Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JPM kuweka historia Uchaguzi Mkuu

0abc65f1e66d124551770d3f9d1ef2d9 JPM kuweka historia Uchaguzi Mkuu

Fri, 24 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KWA mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi siasa nchini mwaka 1992, mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) anatarajiwa kumaliza mchakato wote Dodoma, kumwezesha kugombea nafasi hiyo.

Tangu kuanzishwa kwa mfumo huo na uchaguzi wa kwanza mwaka 1995, mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia CCM, umekuwa ukifanyika Dodoma lakini wagombea wamekuwa wakienda kwenye ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dar es Salaam kuchukua fomu za uteuzi.

Michakato ya ndani ya vyama vingine vya siasa, kupata wagombea wao imekuwa ikifanyika Dar es Salaam na pia wamekuwa wakichukua fomu za uteuzi ofisi za NEC jijini humo.

Mgombea urais kupitia CCM kwenye uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, Rais John Magufuli amemaliza mchakato wa ndani ya chama mjini Dodoma na anatarajiwa kuchukua fomu ya uteuzi jijini humo kwenye ofisi mpya za NEC eneo la Njedengwa.

Si hivyo tu, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage anatarajiwa kumtangaza kwenye ofisi hizo mshindi wa uchaguzi wa Rais, utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Rais Magufuli anagombea urais kwa mara ya pili, ambapo Julai 11 mwaka huu wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Dodoma, walimchagua kwa asilimia 100 agombee nafasi hiyo. Wajumbe wote 1,822 walipiga kura za Ndio.

Hapakuwa na kura ya hapana au kura iliyoharibika. Baada ya kutangazwa mshindi, Rais Magufuli alimchagua Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan awe Mgombea Mwenza wake.

Juzi, Rais alifungua ofisi ya makao makuu ya NEC, yenye majengo matatu likiwemo litakalotumika kumtamka mshindi. Tangu NEC ilipoanzishwa mwaka 1993, makao makuu yalikuwa Dar es Salaam. Ofisi hiyo iliyofunguliwa inajulikana kama Uchaguzi House.

“Hili ndilo jengo letu, tutakuja kuchukua fomu hapa, lakini mnaweza msije kuchukua mkasema Magufuli tu umepita” alisema Magufuli akiwatania viongozi wa vyama vya upinzani waliokuwepo kwenye hafla hiyo ya kufungua Uchaguzi House.

Baada ya Watanzania kupiga kura Oktoba 25 mwaka 2015, Mwenyekiti wa NEC wakati huo, Jaji mstaafu Damian Lubuva alimtangaza Magufuli kuwa mshindi wa kiti cha urais kwa kupata kura 8,882,935, ambazo ni sawa na asilimia 58.46 ya kura zote.

Mpinzani wake wa karibu kwenye uchaguzi huo, Edward Lowassa kutoka Chadema alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 ya kura. Kwa sasa Lowassa amerejea CCM. Kwa mujibu wa NEC mwaka 2015, watu 23,161,440 walijiandikisha kupiga kura na 15,596,110 sawa na asilimia 67.34 ya waliojiandikisha walipiga kura Oktoba 25.

Katika uchaguzi huo wa 2015, kulikuwa na wagombea wanane wa urais wa Tanzania, ambao ni Rais Magufuli wa CCM, Anna Mghwira wa Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), Edward Lowassa wa Chadema na Fahmi Dovutwa wa United People’s Democratic Party (UPDP).

Wengine ni Hashim Rungwe Spunda wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Janken Kasambala wa National Reconstruction Alliance (NRA), Lutalosa Yembe wa Alliance for Democratic Change (ADC), Macmillan Lyimo wa Tanzania Labour Party (TLP).

Kwa sasa Anna ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Lowassa tayari yupo CCM. Wakati wa uzinduzi wa jengo la NEC juzi, viongozi kadhaa wa vyama vya upinzani walikuwepo, ambao ni Kiongozi wa CCK, David Mwaijojele, wa SAU Bether Mpale, wa NLD Oscar Makaidi, wa DP Philip Fumbo na wa UMD Massodo Kamani.

Wengine ni Mohammed Aboud wa Demokrasia Makini, wa UPDP Twalib Ibrahim, wa TLP Richard Lyimo, wa Chaumma Kayombo Kabutai, wa ADC Queen Cuthbeth, wa Ada -Tadea John Shibuda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, wa UDP John Cheyo na James Mbatia wa NCCRMageuzi.

Rais Magufuli alivitaka vyama vya siasa, kufanya kampeni kistaarabu bila kutukana wakati wa kunadi sera, ili wananchi wawapime na kuchagua wagombea wanaowataka. Uteuzi wa wagombea urais wa Tanzania utafanyika Agosti 25 na kampeni zinatarajiwa kuanza Agosti 26 na zitamalizika Oktoba 27.

Chanzo: habarileo.co.tz