Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hoja za mafanikio makubwa zaibeba CCM

4f7cb02ff109e173074e514f6f3decdf Hoja za mafanikio makubwa zaibeba CCM

Sun, 25 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ZIMEBAKI siku tatu kabla ya wagombea urais kuhitimisha tambo za kuomba ridhaa ya kuongoza nchi huku tathimini ya watu tofauti ikitaja Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa ushindi wake uko wazi kutokana na kinavyoonesha mambo yaliyofanywa na serikali ikilinganishwa na vyama vilivyojikita kukosoa na kubeza.

Tangu CCM ilipozindua kampeni zake Agosti 29 mwaka huu mjini Dodoma, mgombea urais, John Magufuli, mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan na makada wengine wamekuwa wakieleza maendeleo yaliyofanywa na kuainisha mambo mengine makubwa yatakayotekelezwa kikichaguliwa tena.

Vyama vingine vya siasa vimejikita kukosoa, kubeza yaliyofanywa na serikali ya CCM na kushindwa kueleza sera za namna watakavyoendeleza yaliyofanyika, jambo ambalo linatajwa kuwa dosari machoni pa wapiga kura wanaoona uhalisia wa utekelezaji.

“Nimebahatika kuhudhuria kampein za vyama vitatu tofauti. Nilibaini Chama cha Democrasia na Maendeleo (Chadema) wamekuwa wakibeza maendeleo yaliyofanywa na serikali lakini wameshindwa kuandaa sera zinazojikita wapi wataendeleza maendeleo ambayo serikali imeyafanya,” alisema mwanasiasa mkongwe, Pius Ngeze.

Ngeze ambaye ni mwandishi wa vitabu, katika kampeni za CUF ambazo amehudhuria, pia zimejikita kutumia upungufu wa baadhi ya mambo kujinadi kuwa watayatafutia ufumbuzi bila kuonesha watafanyaje.

Katika mahojiano maalumu na mwandishi kuhusu tathimini yake juu ya kampeni, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dk Abednego Keshomshahara, alisema vyama vilipewa muda wa kunadi sera zao lakini baadhi sera zake hazikujikita kuonesha watafanya nini isipokuwa kukosoa.

Shehe wa Mkoa wa Kagera, Haruna Kichwabuta alisema ameshuhudia vijana ambao hawana uelewa wa kutosha wakitumiwa vibaya kutoa lugha za matusi na kuongea mambo bila kutafakari.

"Mfano tumekuwa tukiona kupitia videdea vya kampeini vijana wakifanya vurugu,wakiendesha pikipiki vibaya na wakichochewa kwamba ukipiga kura ulinde kura ,sasa unajiuliza unalinda kura wewe ni tume?...Mimi kama kiongozi wa dini nasema warekebishe kabla ya uchaguzi, " alisema Kichwabuta.

Kiongozi wa wazee wa Mkoa wa Kagera, Samwel Masabala alisema wananchi wanachopenda kuona na kusikia kutoka kwa wagombea, ni ukweli kuhusu waliyofanya na watakayofanya kuwaletea maendeleo.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko alisema wagombea wamejitahidi kuwasilisha hoja zao ingawa alisisitiza kwamba wananchi wanataka kuelezwa vitu watakavyofanyiwa na serikali itakayoingia madarakani.

"Wagombea walijikita zaidi kueleza waliyofanya… huku wengine wakikosoa na kujibu mapigo badala ya kujikita kwenye sera," alisema Soko na kusisitiza umuhimu wa elimu ya uraia kwa wananchi waweze kuwa na maono ya kuchagua viongozi bora watakaoweza kuwaletea maendeleo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine Tanzania (SAUT) Dotto Bulendu alisema pamoja na wagombea wa urais kuwasilisha vizuri sera za vyama vyao, kumekuwa na changamoto ya kukosekana kwa fursa kwa wananchi kuuliza maswali wafahamu walivyoweza au watakavyoweza kuhudumia wananchi.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU), Profesa Gaudence Mpangala alisema, wananchi wana elimu ya kutosha ya kutafakari na kuchanganua yanayozungumzwa na wanasiasa kwenye kampeni na ndio watakaoamua ni nani wampe kura.

Alipozungumza na waandishi wa habari kabla ya kuzindua kampeni za CCM, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole alisema: “Niseme tu uchaguzi wa mwaka huu utajumuisha watu waliofanya kazi kubwa kwa nchi yetu na wale wanaobeza, sasa rai yangu wananchi wasipotoshwe wala kuhangaika na wale wasioguswa na maendeleo ya nchi yetu.”

CCM kupitia ilani yake ya mwaka 2020-2025, inaongozwa na kauli mbiu yaTumetekeleza kwa kishindo; Tunasonga mbele pamoja’ ikionesha namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imetekeleza kwa kishindo ilani ya mwaka 2015-2020.

Chadema kupitia kwa mgombea wake wa urais, Tundu Lissu, sehemu kubwa ya kampeni zake imekuwa ni kubeza na kukosoa juhudi zilizofanywa na serikali ikiwamo ujenzi wa miundombinu mbalimbali jambo ambalo limekuwa likifanya CCM na wafuasi wake ‘kujibu mapigo’.

Miongoni mwa wakosoaji, wamekuwa wakielezea miradi iliyotekelezwa na serikali kuwa ni maendeleo ya vitu huku wakirejelea uamuzi kama vile wa ujenzi wa reli ya kisasa, ununuzi wa ndege, mradi wa Mradi wa Umeme wa Maji Rufiji (RHPP).

Jambo lingine ambalo wamekuwa akibeza ni vitambulisho vilivyotolewa na serikali kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo (wamachinga) wakiwaambia kuwa wameibiwa.

Chanzo: habarileo.co.tz