Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JPM apania Mbeya ipae kiuchumi

9391df39cf76d38e0892cc15ebb6a5f6.png JPM apania Mbeya ipae kiuchumi

Thu, 1 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli amesema mkakati mkubwa umewekwa wa kuubadilisha Mkoa wa Mbeya kuwa lango kuu la uchumi na utalii katika Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini sambamba na kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya ili kuhudumia nchi jirani.

Akihutubia maelfu ya wanachi kwenye Uwanja wa Ndege wa Zamani wa Mbeya jijini humo jana, Rais Magufuli alielezea mapenzi yake kwa Mkoa wa Mbeya na kusema anaupenda na anataka kuubadilisha kuwa lango kuu la uchumi na utalii sambamba na kituo umahiri wa huduma za jamii ikiwemo tiba.

“Nina mapenzi ya dhati na Mbeya, ninataka kuifanya iwe lango kuu la utalii na uchumi katika ukanda huu wa Nyanda za Juu Kusini, huduma za jamii ikiwemo afya, elimu tutaziboresha miaka mitano ijayo, nataka iwe hivyo na ndivyo Ilani yetu ya CCM inavyosema,” alisema Rais Magufuli.

Akielezea jinsi ya kufanikisha mikakati hiyo, alisema katika sekta ya afya wamepanga kuimarisha miundombinu ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, ikiwemo kukamilisha jengo la kisasa la mama na mtoto katika Hospitali ya Meta.

Alisema maboresho hayo yameanza hospitalini hapo na yakikamilika itakuwa na uwezo wa kuhudumia wanawake 200 kwa wakati mmoja na kuwa na vyumba vya upasuaji, vya kujifungulia na wodi za wagonjwa wenye uangalizi maalumu (ICU).

Alisema mradi huo mkubwa na wa kisasa una thamani ya Sh bilioni 9.2. Sambamba na mradi huo, pia mkoa huo utaimarishwa na huduma za kibingwa katika hospitali ya kanda kwenye magonjwa ya moyo, figo na kansa.

“Tunataka tuimarishe huduma za kijamii za afya hapa, ili tunaposema tunaibadilisha Mbeya kuwa lango kuu la uchumi na utalii, pia huduma za jamii za tiba za kibingwa zitolewe hapa na tupate wateja kutoka nchi jirani,” alisema Rais Magufuli anayeomba ridhaa ya Watanzania aongoze kwa muhula wa pili.

Alisema nguvu kubwa itakuwa kwenye kuimarisha hospitali nyingine za mkoa huo na kwamba ndani ya miaka mitano iliyopita, wamepunguza idadi ya vifo vya wajawazito na watoto wachanga.

Kuhusu miundombinu, alisema moja ya kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa eneo lolote ni ubora wa miundombinu. Hivyo katika kubadilisha mkoa huo, serikali ndani ya miaka mitano imepanga kukarabati na kujenga miundombinu ya barabara, reli, maji na umeme ili kuhakikisha inaunganisha wananchi wa maeneo ya uzalishaji na masoko.

Alisema katika eneo hilo la miundombinu, jumla ya Sh bilioni 252.36 zinatumika kuboresha na kukarabati barabara za Kikusya, Ipinda, Matema Beach, barabara ya Chunya hadi Makongorosi, Mafinga hadi Mkwajuni na pia kuboresha barabara za mjini kwa umbali wa kilometa 11.

“Tunaibadilisha Mbeya, itakuwa jiji la kisasa kupitia mradi mkakati wa kuboresha majiji. Jiji la Mbeya lipo kati ya majiji nane yanayojengwa barabara zake za mjini.

Jumla ya mradi wote katika maeneo hayo nane ni shilingi bilioni 796.52,” alibainisha Rais Magufuli. Alisema iwapo watapewa ridhaa ya kuongoza awamu ya pili, serikali itakamilisha ujenzi wa barabara zilizoanza ikiwemo barabara za Mbambo, Makete, Kitulo, Makongorosi hadi Mkiwa, Ileje, Ngana, Kasumulo, Katumbasongwe, Kiwira Port na Mbeya -Igawa na kupanua daraja ya Ipyana.

Kadhalika katika kukabiliana na msongamano, ujenzi wa barabara ya Iyole hadi Songwe kwa kiwango cha lami utaanza. Kuhusu usafiri wa maji, alisema ndani ya miaka mitano, serikali imeimarisha usafiri kwenye bandari ya Ziwa Nyasa kwa kununua meli mpya za Mv Njombe na Mv Mbeya II.

Kuhusu kufanya Mbeya kuwa lango la utalii na uchumi kwenye eneo la usafiri wa ndege, wamedhamiria kupanua Kiwanja cha Ndege cha Songwe, ambako zitatumika Sh bilioni 14.7 kwa ukarabati, ikiwemo kuongeza jengo la abiria, kuongeza njia ya kurukia ndege, kuweka taa na kufunga rada ili ndege kubwa zitue muda wote.

“Tutafanya hayo yote ndani ya miaka mitano ijayo, tunataka kuibadilisha Mbeya, ndege kubwa zitue hapa muda wote, lakini kufanikiwa kwa haya kutategemea na ninyi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema yote yatafanikiwa kwa urahisi wakiwachagua wagombea wa CCM. Aliomba wananchi wamchague Dk Tulia Akson kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, kwani amefanya mengi katika jimbo hilo licha ya kwamba hakuwa mbunge.

“Ndio maana nawaomba nileteeni Dk Tulia, nishauriane naye pia jinsi ya kugawa Mbeya iwe na wilaya mbili kama yalivyo majiji mengine mfano Dar es Salaam na Mwanza…hata Sugu (mbunge anayemaliza muda wake – Joseph Mbilinyi) naye namuomba anipe kura, huu sio wakati wa kubishana, ni wakati wa maendeleo na maendeleo hayana chama,” alisisitiza Rais Magufuli.

Aliwaomba pia wananchi wa Mbeya, kuwachagua madiwani na wabunge wengine wa CCM katika majimbo ya mkoa huo.

Aliwaagiza madiwani hao endapo watachaguliwa, kazi yao kwanza wakae kikao wapange jinsi ya kuipanga Mbeya na kuigawa iwe na wilaya mbili, kwa sababu moyo wake uko kwenye jiji hilo.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka mitano kitaifa, Rais Magufuli alisema wameimarisha huduma za jamii huku wakijenga hospitali za rufaa 10, zahanati zaidi ya 1,198,vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 99 na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa vya thamani ya Sh bilioni 232.

Pia wameimarisha huduma za afya na kufanya upanuzi katika Hospitali ya Kanda kwa kujenga jengo la wazazi, ununuzi wa vifaa tiba mfano CT Scan, ultrasound, CR kwa gharama ya Sh bilioni 8.84.

Katika ukarabati huo, pia hospitali za mkoa huo sita za wilaya zimenufaika ikiwemo hospitali ya Busokelo, Mbarali, Mbeya Jiji, Rungwe na Mbeya Halmashauri.

Kuhusu elimu, mkoa huo umejengewa madarasa 1,073, ukarabati wa shule kongwe nne ikiwemo Loleza, Mbeya, Rungwe na Iyunga ambazo zilikuwa zimechakaa.

Aidha, alisema ndani ya miaka mitano ijayo iwapo CCM itachaguliwa, wamedhamiria kujenga shule mpya 26 kila mkoa shule moja ya sayansi na lengo ni kuongeza udahili wa wanafunzi wa mchepuo huo.

Pia ujenzi wa nyumba za walimu kwa shule za msingi na sekondari 229, ujenzi wa maktaba nane, hosteli mbili zenye uwezo wa kulaza wanafunzi 1,000 na ujenzi wa kumbi za mihadhara mbili katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) kwa gharama ya Sh bilioni 3.1 na vyuo vingine.

Pia mkoa huo umenufaika na miradi mingine ikiwemo ya maji 52 yenye thamani ya Sh bilioni 22.5 na miradi hiyo ni pamoja na ule wa Shongo Mbalizi, Mawindi Kapapa, Mwakaleli na mingine inaendelea.

Pia kwenye sekta ya nishati jumla ya vijiji 385 zimeunganishwa umeme hadi sasa. Kuhusu vitambulisho vya wamachinga, mgombea huyo alisema vitaendelea kutumika kwa kuwa vina faida nyingi na sasa vimewezesha watu wa kundi hilo kupata mikopo benki, jambo ambalo awali lilikuwa gumu.

Chanzo: habarileo.co.tz