Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JPM: Nataka kuacha alama

D7de68cf23f9635e975b9332d5324b18 JPM: Nataka kuacha alama

Wed, 2 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli amesema katika miaka mitano iliyopita, kazi kubwa zimefanywa na ushahidi ni utekelezaji wa wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2015-2020.

Magufuli ametoa mifano kadhaa, vikiwemo vijiji 9,570 vilivyounganishwa na umeme.

Amesema Tanzania ina jumla ya vijiji 12,228, na wakati wanaingia madarakani mwaka 2015, ni vijiji 2,018 pekee ndivyo vilikuwa na umeme, huku uzalishaji wa umeme ukiwa chini ya megawati 1,000.

Amesema anataka miaka kumi ya uongozi wake itapomalizika, awe ameacha alama kwa wananchi wakikumbuka mambo makubwa aliyowafanyia.

Alisema hayo alipozungumza na wananchi wa Ikungi wilayani Singida, aliposimama kuwasalimia na kuomba kura.

Akifafanua, Magufuli alisema ndani ya miaka mitano sasa vijiji 9,570 vimeunganishwa na umeme; na kwamba vilivyobaki ni vijiji 2,600 tu. Aliahidi kwamba ndani ya miaka miwili ijayo, vijiji vyote nchini vitakuwa vimeshaunganishwa, vikiwemo vya maeneo ya Ikungi wilayani humo.

“Nasema ukweli, sitaki kuwadanyanya na jua linawaka, na mimi sipendi uongo, ni lazima tutimize ahadi hizo, ili hata tukiondoka niwe nimeacha alama kwa wananchi kukumbuka mambo makubwa tuliyoyafanya kwa manufaa yao,” alisema Magufuli.

Magufuli alisema ndani ya miaka mitano ijayo, iwapo wananchi watamchagua tena, serikali itahakikisha inaongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme, kwa kuongeza megawati 5,000 zinatazopatikana kwenye vyanzo vitakavyojengwa, ikiwemo kwenye Bwawa la Julius Nyerere lililopo Mto Rufiji.

Alisema Ilani ya CCM ya sasa yenye kurasa 303, inaelezea kazi zinazopaswa kutekelezwa ndani ya miaka mitano ijayo ;na kwamba wao wamejipanga kutekeleza kwa kiwango kikubwa zaidi. Aliwaomba wananchi kuwachagua wabunge na madiwani kutoka CCM.

“Ndio maana ninaomba mniletee wabunge wa CCM, ili niwabane kisawasawa, kazi ni ibada, ni utumishi, sio ukubwa, tushikamane kipindi hiki cha kampeni twende mbele, tushikamane kama tulivyoshikamana kwenye corona. Mimi ni yuleyule, sijabadilika na sitabadilika, nitaendelea kuwa mtumishi wenu. Kazi ya urais ni ya kujitolea, unakatishwa tamaa, unatukanwa, lakini sikati tamaa, ndio wananipa nguvu ya kuendelea kuwatumikia’’alisema Rais Magufuli.

Alisema pamoja na kushikamana, ni vyema pia katika kipindi hiki, taifa likamtanguliza Mungu na kutambua kuwa yanayoshindikana kwa wanadamu Mungu anayaweza.

“Tulisema na Mungu kipindi cha corona na akasikia. Nitoe wito duniani kwamba wasioamini Mungu waamini yasiyowezekana kwake yanawezekana, ndio maana nawaomba tuijenge amani yetu. Akipita mtu anasema hadi kieleweke, ogopeni. Unaweza kumpenda binti ni Chadema wewe ni CCM, mnaoana, kwani mapenzi hayatanoga? Tunaomba tushikamane. Tudumishe amani yetu, siasa isitugawe”’alisema Magufuli.

Akizungumza kwenye kampeni akiwa Singida mjini, Magufuli alisema miradi mingi mkoani Singida imetekelezwa na kwamba zaidi ya Sh bilioni 470.4 zimetumika kwa kazi hiyo.

Alisema, kwenye miundombinu ya barabara na uwekaji taa barabarani, zimetumika zaidi ya Sh bilioni 17.

Kuhusu miradi mingine iliyotekelezwa mkoani humo, Rais Magufuli alisema ujenzi wa vituo viwili vya afya vya Ihanja na Sepuka Wilaya ya Ikungi, vimegharimu Sh milioni 900 na ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya hiyo umegharimu Sh bilioni 1.5.

Chanzo: habarileo.co.tz