MBUNGE wa Ukonga, Jerry Silaa (CCM), amesimamishwa kushiriki mikutano miwili ya Bunge huku Spika Job Ndugai akimtaka aombe radhi hadharani.
Uamuzi huo uliridhiwa na Bunge jana baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwasilisha taarifa yake kuhusu shauri dhidi ya mbunge huyo ikimtia hatiani kwa kauli yake kwamba 'mishahara ya wabunge haikatwi kodi'.
Bunge pia limeridhia mbunge huyo avuliwe uwakilishi wake kwenye Bunge la Afrika (PAP) kwa madai anaweza kusema uongo huko.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Emmanuel Mwakasaka, alitumia dakika 28 kuanzia saa 5:42 asubuhi kuwasilisha bungeni jijini hapa taarifa ya kamati kuhusu shauri dhidi ya mbunge huyo aliyewahi kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.
Mwakasaka aliliambia Bunge walipata wasaa wa kufuatilia mwenendo wa shahidi huyo mbele ya kamati na kubaini ni mkaidi, jeuri na hakutaka kujutia kauli zake licha ya kuitwa mbele ya kamati hiyo.
Alisema Silaa, akizungumza na wananchi wa Ukonga, alitoa kauli kwamba wabunge hawalipi kodi katika mishahara yao, jambo lililopingwa kwa kuwa wabunge wanakatwa kodi katika mishahara yao.
"Mheshimiwa Silaa alikiri kutoa kauli hiyo alipokuwa anahutubia wananchi wa Ukonga. Alikiri mbele ya kamati kuwa kwenye mshahara wake wa ubunge kuna kiasi kinakatwa kodi na kingine hakikatwi kodi.
"Mheshimiwa Silaa aliiambia kamati kwamba posho za wabunge hazikatwi kodi. Kinachokatwa ni ‘basic salary’," alisema.
Mwakasaka alibainisha kuwa kamati ilimhoji Mhasibu Mkuu katika Sekretarieti ya Bunge ambaye alikiri mishahara ya wabunge inakatwa kodi lakini posho za watunga sheria hao hazikatwi kodi na kwamba utaratibu huo wa kutokata kodi kwenye posho unatumika maeneo mengine serikalini.
Alisema shahidi huyo aliikabidhi kamati hati ya mshahara wa Silaa na kutumika kama moja ya vielelezo vya shauri hilo.
"Tumeona Mheshimiwa Silaa alikuwa na nia ovu ya kulichonganisha Bunge na wananchi. Kitendo hicho ni utovu wa nidhamu uliokithiri.
"Kamati ilipata wasaa wa kufuatilia mwenendo wa Mheshimiwa Silaa mbele ya kamati na kubaini hakuwa tayari kujibu maswali kikamilifu. Kwa kifupi, shahidi hakutoa ushirikiano kwa kamati.
TUHUMA NZITO
Mwakasaka alisema Silaa aliandika barua kwa Katibu wa Bunge akiituhumu kamati kutomtenda haki na shauri lake liliendeshwa kwa upendeleo.
"Barua yake ilikuwa na maneno makali dhidi ya kamati. Kwenye barua yake alisema hatafika mbele ya kamati kwa sababu hakupatiwa taarifa ya wito na akahoji kwa nini kamati umulize kama anafaa kuwa mbunge wa PAP na uvumilivu wake umefika mwisho, hivyo atashtaki kwenye mahakama ya umma.
"Tulijiridhisha huyu mbunge kwa mwenendo wake huu, atasema uongo kwenye Bunge la Afrika (PAP). Tunapendekeza Bunge liazimie asimamishwe kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge na aondolewe kuiwakilisha nchi katika Bunge la PAP," Mwakasaka aliwasilisha.
AOMBE RADHI
Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema kitendo cha mbunge huyo kulichafua Bunge mbele ya jamii kwamba wabunge hawalipi kodi, hakikubaliki na anapaswa kuomba radhi hadharani.
"Lazima aombe radhi kwenye 'public' kuhusu hili suala la kudhalilisha wabunge. Hatujaomba ubunge ili kuvunjiwa heshima," aliagiza.
Spika Ndugai alisema kuwa kwa nchi za Magharibi, mtu akitajwa kuwa mkwepaji wa kodi za serikali, anaweza kuchukua uamuzi mgumu, ukiwamo wa kujinyonga.
"Adhabu hizo ni ndogo sana, basi tu kwa sababu hawa ni ndugu zetu. Gwajima hayupo. Silaa yupo humu ndani. Sasa kwa heshima ninakutaka uondoke humu bungeni, tukutane mkutano wa Januari. Na askari hakikisheni mnamsindikiza hadi nje kabisa ya viwanja vya Bunge," Spika aliagiza.