Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JPM ndiyo turufu ya wagombea wa CCM

10040 Pic+msukuma TanzaniaWeb

Sat, 4 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Babati. Mbunge wa Jimbo la Geita Vijiji, Joseph Kasheku maarufu Musukuma amesema utendaji wa Rais John Magufuli ndiyo turufu ya wagombea wa CCM kushinda uchaguzi mdogo.

Musukuma aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa kampeni ya kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Bagara mjini Babati mkoani Manyara, Nicodemus Tlaghasi (CCM).

Alisema wananchi wanatambua uwajibikaji wa Rais Magufuli kwao kwa namna anavyowatumikia, hivyo siyo rahisi wakatoa kura sehemu nyingine isipokuwa kwa CCM.

“Moto wa Rais Magufuli unaendelea kutimka kwa namna anavyochapa kazi hadi wapinzani wanajiondoa huko na kujiunga na CCM, siyo kwa madiwani tu hadi wabunge wa vyama tofauti,” alisema Musukuma.

Mbunge wa viti maalumu wa Mkoa wa Manyara, Esther Mahawe alisema ana uhakika wananchi wa Bagara watamchagua mgombea wa CCM ili kuunga mkono maendeleo yanayofanywa na CCM.

Mahawe alisema Serikali ya CCM inatekeleza miradi mingi ya maendeleo ikiwemo barabara, afya, elimu na maji, hivyo wananchi wataendelea kuiunga mkono CCM.

Mgombea udiwani wa Kata ya Bagara, Tlaghasi alisema wapinzani wana hofu ya kupoteza jimbo la Babati Mjini hivyo wafungashe virago.

“Hakuna suala la maendeleo walilolifanya zaidi ya kuendeleza malumbano ndiyo sababu mimi nikaondoka huko na kuja CCM ambapo ni utekelezaji wa maendeleo tuu,” alisema.

Uchaguzi huo utafanyika Agosti 12 mara baada ya Tlaghasi kujiuzulu nafasi hiyo kwa kujiondoa Chadema na kujiunga na CCM, akidai kuwa anamuunga mkono Rais John Magufuli na mkuu wa Mkoa huo Alexander Mnyeti.

Chanzo: mwananchi.co.tz