Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jenerali Ulimwengu ataka usawa uwanja kisiasa

Ulimwengu Jen Jenerali akiwa na kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto

Wed, 18 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanahabari mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu amependekeza kuwepo kwa uwanja sawa wa siasa ili wenye mawazo yanayotofautiana wawe na uhuru wa kuyatoa, huku akiwataka viongozi kujenga utamaduni wa kuvumiliana badala ya kutumia nguvu kuwadhibiti.

Akizungumza Dar es Salaam baada ya kutoa maoni yake mbele ya wajumbe wa Kikosi Kazi kinachoratibu maoni kuhusu demokrasia ya vyama vya siasa nchini, Ulimwengu alisema hali ya kisiasa kwa miaka sita iliyopita haikuwa nzuri .

Alisema watu hawakuwa na uwezo wa kujieleza kwa uwazi kwa kubainisha mambo ambayo waliyahisi kutokwenda sawa.

“Hali hiyo lazima igeuzwe, na watu wawe na uhuru wa kuambizana ukweli kwa vile wanavyohisi bila kuogopana wala kutishwa ni vizuri tujenge uwanja ulio sawa wa kisiasa. Tujenge utamaduni uleule ambao miaka michache iliyopita ulikuwepo, licha ya kwamba miaka ya katikati hapa ulianza kupotea. ‘‘

‘‘Kuwe na uhuru wa kupambanisha hoja na si kupambana kwa mabavu. Kutofautiana ni hali ya kawaida si ugomvi na ni vizuri kuelewa kwamba binadamu tumeumbwa tofauti,” alisema Ulimwengu

Alisema viongozi wanapaswa kujenga utamaduni wa kupambana kwa hoja tena kwa kuulizana maswali hasa pale wanapoonekana wamekosea na kujenga uvumilivu katika mawazo hasa pale wanapotofautiana.

Advertisement Mkongwe huyo wa habari ambaye pia ni mwanasheria, alibainisha kuwa hali ya asasi za kiraia haiko sawa, huku akizitaka kuacha uoga na kupigania haki zao, kwani hakuna anayeweza kujitokeza kuwasaidia.

“Asasi za kiraia bado haziko huru ni vizuri na zenyewe zikajitokeza kupigania haki zao badala ya kuendelea kukaa kimya,”alisema.

Kuhusu hoja ya Katiba, Ulimwengu, alisema ni vizuri ikaanza kwa sababu ni msingi thabiti wa kupata tume huru ya uchaguzi, ambayo itakuwa inasimamia misingi inayotokana na Katiba.

Mchakato Katiba uharakishwe

Naye mjumbe kutoka Chama Cha ACT- Wazalendo, Ismail Jussa aliyetoa maoni yake katika kikosi hicho, alishauri kuharakishwa kwa mchakato wa Katiba mpya.

“Katiba mpya si suala la mjadala tena. Katiba Mpya inahitajika sasa kwa sababu historia ya Katiba zote za Tanganyikana Zanzibar, kabla ya Muungano na Katiba ya Jamhuri ya Muungano, hazikutokana na ushirikishaji wa wananchi.

“Tunahitaji Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya wananchi kama yalivyokusanywa na Tume ya Jaji Warioba,” alisema.

Alisema kabla ya kwenda kwenye upitishaji wa Katiba Mpya kupitia Bunge la Katiba, itafutwe njia ya kuondokana na mkwamo akitaja haja ya kuwa na mkutano wa majadiliano ya kitaifa.

“Iundwe tume ya wataalamu wa ndani na nje ya nchi watakaochukua rasimu ya Katiba yenye mapendekezo ya wananchi (Rasimu ya Warioba) na maafikiano yatakayopatikana kwenye mkutano wa majadiliano ya kitaifa na kisha kutengeneza rasimu itakayofikishwa kwenye Bunge la Katiba,’’ alisema.

Kuhusu tume huru ya uchaguzi alisema inapaswa iwe na makamishna ambao watapatikana kwa sifa na vigezo maalumu kupitia matangazo ili wenye sifa na vigezo hivyo waombe.

“Iwepo kamati huru ya uteuzi itakayowahoji kupitia utaratibu wa wazi unaoonekana na wananchi wote, na watakaochaguliwa wawe ni wale waliokubalika na wote kwamba wametimiza sifa na vigezo kisha kufikishwa kwenye mamlaka ya uteuzi kwa ajili ya kutangazwa tu.”, alisema

Alishauri tume kuajiri watendaji wake wote kuanzia kwenye majimbo ya uchaguzi hadi kwenye vituo vya kupigia na kuhesabu kura na kwamba haki za vyama na wagombea kuweka mawakala na haki za mawakala hao kwenye hatua zote za uchaguzi, zitamkwe waziwazi kwenye sheria na kulindwa.

“Kuwepo na taasisi ya kudumu itakayoundwa kwa mujibu wa sheria kusimamia maridhiano katika nchi na kuwa jukwaa la kudumu la mazungumzo na majadiliano. Unaweza kuangaliwa mfumo kama wa iliyokuwa Tume ya Rais ya Pamoja ya Usimamizi wa Mwafaka (Joint Presidential Supervisory Commission) ya Zanzibar,” alisema Jussa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live