Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jaji Werema aeleza mawaziri walivyomtenga, Kikwete akamgomea kujiuzulu mara tatu

Werema Jk.jpeg Jaji Werema akiapishwa na Rais Kikwete (Picha na maktaba)

Sun, 24 Jul 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amesimulia jinsi mawaziri walivyojiweka kando naye, wakati wa sakata la Escrow mwaka 2014, jambo ambalo lilimsukuma kujiuzulu katika nafasi yake kulinda heshima.

Jaji Werema alieleza hayo juzi jijini Dar es Salaam, wakati wa mahojiano maalumu na kuzungumzia masuala mbalimbali aliyopitia wakati wa utumishi wake na hali ya kisiasa inayoendelea sasa hapa nchini.

Mwanasheria huyo mkongwe ambaye sasa ni mbia na mwasisi mwenza wa kampuni ya uwakili ya FMD Legal Consultants and Advocates, aliteuliwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Oktoba 19, 2009 na alijiuzulu Desemba 16, 2014.

Katika mahojiano hayo, Jaji Werema alizungumzia mambo mbalimbali, ikiwamo kashfa ya Escrow, maridhiano ya kitaifa, upatikanaji wa majaji, kurejea kwa machifu nchini, zuio la mikutano ya hadhara na elimu ya uraia.

Jaji Werema alisema jambo lililomsikitisha na kumsononesha katika utumishi wake lilikuwa ni kashfa ya Escrow, hasa pale alipoambiwa yeye ni mwizi wakati hajawahi kuambiwa hivyo hata siku moja katika maisha yake.

Kashfa ya ufisadi wa Escrow ilihusisha uchotwaji wa fedha Sh306 bilioni katika akaunti ya Tegeta Escrow, huku vigogo kadhaa serikalini wakinufaika na mgawo wa fedha hizo na mjadala uliokuwepo bungeni wakati huo ulikuwa ni kama fedha hizo zilikuwa za umma kwa maana ya kumilikiwa na Shirika la Umeme Tanesco (Tanesco) au kampuni ya kufua umeme ya IPTL.

Viongozi kadhaa wa Serikali waliotuhumiwa kupata mgawo wa fedha hizo, wakiwamo mawaziri, walilazimika kujiuzulu nafasi zao. Jaji Werema akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, naye aliamua kujiuzulu licha ya kwamba hakupata mgawo huo.

Mawaziri waliong’oka kutokana na sakata hilo ni, Profesa Anna Tibaijuka aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Profesa Sospeter Muhongo wa Nishati.

Pia kulikuwa na wabunge waliovuliwa nyadhifa zao za uenyekiti wa Kamati za Bunge ambao ni pamoja na Andrew Chenge (Bajeti), William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala), Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini).

Jaji Werema anasema awali alikataa kujiuzulu kwa sababu hakuona sababu ya kufanya hivyo kwani hakuhusika katika tuhuma alizohusishwa nazo. Hata hivyo, alisikitishwa na kitendo cha mawaziri kujiweka pembeni bungeni badala ya kuwajibika pamoja kama Serikali.

“Kilichonisikitisha zaidi ni kukosekana kwa collective responsibility (uwajibikaji wa pamoja) wa Serikali ndani ya Bunge, hicho kitu sikutegemea kwamba kitatokea, bahati mbaya sasa Rais (Jakaya Kikwete) hakuwepo nchini wakati huo lakini nilikuwa nikifanya mawasiliano naye kila wakati,” anasema.

Alisisitiza kutokana na alichokiita kama usaliti huo wa mawaziri, alisubiri hadi Rais aliporejea nchini na kumuomba ajiuzulu nafasi yake ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, jambo ambalo Kikwete hakulikubali kwa mara moja.

“Baadhi ya mawaziri wakaonekana kwamba wako upande mwingine; na hilo nikaona kama ni usaliti. Na kwa sababu sasa mawaziri hawa ambao mimi nawashauri wako hivyo, nikamwambia Rais aliporudi kwamba mimi nataka kuachia ngazi,” alisema Jaji Werema.

Kikwete amkatalia kujiuzulu

Baada ya kuona mawaziri wamegawanyika, Jaji Werema anasema alikwenda Ikulu kwa Rais Kikwete mara tatu kumwomba ajiuzulu nafasi hiyo, hata hivyo anasema mara ya kwanza na ya pili alikataa kujiuzulu kwake na mara ya tatu alimkubalia.

“Rais alikataa mwanzoni, nikamwambia tena akakataa, nikaenda safari ya tatu, safari hii nikakaa naye nafikiri kwa saa nne tunazungumza, mimi nikasema nimeshaamua kutoka, kwa hiyo nikatoka,” anasema.

Anasema alikuwa akipata shinikizo la kujiuzulu kutoka kwa wabunge, jambo ambalo anasema lilichukua muda kufanya hivyo. Anasema anaamini pengine angejiuzulu wakati ule mambo yale yasingeenda mbali zaidi.

Jaji Werema anasema baada ya kujiuzulu, Rais Kikwete alitaka kumpa kazi ya kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa, hata hivyo anasema alikataa kwa sababu alitiliwa shaka na wabunge kwamba anahusika kwenye wizi wa fedha za Escrow.

“(Kikwete) akaniambia anipe kazi ya ujaji wa mahakama ya rufaa, nikakataa nikasema tayari watu wameshaanza kuhisi kwamba inawezekana mikono yangu ni michafu, sasa hii ni Mahakama ya juu ambayo haitakiwi kuwa na mashaka yoyote, kama mke wa Kaizari,” anasema mwanasheria huyo.

Baada ya kujiuzulu na nafasi yake kuchukuliwa na George Masaju, kazi yake ya kwanza kwenda kufanya ilikuwa kwenda kulima, huku akisema alipata mazao mengi lakini mwaka uliofuata sera ya Serikali ilibadilika, akashindwa kuendelea kulima.

Anasema baadaye aliteuliwa na Rais Kikwete kwenda kuwa msuluhishi wa mgogoro wa Lesotho akishirikiana na Rais wa sasa wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambaye wakati huo alikuwa Makamu wa Rais.

Hakumwita Kafulila “tumbili”

Neno “tumbili” liliibuka kwenye mjadala bungeni ambapo Jaji Werema alidaiwa kumwita aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini wakati huo kupitia NCCR-Mageuzi, David Kafulila wakati akijibu mchango uliotolewa na mbunge huyo.

Hata hivyo, Jaji Werema anasema hakumwita Kafulila tumbili, bali anasema alitumia msemo wa Kiganda usemao “enkima etagwisanga emisango ye kibira” kwa maana kwamba “tumbili haamui mambo ya msituni.”

Anasema alitumia msemo huo kulingana na muktadha uliokuwepo wakati wa mjadala huo akimjibu Kafulila ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kwamba hakuwa na taarifa sahihi kuhusu fedha za Escrow kama zilikuwa za umma au za kampuni ya IPTL.

“Mimi ni Mkristo, siwezi kumwita mtu tumbili kwa sababu ni kiumbe wa Mungu na tumeumbwa kwa mfano wa Mungu. Kwa hiyo, mimi hainipi shida, nilizungumza kisheria zaidi, kwamba ukitaka kuamua kesi ya mtu lazima uwe na facts (taarifa za hakika) zote.

“Kwa hiyo hizo ‘facts’ ambazo nilikuwa nazo, yeye Kafulila hakuwa nazo, ndiyo maana ya ‘tumbili haamui mambo ya msituni’,” alisema Jaji Werema, aliyezaliwa Oktoba 10, 1955.

Anasema kwenye suala la Escrow alikuwa akipokea taarifa kutoka wizarani na katika ripoti za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Anasema CAG wa wakati huo, Ludovick Utouh alisema fedha za Escrow siyo mali ya Tanesco, ni za IPTL lakini baadaye alikuja kusema zilikuwa fedha za umma.

Arudisha heshima ya ofisi

Jaji Werema alisema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilikuwa imepoteza heshima bungeni, hasa baada ya kutoka kwa watangulizi wake.

Anasema alikwenda bungeni akifahamu mtazamo wa wabunge kuhusu ofisi hiyo, hivyo alijitahidi kuibadilisha ili iheshimike. Anasema alifanikiwa katika jambo hilo kwa sababu ofisi hiyo hatimaye iliheshimika.

“Wabunge walikuwa wanaamini Mwanyika (aliyekuwa mwanasheria kabla yake) hakufanya kazi vizuri, mimi najua alifanya kazi vizuri ingawa hakuwa mtu wa makeke. Kwa hiyo mimi nilipoingia nilijua huo mtazamo ya wabunge kuhusu ofisi na nafikiri nimeijenga,” anasema.

Anasema anakumbuka aina ya demokrasia iliyokuwepo bungeni wakati ule na baadhi ya wabunge walikuwa wanatumia fursa hiyo kufanya kampeni, kwa sababu walikuwa wanaonekana moja kwa moja kupitia vyombo vya habari.

“Wabunge walikuwa wanatumia fursa ile kujitangaza kwa jinsi walivyokuwa wanaongea kwamba mtu akiongea tough (kwa nguvu) ataonekana yuko tough. Ilikuwa ni aina ya demokrasia ambayo tunaitaka kwa kweli,” anasema.

Ahofia kurudi kwa uchifu

Katika mahojiano yake, Jaji Frederick Werema ameonya utawala wa viongozi wa jadi (machifu) ukiendelea kupewa nafasi unaweza kusababisha utawala wa serikali za majimbo.

Jambo hilo limewahi kutahadharishwa pia na viongozi wengine wastaafu, akiwamo Kikwete na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba ambao walisisitiza kwamba uchifu ukipewa nafasi utaligawa Taifa.

Anasema huko nyuma kulikuwa na sheria iliyokuwa inawatambua, lakini baadaye iliondolewa na lengo lilikuwa kuondoa mgawanyiko.

“Kuna kitu kimoja ambacho sijakielewa na nilishawahi kuzungumza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na bado hajarudi kwangu, kuhusu hili suala la viongozi wa jadi (machifu), hilo silielewi kwa kweli kwa sababu machifu hawa hata ukitaka kuhalalisha utakuwa unavunja sheria,” anasema.

Anasema anavyotambua yeye ni kwamba utawala wa viongozi hao ulishaondolewa na kama wanatumiwa ikiwa sehemu ya kuwashirikisha, itakuwa sawa kwa sababu Watanzania wote ni jamii moja.

Maridhiano ya kitaifa

Jaji Werema anasema akiwa mtumishi wa umma na baada ya kustaafu, anaamini mfumo wa maridhiano ni mzuri, hasa kwa sasa Serikali inapoanza mchakato wa kuratibu kuandikwa kwa Katiba mpya.

“Zamani, Katiba tuliyonayo ilipopatikana Uingereza kabla ya kufanyiwa marekebisho baada ya uhuru hakukuwa na mchakato wa ushirikishwaji wa wananchi kwa ukubwa na upana wa maoni yanayostahili, lakini kulikuwa na timu iliyokuwa inazungumza na Serikali na wakati mwingine mabadiliko yalikuwa yanafanyika ndani kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu,” anasema.

Anasema kwa sasa Katiba inajumuisha nchi nzima, kwa hiyo ni vizuri watu wengi wakashirikishwa na watu walianza kushirikishwa tangu kwenye Bunge la Katiba na kwamba watu walikuwa wanatoka sehemu zote za nchi.

“Kwa vyovyote vile hakutakuwa na jambo litakalokubaliwa na watu wote, kwa hiyo kinachotakiwa kuna vitu vingine ambavyo lazima tukubaliane kwa kufanya maridhiano, kwa mfano kuna mambo ya kitaifa ambayo tunakubaliana na kuna mengine hatuna mwafaka,” anasema.

Alisema kwenye suala la Muungano kama watu wengi wanavyozungumza ni jambo ambalo linahitaji maridhiano, huku akieleza Katiba ya 1977 inaeleza aina ya muungano uliopo na kwamba Tanzania ni nchi moja.

“Katiba inasema Tanzania ni nchi moja ya Jamhuri ya Muungano na Katiba hiyo imeipa Zanzibar mamlaka kwenye mambo fulani ya Muungano na yasiyokuwa ya Muungano. Ukija kwenye Katiba Pendekezwa, inasema nchi moja, lakini msingi wake ni hati ya makubaliano.

“Haya ndiyo mambo ambayo tunapaswa kuridhiana, tuwe na muungano wa aina gani ambao utakuwa wa haki kwa pande zote,” anasema Jaji Werema.

Uteuzi wa majaji

Jaji Werema anasema kuna haja ya kufanya utafiti kuangalia namna majaji wanavyopatikana kwa kurejea malalamiko yanayotolewa na wadau mbalimbali, wakiwamo wanasiasa na wanaharakati.

“Hakuna kiatu kinachomtosha kila mtu na hakuna jambo linalofaa kwa kila nyumba isipokuwa kila nyumba ina utaratibu wake, kinachotakiwa ni haki ya watu katika nyumba ile.

“Kuna baadhi ya watu wanasema uteuzi wa majaji umekuwa si mzuri, nafikiri kuna haja ya kufanya utafiti zaidi kuangalia uteuzi wao kwa sababu ilivyo sasa kuna kamisheni inayoenda kuwachuja, mahakimu, mawakili wa Serikali na binafsi ambao wanafaa kuwa majaji,” anasema.

Anasema utaratibu huo ulikuwa unatumika hata yeye alipokuwa jaji na wakati huo alikuwa mjumbe wa Kamati hiyo huku akieleza hajui kama utakuwa umeharibiwa, lakini ni vizuri kuliangalia kwa sababu kila lisemwalo lipo na linapaswa kuchunguzwa.

“Lakini hii ya kusema watu waombe ujaji, vyama vitaingia huko kuwapigia kampeni ili watu wao waingie na mimi sipendi hivyo, bali jaji lazima awe anajitegemea kama tume huru inataka uhuru, basi ndivyo kwa majaji wanatakiwa wawe na uhuru huo,” anasema.

Elimu ya uraia

Jaji Werema anabainisha kwamba elimu ya uraia haitolewi vizuri, ithibati yake haiko vizuri na pia mitalaa yake haijulikani vizuri. Alisisitiza kwamba elimu ya siasa siyo kwa wanafunzi tu bali ni kwa kila Mtanzania kwa nafasi yake.

“Elimu ya siasa siyo wanafunzi tu, hata nyinyi waandishi wa habari na Watanzania wote, wanatakiwa kujua elimu hii, na siyo elimu ya siasa tu, hata elimu yako mwenyewe, maadili yako mwenyewe,” anasema Jaji Werema.

Anasisitiza kwamba suala la haki jamii ni muhimu, ndiyo maana Katiba ya sasa, rasimu ya Katiba ya Warioba na katiba Inayopendekezwa, zote zinazungumzia haki jamii kama moja ya tunu za Taifa.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz