Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi ndivyo jinsi Samia alivyo 'upiga mwingi' kukutana na Mbowe

039dd5991341b4e54d85a125d29a7a79 Hivi ndivyo jinsi Samia alivyo 'upiga mwingi' kukutana na Mbowe

Mon, 7 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wanasiasa wamesifu uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe Ikulu, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Chama Cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema jana alisema Rais Samia ameonesha ushujaa na utayari wake kushirikiana na wanasiasa katika kuendeleza nchi.

Mrema mkutano huo utaongeza umoja wa serikali na wapinzani katika masala yenye maslahi kwa nchi.

“Rais ameonesha kuwa siasa siyo uadui ila ni kazi inayotakiwa kusikilizana na kusaidiana. Kukutana na Mbowe hakika ni uamuzi mzuri na wenye tija kwa maendeleo na nimtakie kazi njema na aendelee kufanya kazi kwa kushirikiana na wanasiasa hivihivi,” alisema.

Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema Rais Samia ameonesha ukomavu kisiasa na ni hatua nzuri katika kusikilizana na kujadiliana mambo yenye manufaa kwa nchi.

“Wakati akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa vyama vya siasa na Rais Samia mkoani Dodoma Kiongozi Mkuu wa ACT, Zitto Kabwe aligusia suala la kuachiwa kwa Mbowe na hakika kuna kitu kimefanyika na ndiyo mwanzo mzuri wa kuwa na demokrasia ya kweli nchini,” alisema Shaibu.

Katibu Mkuu wa Chama cha Siasa- ADC, Hassan Doyo alisema Rais Samia kaonesha nia ya dhati kuondoa tofauti zenye athari hasi na kudumisha umoja.

Doyo alisema Rais Samia ameonesha uzalendo na nia ya dhati ya kuzika tofauti za kisiasa kati ya serikali na vyama vya upinzani.

Juzi, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) - Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka alisema kwa hatua iliyooneshwa na Mbowe ni siasa safi na ndio Tanzania wanayojivunia kuwa nayo.

“Lengo la CCM katika kipindi hiki ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kupata haki kwa mtu mmoja mmoja na makundi mbalimbali kama ilani yetu ya uchaguzi mwaka 2020-25 inavyosema katika Ibara ya 118," alisema Shaka.

Alisema chama kinampongeza Rais Samia kwa kuendelea kutekeleza maelekezo hayo ya Ilani na kusema kazi inaendelea vizuri.

“Siasa safi ni pamoja na uzalendo, utu, heshima na kuweka mbele maslahi ya taifa kuliko chochote, Rais Samia ni kielelezo katika hili na ameendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuijenga nchi moja yenye ustawi kwa wananchi wote tuzidi kumpa ushirikiano," alisema Shaka.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Tumaini, Tawi la Dar es Salaam, (Tudarco), Rachel Yusuph alisema Rais Samia kaonesha nia ya dhati kuliunganisha taifa la Tanzania licha ya tofauti za kisiasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live