkurugenzi wangu alisimamishwa kazi, Afisa ushirika alipigwa risasi akaibiwa laptop tu”
“Maeneo ya wazi , maeneo ya huduma, maeneo ya Taasisi kama mliyabadilisha matumizi mtayarudishia matumizi yake, kama Baraza la Madiwani lilihusika tutaishauri Mamlaka kama mlingoja Madiwani wako kwenye uchaguzi mkabutua mtarejesha, nilipokuwa Meya niliacha maeneo ya wazi 264 Kinyamwezi, Viwege, Buyuni, Zavala, sikuchukua hata eneo moja, siku nikifanya ziara Ilala niyakute yote”
“Kuhusu nyumba za NHC miradi ilisimama, ianze haraka na tuone mpango ujenzi wa nyumba, za gharama ya chini, kati, juu na juu kabisa, sheria kama zina mapungufu tufate taratibu zibadilishwe”
“Nchi hii lazma ipimwe yote na ipangwe yote na kule wanakouziana viwanja kwa miguu Wizara itoe maelekezo size ya kiwanja , size ya barabara na nani atatoa eneo la huduma za jamii”