Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JPM alivyotumia ilani kushinda

F7f4c2e5cdceca4f825a1b115cde4e67 JPM alivyotumia ilani kushinda

Thu, 5 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

LEO ni shangwe kila kona ya nchi kutokana na ushindi mkubwa alioupata Rais John Magufuli katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Kwa muda wa miezi kadhaa iliyopita, Watanzania wamekuwa kwenye hekaheka ya mchakato mzima wa uchaguzi ambao mwishowe, walimchagua na kumrejesha tena madarakani kwa muhula wake wa pili Rais Magufuli.

Kiongozi huyo alipata ushindi kwa sababu mbali mbali za kukubalika kwake ikiwemo namna alivyotekeleza kwa vitendo Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020, lakini pia mambo makubwa ya maendeleo yaliyobainishwa katika ilani ya chama hicho ya mwaka 2020-2025.

Katika awamu yake ya kwanza ya uongozi ya muda wa miaka mitano, pamoja na mafanikio mengine, Rais huyo ameifanya nchi hiyo kuingia kwenye kundi la nchi zenye kipato cha uchumi wa kati, huku ikiongoza duniani katika nchi za uchumi wa chini kwa kuwa na ubunifu katika uchumi.

Katika kipindi chake hicho, alionesha kwa vitendo utendaji wake kwa kupambana na mafisadi, kuboresha utendaji wa umma, kuondoa urasimu, kudhibiti wizi na matumizi mabaya ya serikali.

Aliboresha miundombinu kwa kuunganisha mikoa kwa mikoa na nchi za jirani kwa barabara za lami, kuanzisha miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), ufufuaji wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Arusha, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), lakini pia kuboresha zaidi huduma za elimu na afya.

Sasa, amepewa tena nafasi ya kuwatumikia Watanzania na kumalizia miradi ya maendeleo, mipango na mikakati ya kujenga uchumi wa Tanzania na maendeleo ya Watanzania kwa ujumla, ambako leo anaapishwa rasmi kutekeleza wajibu wake huo.

Katika kipindi cha miaka mitano, Rais Magufuli amebainisha vipaumbele vyake vya kuboresha zaidi huduma za kijamii kama vile afya, elimu, maji, miundombinu, nishati na madini, kupambana na rushwa na ufisadi, lakini kubwa zaidi kuupaisha zaidi uchumi wa Tanzania.

Akielezea mipango iliyopo kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020-25 yenye kurasa 303, Rais Magufuli anataja vipaumbele sita vitakavyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Vipaumbele hivyo ni pamoja na kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi, utalii sanaa na michezo, usafiri na mawasiliano, afya na maji na kutoa ajira milioni nane.

Rais huyo alifafanua kuwa kwa upande wa uvuvi itajengwa bandari ya uvuvi katika ukanda wa Pwani, kuongeza uzalishaji wa vifaranga na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki.

Eneo la umwagiliaji, alibainisha kuwa mipango iliyopo kwenye ilani ni kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 511,383 hadi kufikia milioni 1.2 na kuimarisha huduma za ugani na vyama vya ushirika.

Kwa upande wa ufugaji, alielezea kuwa ilani hiyo imepanga kuongeza eneo la ufugaji kutoka hekta milioni 2.7 hadi kufikia hekta milioni sita na kuongeza vituo vya kuzalisha mbegu bora ili kuwa na tija ya mifugo nchini.

Aidha, katika sekta ya madini, Serikali hiyo ya Awamu ya Tano itaimarisha zaidi, kudhibiti na kusimamia uchimbaji madini ili iweze kunufaisha taifa, ikiwa ni pamoja na kuwezesha wachimbaji wadogo wafanye shughuli zao kwa tija.

“Tutaimarisha masoko kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji madini na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji madini,” alisema Rais Magufuli wakati alipokuwa akiomba kura kwa wananchi.

Alibainisha kuwa katika Ilani ya CCM wamedhamiria wananchi ndio wawe wamiliki wakuu wa rasilimali zikiwemo madini na kusisitiza kuwa leseni na vibali vitaendelea kutolewa kwao ili wafanye shughuli hiyo kwa kujiamini na kujipatia fedha.

Alisema katika kutekeleza kipaumbele hicho, atahakikisha miradi mikubwa ya kimkakati inaajiri vijana wengi zaidi wa Kitanzania katika kuchochea ukuaji wa uchumi hususani katika sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi za kilimo, mifugo, uvuvi, madini, maliasili na sekta ya huduma za kiuchumi pamoja na utalii.

Mambo mengine yatakayozingatiwa ni kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za ujasiriamali ikiwemo kuwapatia mafunzo na kuwaunganisha na taasisi na asasi za utoaji mikopo yenye riba na masharti nafuu.

Pia kuwahamasisha na kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika utamaduni, michezo na sanaa kwa ajili ya afya bora na burudani na kuongeza fursa za ajira na kipato.

Katika afya, Rais Magufuli alisema watumishi mbalimbali wa kada ya afya wataongezwa kufikia 25,000 pamoja na kukamilisha ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na rufaa.

Katika sekta ya maji, kwa mujibu wa ilani hiyo mpya, Rais Magufuli anasema atahakikisha asilimia 90 ya Watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama.

Katika kipaumbele cha usafiri mawasiliano, anasema serikali yake itanunua meli ya kubeba mizigo katika Bahari ya Hindi, kujenga meli tatu na kununua meli ya kubeba mabehewa ya treni.

Katika usafiri wa anga, anasema wanatarajia kununua ndege mpya tano na kati ya hizo mbili zitakuwa za masafa marefu, mbili za masafa ya kati na moja ya mizigo.

“Nitaimarisha pia Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kiwe na uwezo wa kutoa wataalamu mbalimbali wa anga. Lakini pia nitaongeza matumizi ya intaneti kutoka asilimia 43 ya sasa hadi kufikia asilimia 80,” alisema Rais Magufuli akinukuu ilani hiyo ambayo imewavutia wapigakura kumrejesha madarakani.

Akizungumzia miundombinu, anasema bado serikali yake itaendelea na mpango wa kuunganisha mikoa kwa barabara za lami, hususani ile ambayo haijaunganishwa.

Alitaja baadhi ya barabara hizo zitakazojengwa kwa kiwango cha lami kuwa ni pamoja na ujenzi wa kilometa 359 kutoka Mpanda – Tabora, Manyoni – Tabora – Mpanda – Kigoma – Nyakanazi na ile ya Lupilo – Malinyi – Kilosa pamoja na madaraja makubwa saba yakiwemo ya Busisi na Selander.

“Mambo ni mengi, huwezi kutatua changamoto zote kwa siku moja, lakini pia ukiwa kiongozi lazima uwaambie ukweli wananchi, usiwadanganye, maana tunasikia mgombea mmoja anasema akichaguliwa wananchi hawatalipa kodi, ni taifa gani halilipi kodi?

“Hata Marekani wanalipa, ndio maana nasema changamoto zipo na tunaendelea kuzitatua, msinipime kwa miaka mitano, nipimeni kwa miaka kumi. Msikubali kudanganywa hadi sasa sijaona anayeweza kunifikia hata robo kwa hao wanaozunguka kuwania nafasi hii, sasa mkiwapa mtaenda kuanza moja,” alisema Dk Magufuli akiomba kura.

Rais Magufuli alisema yeye na wanaCCM wenzake wana uwezo wa kujenga uchumi mkubwa zaidi kwa kuwa mbinu za kutafuta fedha anazo, uwezo wa kuwabana mafisadi anao, lakini pia nia ya kuyafanya hayo anayo.

Anasema moja ya mambo ambayo Watanzania watayafurahia katika kipindi chake cha miaka mitano ijayo ni kusafiri kwa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam kwa muda wa saa nane tu.

Lakini pia amepanga kuhakikisha Watanzania wote wenye uwezo wanakuwa na bima ya afya ili kuboresha maisha yao na kuwawezesha kuwa na afya njema itakayowasaidia kuendelea kuchapa kazi.

Anaeleza maeneo mengine ambayo serikali yake imefanya vizuri kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi iliyomaliza muda wake ya mwaka 20150-2020 kuwa ni afya, elimu bure ambako jumla ya Sh trilioni 1.6 zimetumika, maji na umeme ambako ni vijiji 2,600 pekee ndio havina umeme kati ya vijiji zaidi ya 12,000 nchi nzima.

Chanzo: habarileo.co.tz