Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hoja moto za Mchungaji Msigwa, Sugu kwenye mdahalo

Sugu Msigwaaaaaa Mchungaji Msigwa kulia na Sugu wakishiriki kwenye mdahalo huo uliorushwa na Kituo cha Televisheni ch

Sun, 26 May 2024 Chanzo: Mwananchi

Vigogo wawili wa Chadema wanaowania uenyekiti wa kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa na Joseph Mbilinyi 'Sugu' wamenyukana kwa hoja na kurushiana vijembe hadharani, huku kila mmoja akidai ni bora zaidi ya mwenzake.

Wagombea hao jana walishiriki katika mdahalo uliopewa jina: 'Nyasa tunakwenda na nani' uliorushwa mubashara na kituo cha televisheni cha Star TV, ukiwashirikisha pia mashabiki wa kila mgombea.

Sugu na Mchungaji Msigwa waliowahi kuwa wabunge kuanzia mwaka 2010 hadi 2020, wanatarajiwa kuchuana katika uchaguzi wa kanda ya Nyasa utakaofanyika Mei 29,2024 mkoani Njombe.

Kwenye uchaguzi huo, Mchungaji Msigwa ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema anatetea nafasi hiyo kwa mara ya tatu, wakati Sugu anawania kwa mara kwanza.

Kanda ya Nyasa inajumuisha mikoa ya Njombe, Mbeya, Iringa, Songwe na Rukwa.

Wawili hao walikutana kwenye mdahalo huo ambapo kila mmoja aliweka wazi anamheshimu mwenzake kulingana na uwezo wake, alivyojijenga kisiasa na mambo mengine ya kijamiii. Walinadi wanachokwenda kukifanya na waliulizwa maswali.

Walivyochuana

Mdahalo ulikuwa mzuri hasa wakati wa maswali na majibu kutoka kwa wafuasi wanaowaunga mkono wagombea.

Kada anayemuunga mkono Mchungaji Msigwa, Benjamin Chiseo alimuuliza Sugu endapo akipata ridhaa hiyo, ataongozaje chama pasipo kujali katiba ya Chadema.

Katika majibu yake, Sugu amesema atafuata katiba lakini atakwenda kutoa maoni ya kuiboresha ili kuondoa ombwe la viongozi kutumia upungufu wa katiba kufanya mambo kinyume na matakwa ya wananchama.

"Mfano haiwezekani wanachama 80 au 150 wanapiga kura kumchagua katibu, halafu kesho yake kamati ya utendaji ya kanda inabatilisha matokeo kwa watu sita kufanya uamuzi, sasa ndio upungufu nitakaokwenda kuyatolea maoni ili kufanyike maboresho," amesema Sugu.

"Sitatatumia upugufu wa katiba uliopo kuwaadhibu wengine, kuna watu walitumia vibaya upungufu huo ndio maana kuna vuguvugu la kutaka mabadiliko ya uongozi wa kanda huko chini, hili linakwenda kutokea hivi karibuni,” amesema.

Lakini kabla ya Sugu hajamaliza sentensi hiyo, Msigwa kabla ya kuruhusiwa na mwendesha mdahalo huo, alirukia na kujibu: “Sidhani kama itatokea.”

Sugu na Msigwa wakishikana mikono

Baada ya kuruhusiwa, Mchungaji Msigwa amejipambanua kwa kusema kwa mujibu wa katiba ya Chadema chombo cha mwisho cha kufanya uamuzi, ni kamati ya utendaji haijalishi hata kama kuna upungufu.

"Kwa kiongozi makini ataheshimu katiba iliyopo na kama anataka utawala bora ataheshimu kitabu hiki," amesema Msigwa, aliyekuwa Mbunge wa Iringa Mjini.

Muongozaji wa mdahalo huo, aliwauliza Msigwa na Sugu watawezaje kukabiliana au kuondokana makundi ndani ya chama hicho katika uongozi wao ili kuepusha mpasuko katika chama chao.

Msigwa alijibu kuwa kanda ya Nyasa inamhitaji kiongozi mwenye ujuzi, anayeunganisha na kukuza watu, anayeomba radhi anapokosea au aliye tayari kukosolewa, anayekemea na kusimamia misingi ya katiba ya Chadema.

"Hizi sifa ninazo nitakwenda kuboresha mafunzo, nimewajengea uwezo watu wengi wengine ni wabunge, hiki ndio ninachokifanya kanda ya Nyasa ili kuacha kizazi bora. Ili kanda ya Nyasa iendelee kuwepo inahitaji kiongozi shupavu jasiri na mwenye uelewa mpana na ujuzi wa kiongozi," amesema Msigwa.

Naye Sugu amesema atawaweka watu pamoja, kuwa mnyenyekevu, kutojikweza ili watu wamfikie, akijipambanua yeye ni mtu wa maono na kwa kuanzia ataanza mchakato wa ujenzi wa ofisi ya kanda ndani ya siku saba baada ya kushika madaraka.

"Unasema unawajengea uwezo vijana kwa programu ipi? Maana usipokuwa na programu, matokeo yake unatengeneza machawa wanaoshindwa kukuambia ukweli ikiwemo muda wako umekwisha badala yake wanakupigia makofi.

"Ndio maana nasema nakwenda kuanzisha programu maalumu zitakazo pata baraka za chama kwa ajili ya kufundisha vijana mambo ya uongozi na siasa kisha kupewa vyeti vitakavyowatambulisha sio kutengeneza 'machawa'," amesema Sugu.

Akitoa mrejesho wa maelezo ya Sugu, Msigwa amesema: “Rafiki yangu anasema anakwenda kufanya mimi nimefanya, nimekuwa mwenyekiti niliyefanya safari na nimetembelea majimbo yote 31 ya Nyasa, nimekuwa nikiwajengea uwezo vijana ili kujua itikadi za chama.”

"Lakini katika kuwafundisha vijana huwezi kuwapa wote unaposema natengeneza machawa, hata katika familia unaweza ukazaa watoto sio wote wakakusikiliza," amesema.

Hoja ya ofisi ya kanda Mwendesha mdahalo huo, alimuuliza Msigwa amekuwa mwenyekiti wa kanda lakini ameshindwa kujenga ofisi, huku mshindani wake akidhamiria kulitekeleza hilo.

Katika majibu yake, Msigwa amesema yeye na mpinzani wake waliwahi kuwa wabunge, lakini walishindwa kujenga ofisi ya jimbo, kusema mshindani wake atajenga ofisi ndani ya siku saba haitawezekana hata Chadema ilichukua miaka 30 kupata ofisi nzuri.

"Mimi ni mtu nisiyeamini katika majengo, bali uongozi ni katika kuwawezesha na kuwajenga watu. Kwangu suala la ofisi haliwezi kuwa kipaumbele isipokuwa watu," amesema.

Alipopewa nafasi tena Sugu amesema:"Mwenzangu amesema tulivyokuwa wabunge tumeshindwa kujenga, sasa nimeshanunua kiwanja kwa kuanzia. Nitaanza mchakato ndani ya siku saba kwa kuteua kamati ya ujenzi, uongozi uliopo ulikataa kwa kuona sifa zitakuja kwangu.

"Msigwa anahoji fedha natoa wapi? mimi ni mfanyabiashara mkubwa wa Mbeya, siwezi kukosa au kuwaambia watu wachangie saruji au mawe.Huwezi kuwaambia watu wachangie, wakati we hauchangii itakula kwako," amesema Sugu.

Hoja ya uwajibikaji

Daniel Ngogo alimuuliza Msigwa kama anaamini katika uwajibikaji wa pamoja na kama anaamini kwa nini kwa nyakati tofauti amekuwa akienda kinyume na misimamo ya kisera ya chama hicho hasa hatua ya Serikali ya kuwaahamisha wananchi wa Ngorongoro, Chadema hakiungi mkono lakini yeye amekuwa na mtazamo tofauti na chama.

Akijibu Msigwa alisema muuliza swali amejielekeza vibaya hakuwa na taarifa sahihi, yeye hajakwenda kinyume na msimamo wa chama chake, wakati suala Ngorongoro linatokea Chadema haikuwa imetoa msimamo wake.

"Wakati suala hili linatokea nilikuwa na mawazo yangu tofauti kama ambavyo (Tundu) Lissu amekuwa, tulitofautiana lakini baadaye chama kikatoka na msimamo ambao upo. Sikuwahi kupingana na chama ndio maana sikuitwa popote kujieleza, haya ni maneno ya barabarani kwa watu wasiofuatilia," amesema Msigwa.

Naye, Zephania Msofe alimuuliza Sugu kwamba alipokuwa mbunge (Mbeya Mjini) kwa miaka 10 Chadema ilikuwa ipo juu, kina nani waliokuwa viongozi.

Akijibu swali hilo, Sugu amesema wakati Nyasa iliongozwa na mwenyekiti Msigwa na katibu akiwa Frank Mwaisumbe ambaye hivi sasa amehamia CCM, Nyasa ilikuwa imara kutokana na kuwepo na watu wenye ushawishi akiwemo yeye na rekodi zipo.

"Nikiwa mbunge nilitembelea majimbo ya Mbeya na Songwe, matokeo yake mwaka 2015 tulipata wabunge kina Pascal Haonga, sasa yeye akiwa mwenyekiti wa miaka 10 na mbunge amezalisha majimbo mangapi kama sio Iringa Mjini pekee?” amehoji Sugu.

Hoja ya rushwa

Katika mdahalo huo, Mchungaji Msigwa na Sugu waliulizwa watadhibiti vipi vitendo vya rushwa ndani ya Kanda ya Nyasa ili wanachama wachague viongozi wanaowahitaji.

Msigwa alisema Chadema kimekuwa kinara katika kupinga na kukemea vitendo vya rushwa vinavyosababisha kupatikana viongozi wasiokuwa na ushindani na kusababisha jamii kuhangaika.

"Nitaendelea kukemea ili tupate viongozi wanaotokana na matakwa ya wananchi lalini suala lipo, ndio maana chama kimeonya, siamini katika kutumia rushwa, sihitaji kununua uongozi kwamba nikiukosa nitakufa," amesema Msigwa.

Naye, Sugu amesema:"Siwezi kutumia rushwa kupata uongozi, lakini haya mambo tunayasikia kama ambavyo wewe umeyasikia au mchungaji alivyosikia. Lakini siamini kupata uongozi katika rushwa maana nina vigezo na sifa vya kukubalika.”

"Wapiga kura kwenye kanda wapo 120 ni rahisi kuwafikia kuliko kutumia rushwa, nitakemea na sitoshiriki rushwa," amesema.

Sugu na Msigwa wakiwa na wafuasi wao.

Alichosema mchambuzi kuhusu mdahalo

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Faraja Kristomus akizungumza na Mwananchi Digital, leo Jumapili juu ya mdahalo huo amesema ukiacha changamoto ndogondogo za ubora wa urushaji wa matangazo, mwandaaji wa mdahalo ametenda haki kwa wagombea wote wawili kwa kiasi kikubwa.

“Ni mwanzo mzuri wa kuwapima wagombea na kukuza demokrasia ndani ya vyama na kuwapa nafasi wapiga kura kuwapima wagombea wao kwa sera zao wanazotoa. Lakini pia mdahalo huo unaonesha njia ya kuweza kuboresha zaidi kwenye chaguzi nyingine za ubunge na urais mwakani,” amesema.

Dk Kristomus ameongeza:“Kwa mtazamo wangu, tofauti na wengine wanavyodhani, umekuwa mdahalo muhimu sana na utakinufaisha zaidi Chadema kwani wanachama wanaona kweli demokrasia inakuwa ndani ya chama chao.”

“Sidhani kama mdahalo huo unakibomoa chama bali unakikuza zaidi na wanachama wanapata nafasi ya kuwafahamu vizuri wagombea wao na kuweka uwazi kwenye mchakato wao wa kuwapima viongozi wao,” amesema.

Mhadhiri huyo amesema, kwa siku chache zilizosalia kuelekea uchaguzi, wagombea wamepata nafasi ya kunadi sera zao wakiwa pamoja na wafuasi wao.

“Kama viongozi watakuwa na hekima na busara wataheshimu maamuzi ya wapiga kura na wao kuendelea kubaki wamoja kwa sababu watajua ni wanachama ndiyo walioamua kutokana na jinsi walivyojinadi,” amesema na kuongeza:

“Pia nimeona kuwa wafuasi wa kila mgombea wameweza kupima uwezo wa mgombea wao na kuweza kujiandaa kisaikolojia kwa matokeo yoyote kwenye uchaguzi wa tarehe 29.”

Chanzo: Mwananchi