Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jaji Mkeha kusikiliza kesi ya Mdee, wenzake kuanzia kesho

D373cdfdcb853742b9be463ad107b95f Jaji Mkeha kusikiliza kesi ya Mdee, wenzake kuanzia kesho

Thu, 28 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu, Masjala Kuu imepanga kusikiliza kesi ya Mbunge wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee na wenzake 18 wanaopinga uamuzi wa kuvuliwa uanachama wa chama hicho.

Kesi hiyo itasikilizwa Julai 29, mbele ya Jaji Cyprian Mkeha.

Julai 21, mwaka huu, Mdee na wenzake walifungua kesi hiyo mahakamani hapo wakipinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema wa kuwavua uanachama wa Chadema uliotolewa Mei 11, mwaka huu.

Katika shauri hilo, wabunge hao pamoja na mambo mengine, wanaiomba mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi huo wa Baraza Kuu la Chadema kuwafukuza kisha itoe amri tatu.

Wabunge hao wanaomba mahakama itengue mchakato na uamuzi wa kuwavua uanachama; iwalazimishe Chadema kuwapa haki ya kuwasikiliza na amri ya zuio dhidi ya Spika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutokuchukua hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapoamuliwa na mahakama.

Uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema ulitokana na rufaa walizozikata Mdee na wenzake baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa awali wa Kamati Kuu ya Chadema kuwavua uanachama, Novemba 27, 2020 kwa kile kilichodaiwa kuwatia hatiani kwa kosa la kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa Viti Maalumu bila ridhaa ya chama.

Walidai kuwa sababu iliyotolewa na Baraza Kuu kumfukuza uanachama, ilitokana na makosa yasiyo na maana na yasiyoweza kuthibitika, kwamba alikula njama kujiteua mwenyewe na kuapa kuwa Mbunge wa Viti Maalumu.

Pia walidai mchakato na uamuzi wa kuwafukuza uanachama haukuzingatia matakwa ya kisheria na misingi ya haki kwa kuwa hawakupewa haki ya kusikilizwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live