Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Idadi ya wabunge yakwamisha muswada, Ndugai awatetea

16268 Muswaada+pic TanzaniaWeb

Sun, 9 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba 2 wa mwaka 2018, jana ulikwama kupitishwa bungeni baada ya akidi ya wabunge inayohitajika kupiga kura ya uamuzi kikanuni kutotimia.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuomba kiti cha spika kuhusu utaratibu kwa kutumia kanuni ya 77 ya Bunge, akisema akidi iliyokuwepo bungeni haijafikia nusu ya idadi ya wabunge wote kama kanuni inavyotaka.

Mdee alisema ingawa idadi ya wabunge wote ni 393, lakini alihesabu waliokuwapo ukumbini kuwa walikuwa 67.

Alipoulizwa nje ya Bunge kuhusu kutotimia kwa akidi, Spika Job Ndugai alisema zipo sababu mbalimbali ikiwemo jana Ijumaa kuwa ni siku ya ibada kwa waumini wa dini ya Kiislamu.

“Wabunge wengi sana waumini wa dini ya Kiislamu wanakuwa wanaenda misikitini hiyo inaweza kuwa ni sababu mojawapo, lakini pia na taarifa baadhi ya kamati zimesafiri kwenda kukagua shughuli nyingine za kiserikali ili waweze kutumia Jumamosi na Jumapili kwa kazi hiyo,” alisema.

“Kwa hiyo ni mchanganyiko mkubwa tu lakini siyo makusudi kwamba labda kuna mgomo ama nini. Ni jambo lililojitokeza tu ambalo linarekebishika.”

Muswada huo uliowasilishwa jana na waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi unapendekeza marekebisho katika sheria 13 ikiwemo ile ya Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).

Hoja ya Mdee

Kwa mujibu wa kanuni ya 77(1) akidi kwa kila kikao cha Bunge cha kufanya uamuzi itakuwa nusu ya wabunge wote kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 94 ya Katiba.

Awali akijibu hoja ya Mdee ya kutopiga kura, mwenyekiti wa kikao cha Bunge jana, Najma Giga alisema wataangalia suala la idadi ya wabunge utakapofika wakati wa kupiga kura.

Baada ya Bunge kumaliza kupitia kifungu hadi kifungu cha muswada huo, Mdee alinyanyuka tena na kuomba kuhusu utaratibu akitaka kanuni kuzingatiwa.

“Mheshimiwa mwenyekiti utoe maelekezo kengele ipigwe walioko nje waje, makatibu wahesabu wabunge walioko bungeni halafu utaratibu wa kikanuni ufuatwe,” alisema.

Wakatwe posho

Baada ya hoja ya Mdee, naibu waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya alishauri kuwakata posho wabunge ambao hawakuwepo wakati huo isipokuwa wale waliokwenda msikitini na wale wenye ruhusa.

Hata hivyo, Najma alitaka kupigwa kwa kengele na kusubiriwa kwa dakika tatu ili wabunge waliopo nje ya ukumbi waingie ndani, hatua ambayo hata hivyo haikuwezesha kupatikana kwa akidi.

“Kwa vile kazi zote zimeisha na imebakia uamuzi tu naahirisha Bunge hadi Jumatatu saa 3.00 asubuhi,” alisema mwenyekiti huyo.

Ndugai awakingia kifua

Kuhusu pendekezo la Manyanya la kukatwa posho kwa wabunge waliokuwa hawapo bungeni bila taarifa, Ndugai alisema si vizuri kuwaza habari ya posho kila dakika.

“Watu hawaji bungeni kwa sababu ya posho. Wanakuja kufanya kazi kama watu wazima na posho ni support kwamba anakuwepo hapa lazima ale alale,” alisema.

Alisema wameliona jambo hilo na watafuatilia kama ni suala linalojirudiarudia na kuchukua hatua ikiwemo kutopanga shughuli zinazohitaji kura ya uamuzi Ijumaa.

Wanachama TLS wabanwa

Awali Serikali iliwasilisha marekebisho ya (TLS) sura namba 307 ambapo sasa watumishi wa umma, madiwani, wabunge na viongozi wa vyama vya siasa hawataruhusiwa kugombea ujumbe wa baraza la chama hicho.

Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaru alisema marekebisho hayo yanaongeza vifungu vinavyoweka sifa za mtu kuchaguliwa kuwa mjumbe wa baraza hilo ambapo mjumbe husika anatakiwa kuwa raia wa Tanzania, na awe amethibitishwa kuwa na akili timamu.

Sifa nyingine zinazoongezwa ni kuwa hajatangazwa kuwa mfilisi na amethibitishwa na kamati ya uteuzi kuwa na weledi.

Pia, alisema muswada huo unapendekeza kuongeza kifungu kinachohusu kumzuia mjumbe wa baraza kujihusisha na shughuli za kisiasa.

Muswada huo umeainisha shughuli za kisiasa zinazokatazwa ni pamoja kugombea nafasi za kisiasa katika chama cha siasa, kupiga kampeni za kumuunga mkono au kumpinga mgombea yeyote katika chaguzi za kisiasa. Shughuli nyingine watakayozuiwa wajumbe hao iwapo muswada huo utapitishwa ni kutoa hotuba za kampeni, kukusanya michango au harambee kwa ajili ya chama cha siasa na kupanga au kusimamia maandamano ya kisiasa au mikutano ama kuwa na nafasi ya madaraka katika vyama vya siasa.

“Inapendekezwa na ibara hii kuwa iwapo mjumbe atakiuka masharti atakuwa amefanya makosa makubwa ya kimaadili na ikitokea, mwanasheria mkuu wa Serikali anaweza kupeleka maombi katika kamati ya mawakili ili mhusika aondolewe kwenye orodha ya mawakili,” alisema Dk Ndumbaro.

Vilevile muswada huo unapendekeza utungaji wa kanuni ufanywe na baraza kwa kushauriana mwanasheria mkuu wa Serikali na kisha kanuni hizo zitatatikiwa kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali.

Dk Ndumbaro alisema kamati hiyo imeridhia mapendekezo ya Serikali kwa sababu yana lengo la kuimarisha misingi ya nidhamu, vigezo na mipaka ya kitaaluma kwa mawakili wa kujitegemea.

AG, waziri wajibu

Akijibu hoja za wabunge kuhusu muswada huo, Waziri Kabudi alisema marekebisho ya sheria ya TLS hayamlengi mtu na kwamba, ilitungwa wakati wa ukoloni.

Alisema TLS inagusa taaluma ambayo ni vyema ikasimamiwa kwa umakini kuliko taaluma nyingine yoyote.

Chanzo: mwananchi.co.tz