Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ilani ya CCM yatabiriwa makubwa

580f33e60b603ab673007f919957e813.png Ilani ya CCM yatabiriwa makubwa

Sun, 19 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

VIPAUMBELE sita vya Ilani mpya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), vimefagiliwa na watu wa kada tofauti, wakisema vina msingi imara, uliojengwa na Ilani ya 2015-2020. Hali hiyo inaakisi kwamba chama kitaendelea kuongoza; na nchi itashuhudia mafanikio makubwa zaidi.

Miongoni mwa waliochambua vipaumbele hivyo, wamepongeza hatua ya chama kuendelea kubeba kilimo na ajira kwa vijana kutoka Ilani ya 2015-2020 inayomalizika na kuyapa kipaumbele masuala hayo kwenye Ilani ya 2020-2025.

Miongoni mwa watu waliozungumza na Habari- Leo wanasema wakati wakisubiri kuona yaliyomo ndani ya ilani hiyo, itakayoanza kusambazwa hivi karibuni, vipaumbele vilivyotajwa vimedhihirisha kwamba chama kinafahamu mambo ya msingi yanayogusa wananchi.

Ilani ya mwaka 2020-2025 ilipitishwa hivi karibuni na Mkutano Mkuu wa chama mjini Dodoma. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Ally Bashiru, Ilani ipo katika hatua ya kuchapishwa na itakuwa tayari kusambazwa wakati wowote kuanzia mwanzoni mwa mwezi ujao.

Vipaumbele Dk Bashiru alitaja vipaumbele sita ni kulinda na kuimarisha misingi ya utu, usawa, haki na uongozi bora kudumisha amani, umoja, mshikamano wa taifa na muungano. Vingine ni kukuza uchumi wa kisasa, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi na kuleta mapinduzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya nchi .

Vipaumbele vingine ni kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi bora mijini na vijijini; Kuchochea matumizi ya tafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi.

Kishindo utekelezaji “Tumeona kwa jinsi ambavyo Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 ilivyotekelezwa kwa kasi … Kwa msingi huo, utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 ni mwendelezo wa msingi mzuri uliojengwa na ilani iliyopita,” alisema Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Chirongo Keregero.

Alitoa mfano wa kipaumbele cha kulinda na kuimarisha misingi ya utu, usawa na haki na kusema Serikali ya Awamu ya Tano, imefanikiwa kuwezesha haki kutendeka kwa raia wengi, ikiwamo kuboresha nidhamu kwenye utumishi wa umma.

Mchambuzi Magid Mjengwa alitaja kipaumbele cha uchumi wa kisasa na jumuishi, kina msingi imara wa utekelezaji kutokana na ujenzi wa miundombinu uliofanyika kwa kasi kubwa chini ya Ilani ya 2015-2020.

“Unapoingia kwenye miundombinu, zile ni ajira… hata hizo ajira milioni nane zitazidi kutokana na wingi wa miradi ya kimkakati iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa,” alisema Mjengwa.

Mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) katika Mto Rufiji, utakaozalisha megawati 2,115 ni miongoni mwa miradi inayotegemewa kuchangia utekelezaji wa vipaumbele kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za kijamii.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) Wilaya ya Kibiti na Rufiji mkoani Pwani, Max Masero alisema kilimo ni sekta nyeti, ambayo chama makini hakiwezi kuacha kuipa kipaumbele.

Masero alisema anaamini ilani itakuja na ufafanuzi zaidi namna ya kuendesha kilimo, uvuvi na ufugaji wenye tija kwa kuwezesha kuwapo malisho bora, masoko na kuelekeza idadi maalumu ya mifugo.

“Nina imani tunakwenda kupata matokeo makubwa katika miaka mitano ijayo,” alisema Masero.

Alishauri CCM na serikali kutafsiri ilani hiyo, kuhakikisha nchi inaondokana na kilimo cha asili, kwa kuboresha miundombinu ya umwagiliaji na kujenga maghala ya kisasa kuhifadhi nafaka. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uchumi, Segere Yusuf alisema kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ilikuwa ni kurudisha rasilimali uchumi kwa watu.

“Kwa kuwa zoezi la kwanza limefanyika na limefanikiwa… Katika Awamu ya Tano kipindi cha pili, kazi kubwa inategemea kurudisha uchumi kwa watu kupitia maeneo muhimu kama vile kilimo,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz