Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi CCM ina madaraja mawili ya wanachama?

69250 Mloto+pic

Thu, 1 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ametoa tamko la kuwashughulikia wana-CCM watakaojadili upepo wa kisiasa unaoendelea. Bashiru anasema mwanachama atakayejifanya kada sana na kujadili “upumbavu wa wapumbavu” atafukuzwa.

Bashiru hakutaja huo upumbavu wala wapumbavu. Nikakumbuka mstari wa mwanajeshi mshairi wa Marekani, Anthony Liccione, unaosema: “Wakati mwingine kucheza upumbavu hufungua macho kuuona ukweli.”

Mstari huo wa Liccione ni ukumbusho kwa Bashiru kuwa mara chache si aghalabu, ndani ya upumbavu hupatikana ukweli. Na watu wazima hawaachi kwa vitisho bali kwa utashi. Wakinyamaza mbele yako kwa hofu, koridoni watanong’ona!

Bashiru hajasema upumbavu ni upi na wapumbavu ni akina nani. Hata hivyo, upepo wa kisiasa ndani ya CCM na nchi kwa jumla, uligeuka baada ya makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana kuandika waraka wenye kujitakasa na tuhuma zinazorushwa kwao na kada wa CCM, Cyprian Musiba.

Kinana na Makamba walitaka Musiba apuuzwe na maneno yake, kwamba wao wamekuwa wakila njama za kumhujumu Rais Magufuli, pia wanataka kumkwamisha asipitishwe na chama kuwa mgombea urais mwakani kwa ajili ya kuendelea na muhula wake wa pili.

Pamoja na kujitenga, Kinana na Makamba, walionyesha wasiwasi wao kuhusu tambo za Musiba na kutochukuliwa hatua.

Pia Soma

Walijenga shaka kuwa Musiba huenda analindwa na watu wenye mamlaka isiyohojiwa, ndio maana kwa kipindi chote amekuwa akituhumu watu, lakini haonywi wala kuchukuliwa hatua.

Musiba amekuwa akijiita mwanaharakati huru na mtetezi wa Rais Magufuli. Tangu mwaka 2017, alianza kutokeza kwenye vyombo vya habari, akitaja majina ya wanasiasa na watu wa kada nyingine kuwa ni hatari kwa nchi na wanamhujumu Rais.

Tangu Musiba aanze kuporomosha tuhuma hizo, hakuna yeyote ambaye alisemwa, amewahi kufikishwa kwenye vyombo vya dola, wala yeye mwenyewe kuulizwa ili atoe ushahidi.

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe ndiye pekee alimpeleka Musiba mahakamani ili athibitishe tuhuma zake. Wengine walikuwa kimya mpaka Kinana na Makamba walipovunja ukimya.

Kuna hoja kuwa mbona Kinana na Makamba hawakuacha suala lao lishughulikiwe kwenye vikao vya chama? Lakini mbona wanaowashambulia wazee hao, hawakuwahi kumjibu Musiba atulie masuala ya chama yashughulikiwe na chama?

Mbona Musiba hakuwahi kuambiwa kuwa kama ana tuhuma za wanachama wenzake CCM aziandike kwa mamlaka za chama ili zipatiwe ufumbuzi ndani kwa ndani badala ya kupayuka?

Hizo mamlaka za chama zilikuwa wapi kuwatetea viongozi wake wastaafu, tena wa ngazi za juu kabisa?

Hatukusikia Bashiru akimwita Musiba afafanue tuhuma hizo, ila Membe ajieleze alivyotuhumiwa.

Wabunge Livingstone Lusinde na Juma Nkamia pia wametokeza kuwasema Kinana na Makamba. Ongeza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi na Hussein Bashe. Hivi CCM ya siku hizi watu hawaruhusiwi kujitetea wakishambuliwa?

Kosa la Kinana na Makamba ni kusema wanasingiziwa na Musiba au kutamka kuwa Musiba analindwa na mamlaka isiyohojiwa? Hivi, kuwashambulia badala ya kutafakari malalamiko yao, si kuthibitisha maneno yao kuwa Musiba analindwa?

Je, Musiba ana kadi ya CCM daraja A? Kwamba anaruhusiwa kutuhumu yeyote na wale daraja B ni marufuku kujitetea?

Mwandishi wa Uingereza, China Mieville, kupitia kitabu chake cha “King Rat”, anasema: “Mtego ni mtego kama huujui. Ukishaujua si mtego, bali changamoto.

“Sasa basi, Kinana na Makamba wanavyoshambuliwa ni kipimo kuwa waraka wao umefanikiwa na umepenya. Mtego wameshaujua, kilichobaki mbele yao ni changamoto.

Chanzo: mwananchi.co.tz